Fiston Mayele na Henock Inonga wamechaguliwa katika kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo kinachojiandaa na mechi za kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazochezwa baadaye mwezi huu.
Kiwango kizuri kilichoonyeshwa na nyota hao hasa katika mashindano ya klabu Afrika bila ya shaka kimechangia kwa kiasi kikubwa kuchaguliwa kwa wawili hao kwenye kikosi hicho cha DR Congo ambacho kimejaa kundi kubwa la nyota wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya.
Katika mechi tatu za hatua ya kaundi za Ligi ya Mabingwa Afrika, Henock Inonga ndiye aliyeifungia Simba bao pekee ililonalo hadi sasa wakati kwa upande wa Yanga, kati ya mabao manne iliyopachika hadi sasa, Mayele amefunga moja na kupika lingine moja.
Pengine kama sio uwepo wa Simba na Yanga katika hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika, kungekuwa na nafasi finyu kutokana na uwepo wa kundi kubwa la wachezaji wenye majina makubwa na wanaocheza katika ligi mbalimbali barani Ulaya lakini hata hivyo benchi la ufundi la DR Congo likawaona Inonga na Mayele.
Mwanaspoti inakuletea orodha ya nyota wa DR Congo ambao licha ya kucheza katika ligi mbalimbali za Ulaya na wana majina makubwa, wamejikuta wakiwekwa kando na nafasi zao kuchukuliwa na Mayele na Inonga.
Licha ya uzoefu mkubwa alionao, nyota wa Al Ittifaq ya Saudi Arabia, Marcel Tisserand anayecheza nafasi ya beki wa kati, ameachwa huku Inonga akiwepo.
Kabla ya kuchezea Al Ittifaq, Tisserand amewahi kuzitumikia Lens, Monaco, Wolfsburg, Toulouse na Fenerbahce.
Christian Luyindama
Nyota wa zamani wa timu za Galatasaray, Standard Liege na Al Taawon ambaye kwa sasa anaitumikia Antalyaspor, Christian Nekadio Luyindama naye hakuweza kujumuishwa katika kikosi cha DR Congo kilichoitwa hivi karibuni ambacho kimemjumuisha Inonga anayecheza naye katika nafasi moja ya beki wa kati.
Chris Mavinga
Inonga hajatamba mbele ya Tisserand na Luyindama pekee bali kuna nyota wengine wanaocheza nafasi yake ambao hawajaweza kulishawishi benchi la ufundi la DR Congo kuwajumuisha mbele yake.
Miongoni mwa nyota hao ni Chris Mavinga anayecheza nafasi ya beki wa kati katika timu ya Los Angeles.
Dieumerci Mbokani
Mkongwe na nahodha wa DR Congo, Dieumerci Mbokani licha ya kucheza soka la kulipwa Ubelgiji katika timu ya SK Beveren, hakupata fursa ya kuchaguliwa kikosini mbele ya Fiston Mayele.
Mbokani amewahi kuzichezea Anderlecht, Monaco, Wolfsburg, Dynamo Kiev na Norwich.
Ben Malango
Hakukuwa na nafasi ya Ben Malango anayeichezea Qatar SC ya Qatar kuitwa mbele ya Mayele licha ya wasifu mkubwa ambao nyota huyo wa zamani wa Raja Casablanca na Sharjah SC anao
Meschack Elia
Nyota wa zamani wa TP Mazembe ambaye kwa sasa anaitumikia Young Boys ya Uswisi, Meschack Eliya naye hakupata nafasi ya kuchaguliwa kikosini mbele ya Mayele anayechezea Yanga.