Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mayele, Sakho wapewa dili bara

Mayelee Pic Data Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele

Fri, 8 Oct 2021 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Bara imeshachezwa mechi za raundi mbili hadi sasa, huku wachezaji kadhaa wakianza na moto na kuanza kutajwa midomoni mwa wadau wa soka, lakini nyota wa Simba, Yanga na Azam wakipewa akili ya kuweza kwenda na kasi ya ligi hiyo.

Wachezaji wanaotajwa mara kwa mara na mashabiki ni Khalid Aucho (Yanga), Fiston Mayele (Yanga), Feisal Salum ‘Fei Toto’ (Yanga), Meddie Kagere (Simba), Ousmane Sakho (Simba) na Sadio Kanoute (Simba) ambao wamekuwa na mwanzo mzuri katika vikosi vyao, lakini wakaopewa akili ya kuongeza ukali watishe zaidi.

Aliyekuwa mtambo wa kuzalisha mabao wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ alisema kuanza kwao vizuri, kunawafanya watazamwe zaidi katika majukumu yao endelevu, hivyo aliwataja kuongeza bidii ya mazoezi.

“Wajitahidi kuwa wabunifu kila wanapopata nafasi ya kucheza, kwani tayari wapinzani wao wanakuwa wamewasoma uchezaji wao, hilo liwape funzo namna wanavyochukuliwa kwa ukubwa, kwa kuwa wachezaji wenzao nao wanataka kung’ara,” amesema.

Mmachinga anayeshikilia rekodi ya mabao mengi (26) katika msimu mmoja alifanya hivyo katika Ligi Kuu mwaka 1999, alisema mastaa hao na wengine waliopo Azam na klabu nyingine waepuke kuridhika mapema, kwani kadri majina yao yanavyokuwa makubwa ndivyo wanavyotakiwa kuonyesha kazi kubwa uwanjani.

Kauli yake iliungwa mkono na Idd Moshi ‘Mnyamwezi’ aliyesema kuanza kwao vizuri, kutawafanya kukumbana na changamoto ya kutazamwa kwa jicho makini wakati wa kutimiza majukumu yao uwanjani.

“Wajitahidi kulinda viwango vyao kwa kuzidisha mazoezi ya kuwaweka fiti na wawe wanaangalia mastaa wa Ulaya wanafanya vitu gani vinavyowapa ubora,” amesema.

Frank Kasanga ‘Bwalya’ beki wa zamani wa Simba, alisema muendelezo wa viwango vyao ndio utawapa heshima mwisho wa msimu, akiwataka waweke akili zao kwenye kazi na siyo kulewa sifa za mashabiki.

“Zamani ulikuwa ukipata jina kubwa ilikuwa kama umepewa mtihani wa kutunza kiwango chako, ndicho wanachotakiwa kukifanya wachezaji wa sasa ambao wanafanya kazi kwenye mazingira mazuri ya kiuchumi,” amesema.

Alisema wachezaji hao wanatajwa kulingana na walichokifanya kwenye mechi hizo, hivyo aliwataka kutambua wanapendwa kwa ajili ya kazi, kinyume chake wakifanya hivyo watazomewa.

Chanzo: Mwanaspoti