Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Fiston Kalala Mayele ametangaza mapema Kiu ya kulipa Deni la kumaliza msimu akiwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu 2022/23.
Mayele alimaliza nafasi ya pili nyuma ya Mshambuliaji Mzawa George Mpole wa Geita Gold FC aliyeibuka Kinara wa ufungaji Bora msimu wa 2021/22, akifunga mabao 18.
Mayele amesema amejiandaa vizuri kuelekea msimu ujao, ili aweze kuisaidia timu yake kupata matokeo mazuri, pia kuhitimisha lengo la kuwa kinara wa Ufungaji Bora.
Amesema msimu uliopita alidhamiria kumaliza katika nafasi ya kwanza, lakini bahati haikuwa kwake, hivyo ameichukua hiyo kama changamoto inayomuongezea juhudi ya kujiandaa vizuri kuelekea msimu ujao.
“Nimejiandaa vizuri kwa ajili ya msimu mpya (2022/2023), nitahakikisha naonyesha makali ili nifunge mabao mengi ambayo yatanipa nafasi ya kushinda kiatu cha ufungaji bora”
“Msimu uliopita haukuwa wa bahati kwangu, nina imani msimu ujao nitakua na wakati mzuri wa kuisaidia timu yangu na kumaliza katika nafasi ya kwanza katika ufungaji, Mashabiki nawaomba waendelee kuwa na imani na timu yetu na watupe ushirikiano wa kutosha.” amesema Mayele