Baada ya kufunga hat trick ya kwanza Ligi Kuu Bara msimu huu, mshambuliaji namba moja wa Yanga, Fiston Mayele ametamba kuwa sasa gari limewaka na lilikuwa ni suala la muda kwake kufunga.
Mayele ambaye amecheza dakika 630 kwenye mechi tisa akikosekama dhidi ya KMC, mara ya mwisho aliifunga Mtibwa Sugar kwenye ushindi wa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Juzi ameibuka upya baada ya kuifungia timu yake mabao matatu ‘Hat trick’ kwenye ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Singida Big Stars mchezo uliopigwa uwanja wa Mkapa na kuisaidia timu kukusanya pointi tatu zilizowarejesha kileleni.
“Nimepitia kipindi kigumu kukaa bila kufunga nawashukuru wachezaji wenzangu na benchi la ufundi kwa kuniamini na kunipa moyo kuwa wanaimani na mimi niendelee kupambana nitafunga hatimaye nimefanya hivyo,” alisema na kuongeza:
“Kufunga ndio kazi yangu lakini suala la kukaa muda bila kufunga lilinipa wakati mgumu sana nashukuru nimefunga mabao matatu, ambayo ni mimi pekee hadi sasa nimefunga kwenye mechi moja hadi sasa.”
Mayele alisema alikuwa anatambua kuwa lilikuwa ni suala la muda kwake kufanya hivyo kwasababu ndio kazi yake lakini alikuwa anaumizwa na maneno ya mashabiki kwamba amefikisha mwezi bila kufunga kwake ilikuwa inampa wakati mgumu.
“Nafurahi mwanangu amekuja na baraka zake, mke wangu amejifungua Jumanne mimi nimefunga Alhamis bao la kwanza lilikuwa ni zawadi kwa mwanangu na ndio maana nimeshangilia kwa mfano wa kumbembeleza na mawili nimetetema ili kuendeleza kutetema baada ya muda mrefu,”
“Suala la mwendelezo wa kufunga litategemea na nafasi kama ilivyotokea kwa Singida United nimefunga, nitafanya hivyo kwa timu nyingine kuhusu vita ya ufungaji ni mapema saana mimi kuzungumzia hilo tusubiri mwisho wa msimu.”
Mayele alisema hayupo kwaajili ya kushindana na mpinzani wa timu nyingine au mchezaji aliye kwenye kikosi cha Yanga anachoangalia sasa ni kuona timu yake inapata matokea na inafikia malengo ya kutetea ubingwa.
Mabao aliyoyafunga mshambuliaji huyo yamefanya afikie vinara wa mabao kwa wachezaji wa kigeni Moses Phiri (Simba) na Idris Mbombo (Azam FC).
Meneja wa Yanga, Walter Harrison alisema baada ya ushindi dhidi ya Singida United timu imeshasahau matokeo na sasa inajiandaa na mchezo dhidi ya Dodoma Jiji utakaochezwa Jumanne mjini Singida.
Kwenye msimamo wa mechi za ugenini msimu huu, Yanga imecheza tano na kushinda zote huku Dodoma ikishinda moja tu nyumbani kati ya nne.