Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mayele, Chama uso kwa uso na Taifa Stars Afcon 2023

Mayele X Chama Mayele, Chama uso kwa uso na Taifa Stars Afcon 2023

Fri, 13 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kama watakuwemo kwenye vikosi vya timu zao za taifa vitakavyoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwakani huko Ivory Coast, Fiston Mayele na Clatous Chama watacheza dhidi ya marafiki zao watakaokuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'.

Hiyo ni kufuatia timu zao za taifa, Zambia na DR Congo kupangwa kwenye kundi moja na Taifa Stars katika fainali hizo zitakazoanza Januari 13 hadi Februari 11 huko Ivory Coast.

Katika droo iliyochezeshwa jana saa 4 usiku huko Abidjan, Ivory Coast, timu hizo tatu zimepangwa katika kundi F sambamba na Morocco.

Timu hizo zote tatu zilizopangwa na Taifa Stars katika kundi F, zina historia kubwa ya kutamba katika fainali hizo ambapo zote zimewahi kutwaa taji la Afcon kwa nyakati tofauti.

Morocco 'Simba wa Atlas' ni mabingwa wa Afcon mwaka 1976 na mwaka uliopita walitinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia huko Qatar.

Zambia 'Chipolopolo' imewahi kutwaa taji la Afcon mara moja ambayo ni mwaka 2012 lakini wamewahi kumaliza katika nafasi ya pili mwaka 1974 na 1994.

DR Congo nao wamekuwa sio wanyonge katika Afcon kwani wamewahi kutwaa taji mara mbili ambazo ni 1968 na 1974.

Kundi A la mashindano hayo mwakani litakuwa na wenyeji Ivory Coast, Nigeria, Guinea ya Ikweta na Guinea Bissau wakati kundi B lina timu za Misri, Ghana, Cape Verde na Msumbiji.

Mabingwa watetezi Senegal wao wamepangwa kundi C pamoja na Cameroon, Guinea na Gambia na kundi litakuwa na Algeria, Burkina Faso, Mauritania na Angola.

Majirani wawili wa Kusini mwa Afrika, Afrika Kusini na Namibia wamepangwa katika kundi E pamoja na tai wa Kaskazini mwa Afrika, Tunisia na Mali ya kipa wa Yanga, Djigui Diarra

Chanzo: Mwanaspoti