Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mayay ajitosa ishu ya Mdamu

Mdamu Pic Data Mayay ajitosa ishu ya Mdamu

Mon, 9 Aug 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

HALI ya Gerrard Mdamu aliyepata ajali akitoka mazoezini na wachezaji wenzake wa Polisi Tanzania na kuvunjika miguu yote, limemgusa nyota wa zamani wa kimataifa na mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay aliyelifikisha suala la mchezaji huyo kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba.

Kaka na Mdamu, Benedictor Mdamu aliliambia Mwanaspoti jitihada za Mayay zimelifanya suala la mchezaji huyo kufika kwa Mwigulu ambaye mbali ya kuwa kiongozi wa kisiasa, ila ni mwanamichezo pia.

“Wakati Mayay alipomtembelea hospitali aliguswa kwa kiasi kikubwa na kutoa pendekezo la kumshirikisha Nchemba ili kuzidi kuweka nguvu kwa ajili ya kuhakikisha dogo anarejea katika hali yake ya kawaida,” alisema Benedictor, huku Mayay akikiri ni kweli walifanya jitihada za kuwasiliana na Mwigulu ili kupata msaada zaidi kwa wadau wa soka lengo ni kumsaidia Mdamu aweze kurejea maisha yake ya kila siku.

“Ni kweli nilizungumza na Nchemba kwa kuwa ni mdau mkubwa wa michezo nchini na hata yeye aliguswa na kuahidi kushiriki katika kutoa msaada wa matibabu ya Mdamu ili kumwona hata kama hatocheza mpira ingawa sitamani kuona hilo likitokea ila anarejea katika hali yake ya kawaida,” alisema.

Aidha Mayay alisema alishirikiana na viongozi wa Polisi Tanzania ambao ndio wamiliki wa mchezaji na kupeana ushauri mbalimbali kuhusu tukio hilo na kufurahishwa na muitikio mkubwa wa wadau wa soka nchini jinsi walivyolichukulia.

“Tuliongea na Makamu Mwenyekiti wa Polisi FC, Robert Munisi na wadau wengi wa michezo nchini ambao hawakutaka kutajwa majina yao hadharani ila kwa kiasi kikubwa walitoa michango yao juu ya matibabu ya Mdamu na kuahidi kuendelea kuonyesha ushirikiano mpaka mwisho,” alisema.

Daktari wa timu ya taifa, Taifa Stars Emily Urassa, ndiye anayemhudumia mchezaji huyo alikaririwa na Kaka yake Mdamu ‘Benedictor’ akisema suala la mchezaji huyo lipo mikononi mwao na hawaoni sababu ya kumpeleka nje ya nchi kwa sasa.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz