Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mayele, Mpole na Sopu wametufikirisha

Mayele Fiston Score Fiston Mayele

Tue, 5 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ndio! Msimu wa soka ndio umetamatika. Yanga imeanza msimu kwa kubeba Ngao ya Jamii. Kisha ikatwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Jumamosi ikamalizia kwa kuchukua Kombe la ASFC au Waingereza wanasema ‘treble’.

Yapo mambo mengi ambayo yametokea msimu huu, lakini ambalo limeimbwa kutoka mwanzo hadi mwisho ni ‘kutetema’ au kwa maana nyingine jina la mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele.

Kutetema ni staili yake ya mwisho katika kifurushi chake cha kushangilia bao. Huanza kwa kunyoosha mkono wa kushoto, na baadaye kutumia mkono wa kulia kupiga mara nne sehemu ambayo huvaliwa saa na kumalizia kwa kusukuma kichwa mbele kama mchezaji anayepiga kichwa mpira. Hufanya hivyo mara mbili na kumalizia kwa kutingisha mabega na kusukuma tena kichwa mbele, au kutetema.

Ndivyo alivyofanya kila alipofunga bao na hivyo staili hiyo kuenea kwenye kila kona ya nchi, achilia mbali katika hafla, makanisani na sehemu nyingine zenye mikusanyiko. Na hivyo, mashabiki wa Yanga walitaka kuona ushangiliaji huo ukifanyika katika kila mechi, yaani wamuone Mayele akifunga na baadaye kushangilia kwa staili hiyo.

Nje ya uwanja ukawa mjadala wa Mayele. Wenye kukejeli na wenye kumtetea. Wengine wakisema ni mshambuliaji wa kawaida na wengine wakisema si kawaida na ndio maana anajadiliwa. Amewafurahisha hivyo Wanayanga na wengine mara 16 kwenye Ligi Kuu na mara nyingine kwenye mechi za mashindano mengine kama Ngao ya Hisani na Kombe la Azam.

Mijadala hiyo ilifunika kabisa uwezekano wa mashabiki na wachambuzi kujadili washambuliaji wengine. Na kwa kweli, wakati mjadala wa ushangiliaji huo ukizidi kupamba moto ndipo ilipogundulika kuwa aliyekuwa akiongoza kwa ufungaji alikuwa Reliant Lusajo na baadaye George Mwaigomole Mpole akaibuka hadi kumaliza akiwa mfungaji bora.

Uliza leo hii, nani anaelewa ustadi wa Mpole katika ufungaji? Ni wachache sana. Hata baadhi ya wale wachambuzi wanahitaji muda kuchungulia mabao yake YouTube kabla kujitokeza hadharani kumzungumzia. Kulikuwa na dhahabu juu ya udongo ambayo wachache waliiona.

Na hata Lusajo alipopoteza shabaha yake ya ufungaji haikuonekana tatizo kama pale Mayele aliposhindwa kufunga, achilia mbali kazi aliyoifanya kwenye mechi. Tangu Lusajo alipofunga bao la 10 hajaonekana wala kujadiliwa kwamba amekumbwa na kitu gani hadi anaondoka na ‘clean sheet’ nyingi.

Yupo pia Abdul Suleiman ‘Sopu’, kijana aliyeanzia timu ya taifa ya vijana walio na umri chini ya miaka 17 na baadaye kwenda Simba kabla ya kuazimwa Coastal Union.

Jumamosi alionyesha watu kuwa alistahili kuangaliwa wakati wote msimu huu hata kama amemaliza na mabao saba tu. Ni dhahiri kwamba Simba walikuwa wakimfuatilia kwa sababu ni mchezaji wao, lakini wengine walimuona katika mechi dhidi yha vigogo wa Kariakoo tu.

Kitendo cha kutundika mabao matatu katika mechi ya fainali ya ASFC kinafanya awe mshambuliaji wa pekee na nadra katika soka, lakini hakupata nafasi katika mijadala labda kwa kuwa alikuwa Coastal. Kumbuka Allan Shearer wakati wote alikuwa Blackburn Rovers na Newcastle United tu, licha ya Manchester United, Arsenal, Liverpool kuwa ndio vigogo wa enzi zake. Hii ni mifano michache inayoonyesha kuwa kuna hazina kubwa ambayo haitupiwi macho, labda kutokana na ukubwa wa Simba na Yanga au kutokana na ile imani kuwa ili uonekane unajua mpira ni lazima uzungumzie Simba na Yanga tu ndipo usikilizwe.

Wapo wengine wengi ambao majina yao yangeweza kutawala mijadala ya soka msimu huu kama wadau wangekuwa makini na wenye kutaka kuchambua soka kwa dhati.

Chanzo: Mwanaspoti