Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imefanya uteuzi wa wachezaji watano kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC).
Tuzo hiyo haikuwa na majina ya wanaowania, wakati tuzo nyingine za TFF zilipotangazwa wiki iliyopita na hiyo ilitokana na kusubiri mchezo wa Nusu Fainali ya pili ya Kombe la ASFC kati ya Yanga na Singida Big Stars uliochezwa Jumapili iliyopita na Yanga kuibuka na ushindi wa goli 1-0.
Kwenye taarifa yao iliotolewa jioni ya leo, wachezaji walioteuliwa kuwania tuzo hiyo na majina ya timu zao katika mabano ni nahodha wetu Bakari Mwamnyeto, mshambuliaji Fiston Mayele na Clement Mzize (Yanga).
Wachezaji wengine ni Prince Dube na Abdul Suleiman Sopu wote kutoka Klabu ya Azam ambapo timu hizo mbili zitakutana katika fainali ambayo bado haijapangiwa tarehe.