Wakati Ligi Kuu ikitarajia kuendelea wikiendi hii, kinara wa mabao Fiston Mayele mwenye mabao 14 na chama lake linajiandaa kuikabili Ihefu kwenye mchezo utakaopigwa Jumatatu, Uwanja wa Mkapa, pamoja na kwamba ana takwimu kali, lakini kuna sehemu John Bocco kamchakaza.
Hata hivyo, katika mabao 14 aliyofunga Mayele, mabao tisa amefunga kwenye michezo tisa ya nyumbani sawa na wastani wa bao moja kwa kila mchezo, huku mabao matano akifunga katika michezo 10 ya ugenini wastani wa kila michezo miwili bao moja.
Katika mabao 14, mabao aliyofunga kipindi cha kwanza ni saba sawa na mabao aliyofunga kipindi cha pili tofauti na msimu uliopita alikuwa mwiba zaidi kipindi cha kwanza.
Msimu uliopita Mayele hadi kufika Januari 15 ukiwa mzunguko wa pili umeanza, alikuwa na mabao sita, wakati msimu huu hadi sasa tayari amefunga mabao 14, ikiwa ni mara mbili ya msimu uliopita.
Moses Phiri kinara wa mabao kwenye kikosi cha Simba mwenye mabao 10 ambaye anamfukuzia Mayele katika kusaka kiatu cha ufungaji bora ambacho msimu uliopita alichukua, George Mpole (Geita) kwa mabao 17 naye mkali zaidi nyumbani.
Phiri katika mabao 10, mabao sita amefunga uwanja wa nyumbani wakati manne akifunga ugenini na katika mabao 10, sita amefunga kipindi cha kwanza na manne kipindi cha pili, aliyofunga ugenini.
John Bocco anayeshika nafasi ya tatu katika orodha ya wafungaji hadi sasa kwa mabao yake tisa, yeye ameonekana kuwa mkali zaidi ya Mayele na Phiri ugenini akifunga mabao sita na nyumbani mabao matatu.
Mabao matatu ya nyumbani ya Bocco ni yale aliyofunga kwenye ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Tanzania Prisons ikiwa hat trick yake ya pili baada ya ile ya kwanza kwenye ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Ruvu Shooting.
Mchezaji wa zamani wa Taifa Stars na Yanga, Bakari Malima 'Jembe Ulaya' alisema kufunga kipindi cha kwanza kwa washambuliaji wengi hiyo ni mbinu ambayo makocha wengi huitumia kwa kuhakikisha kipindi cha kwanza wanapata bao.
"Kuhusu kufunga nyumbani hilo ni jambo la kawaida kwa washambuliaji na hata timu kuwa nyumbani inakuwa na asilimia kubwa kushinda kuliko ugenini," alisema Malima.
Rekodi ya mabao mengi kwenye Ligi Kuu Bara inashikwa na Mohamed Hussein "Mmachinga" (Yanga) ya mabao 26 aliyoiweka mwaka 1997, anayemfuata ni Abdallah Juma (Mtibwa Sugar) mabao 25 mwaka 2005 kisha, Meddie Kagere (Simba) mabao 23 msimu wa mwaka 2018-19.