Shirikisho la Soka Afrika (Caf), limetangaza timu na wachezaji kadha wa kadha wanaowania tuzo za Afrika.
Hizo ni tuzo za ubora barani Afrika, Tanzania imeingia kupitia Yanga kama klabu kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania.
Kabla kama Tanzania tulikuwa tuna rekodi ya kuwa na klabu iliyoivua ubingwa klabu bora ya Afrika pia bingwa wa Afrika.
Hii ilikuwa mwaka 2003, wakati Simba ilipofanikiwa kuwafunga kwa mikwaju ya penalti, Zamalek ya Misri tena jijini Cairo.
Baada ya hapo, hakukuwa na timu yoyote ya Tanzania iliyozungumzwa na kuhusishwa na suala la ubora wa Afrika au vinginevyo.
Yanga wameingia katika tuzo safari hii wakiwa wamefanikiwa kuingia fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita lakini wakapoteza dhidi ya USM Alger ya Algeria.
Kupoteza kwao kulikuwa kwa mapambano hasa kwa kuwa Yanga walifungwa jijini Dar es Salaam lakini wakaenda kushinda ugenini Algers, kanuni ikawaondoa.
Maana yangu wamepoteza lakini haikuwa kinyonge hivyo. Hii imechangia kwao kuingia katika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho na mwisho Watanzania wamefanikiwa kuona kweli hilo halikuwa ni Kombe la Walioshindwa kama ambavyo baada ya watu walikuwa wakisema kutaka kudhihaki na kuonyesha michuano hiyo haina dhamani.
Imewafanya leo Yanga wanaonekana Afrika, wanaitangaza Tanzania na hakuna ubishi sasa Tanzania wanaweza kutembea wakijidai kwa kuwa na timu mbili ambazo zinasumbua Afrika tofauti na misimu sita mfululizo, walikuwa ni Simba pekee.
Wakati Yanga wanafanikiwa kuwania tuzo ya klabu bora Afrika, pia imefanikiwa kuwatoa wachezaji wawili kuwania tuzo.
Djigui Diarra anawania tuzo ya kipa bora, huyu ni mchezaji wa timu ya taifa ya Mali na Fiston Mayele, yeye anawania tuzo ya mshambulizi bora Afrika, huyu ni raia wa DR Congo.
Hujanisikia nikilizungumzia hili kwa muda mrefu lakini ni kutokana na namna ambavyo mambo yamekuwa yakienda. Sivutiwi sana kuona nafasi ambazo wangeweza kuzipata wachezaji Wazalendo zinakwenda kwa wageni.
Kipa alipaswa kuwa mzawa, kama angekuwa ni Msherry au Metacha lingekuwa jambo zuri zaidi na ninatammani kuona hili linatokea.
Kwa upande wa washambulizi, sisemeni ninambagua Mayele, lakini badi nasisitiza, ingekuwa kwa mchezaji Mtanzania, basi lingekuwa ni jambo zuri zaidi kwa maana ya taifa letu kama ambavyo unaona pale inapoonekana Yanga, kunakuwa kuna bendera ya Tanzania.
Wanapoonekana Mayele na Diarra kunakuwa na bendera ya DRC na Mali. Najiuliza kama hii inawaumiza wachezaji wazawa. Isije ikawa mimi ndio nafikiria tofauti au nakerwa wakati wao wanaona ni sawa tu!
Lazima kuwa na wivu wa amendeleo kwa kuwa mafanikio aliyokusanya Mayele, leo analipwa mamilioni ya fedha huko Misri na anawania tuzo lakini mafanikio aliyopata Diarra, yote wameyapatia Tanzania.
Sasa kama wao wanaweza kupatia hapa Tanzania, vipi wazawa washindwe kuzipata hizi nafasi? Lazima mkubali, ndani yenu kuna udhaifu, hamtaki kujituma, hamtaki kupambana na hamko tayari kuukabili ushindani.
Kama vitakuwa ni visingizio kuwa hapa nyumbani mnabaniwa, basi pambaneni mpate nafasi nje na mwisho mcheze kwa mafanikio na siku nyingine tusikie mkiwania tuzo za Afrika na kadhalika kutoka katika timu za nje ya Tanzania.
Mayele na Diarra wameweza kuitumia Tanzania vizuri, lakini wenye Tanzania yao wala hawana habari. Mnapaswa kuinua vichwa vyenu mtazame mbele sahihi.
Wakati huu Simba na Yanga wanafanya vizuri, ni nafasi nzuri sana kuwaona wachezaji wengi wa Tanzania nao waking’ara kutumia nafasi ya timu zao.
Timu sasa ziko katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Isiwe mwisho, wachezaji wa DRC, Mali, Zambia, Msumbiji ndio wakawa na faida kubwa katika timu zao za taifa hadi kwenye michuano ya Afcon na Watanzania, wakaendelea kuwafaidisha wengine kupitia klabu zao. Hii si sawa.