Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mayele: Al Hilal lazima afe

Mayele 2 Fiston Mayele

Wed, 28 Sep 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Staa kipenzi cha mashabiki wa Yanga, Fiston Mayele amewahakikishia kwamba anawajua vizuri Al Hilal na iwe Jua au Mvua hawatoki Kwa Mkapa Oktoba 8.

Akizungumzia mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa, Mayele alieleza namna Yanga inavyopania mchezo wao hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan na marudiano Oktoba 14 Sudan.

Alisema kwamba wanajua umuhimu wa mchezo huo na kila mchezaji ana kiu kubwa ya kuwang'oa Hilal na kutinga hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuikosa muda mrefu.

Alisema wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wote wa Yanga mpango wao mkuu ni kuhakikisha wanashinda mechi ya nyumbani kwa Mkapa akiamini itawapa mwanzo mzuri kabla ya mechi ya marudiano huku akitumia msemo wa 'Iwe mvua, iwe jua'.

"Iwe mvua Iwe jua, ushindi ni lazima katika mchezo wa nyumbani, kwa upande wa timu tumejipanga na tunaendelea kujiweka vizuri zaidi na tunaamini hilo litatimia kwani ni ndoto ya kila mchezaji kusonga mbele," alisema Mayele aliyefunga mabao  sita, 'hattrick' mbili kwenye mechi mbili za kwanza Yanga ikiiondosha Zalan ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 9-0.

Mayele pia ameeleza kuwafahamu vyema Al Hilal kuanzia kwa kikosi, kocha mkuu Frolent Ibenge aliyewahi kumfundisha AS Vita na mashabiki wake huku akiwatoa wasiwasi mashabiki wa Yanga juu ya mechi dhidi yao na kubwa zaidi akiwataka wajae uwanjani siku ya mechi.

"Nilifuatilia mechi yao ya kwanza dhidi ya Saint George ya Ethiopia lakini pia nawajua baadhi ya watu ndani ya timu ile, wako bora uwanjani pia nje wana mashabiki wenye mzuka wa aina yake hivyo kama Yanga tukiungana tunaweza kuwashinda." Hilal iliitoa St.George kwa sare mabao 2-2 ikiwa na faida ya bao la ugenini.

"Mashabiki kwetu ni mchezaji wa 12, kila Mwanayanga siku hiyo aje uwanjani, watupe sapoti kwa kadri wawezavyo na sisi uwanjani tutakuwa tunapambana kuhakikisha tunawafurahisha na kutanguliza mguu mmoja mbele kabla ya marudiano,"alisema.

Mshambuliaji huyo mwenye mabao matatu hadi sasa kwenye Ligi Kuu ndani ya mechi nne ukiwa ni msimu wake wa pili  baada ya uliopita kucheka na nyavu mara 16 nyuma ya kinara George Mpole wa Geita Gold aliyefunga 17, ameelezea kasi yake ya upachikaji mabao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kueleza kama atapata nafasi atafunga sana.

"Ujue ubora wangu unategemeana na ushirikiano mkubwa ninaoupata kwa wachezaji wenzangu, tuna timu nzuri naamini na kama nitajitahidi kutumia vyema kila nafasi timu itafikia malengo na mimi natimiza ndoto zangu," alieleza.

Kabla ya kuwavaa Hilal, Oktoba 3 mwaka huu itajitupa uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye muendelezo wa ligi hiyo itakapoivaana Ruvu Shooting.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz