Wakati Yanga ikishuka ugenini mjini Tunis kukabiliana na US Monastir katika mechi ya kwanza ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika, kuna kitu kikubwa wamefanya matajiri wao wa GSM kwa kuwatengea nyota wa timu hiyo wakiongozwa na Fiston Mayele na Stephane Aziz Ki mamilioni ya fedha kama kuwatia mzuka mbele ya Watunisia.
Yanga na Monastir zitavaana kuanzia saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki sawa na saa 10:00 jioni za Tunis ikiwa moja na mechi mbili za kundi hilo, nyingine ikzikitanisha TP Mazembe ya DR Congo na Real Bamako ya Mali.
Katika kuhakikisha Yanga inaanza na mguu wa bahati wa kushinda ugenini kabla ya kurudi nyumbani kuisubiri TP Mazembe kwenye mchezo ujao wa kundi hilo, matajiri wa Yanga kupitia Rais wa klabu, Injinia Hersi Said wameshtukia kitu katika kutimiza malengo yao kwenye mechi za makundi kwa kutaka kuona timu inapata walau pointi moja katika mchezo huo na mingine miwili ya ugenini kwa kweka bonasi ya maana.
Tofauti na siku za nyuma, mzigo ulikuwa ukiwekwa zaidi kwenye kusaka ushindi, Yanga imeamua kuwapa ofa kina Mayele na wenzake kwa kupambana ili kupata japo sare ambayo itawapa noti za kutosha, ikiwa ni moja ya mikakati yao kwenye mechi za CAF.
Hata hivyo, bado bonasi kubwa itabaki kuwa ile ya ushindi, huku vigogo hao jana jioni walitarajia kukutana na wachezaji katika kikao cha mwisho na kuwatamkia viwango halisi.
Kabla ya hata ya kutamkiwa hilo ujumbe huo tu ukawafanya wachezaji kuongeza morali ya juu katika kambi yao na hata mazoezini kila mmoja akionekana kupambana kutafuta nafasi ya kucheza mechi hiyo.
Hersi aliliambia Mwanaspoti, lengo la bonasi hizo mpya ni kuhakikisha wachezaji wanautafuta ushindi, lakini hata wakikosa basi waambulie japo pointi moja ugenini ambazo zitakuwa msaada mkubwa kwenye mikakati yao ya kuvuka hatua hiyo kwenda robo fainali.
"Hizi ni mechi za makundi ambazo unavuka kwa kukusanya pointi nyingi kwa ujumla wake katika mechi sita mnazocheza, hatupo tena kwenye mtoano, ili tufikie malengo yetu ya kucheza hatua ya robo fainali tunataka hata tukikosa pointi tatu basi tuipate moja," alisema Hersi.
"Tangu tumewapa mpango huu na hata nilipofika hapa Tunisia, nataka niwahakikishie Wanayanga kwamba morali iko juu sana bila kujali changamoto ya hali ya hewa ya baridi kali ambayo wachezaji wetu wamekutana nayo hapa."