Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mayanga atawajibu kwa vitendo

Salum Mayanga Mkataba Mayanga atawajibu kwa vitendo

Thu, 28 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati wadau na mashabiki wa Mbeya City wakiamini chama lao litarejea Ligi Kuu Bara, kocha mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga amesema hawezi kuahidi kwa maneno kwani mpira siyo ahadi bali uhalisia ni vitendo.

Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu uliopita inaendelea kujifua kwa ajili ya mchezo wake dhidi ya Fountain Gate Academy Tallents utakaopigwa Desemba 30 jijini hapa ukiwa wa kumalizia mzunguko wa kwanza wa Championship.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kumuaga aliyekuwa mtendaji mkuu wa timu hiyo, Emanuel Kimbe na kuukaribisha uongozi mpya, Mayanga alisema Championship ni ligi ngumu ambayo inahitaji kupambana.

Alisema pamoja na matumaini na matarajio ya kuipandisha tena timu hiyo,, lakini hawezi kuahidi kwa maneno kwani mpira ni uhalisia wa vitendo akiomba ushirikiano wa ndani na nje ya uwanja ili kufikia malengo.

“Sikuwa tayari kufundisha timu ya Championship, lakini niliheshimu wito wa Kimbe. Niseme malengo yangu ni kuona Mbeya City inarudi Ligi Kuu, lakini siyo ahadi ya mdomo. Ligi ni ngumu inahitaji ushirikiano wa pamoja, mpira ni uhalisia,” alisema Mayanga.

Kimbe alisema pamoja na mafanikio kwa timu hiyo, lakini anatamani kuona City ikirejea Ligi Kuu akiomba uongozi mpya kupambana kupata wawekezaji kwa kuwa mpira ni pesa.

“Mpira ni pesa, uchumi, fursa na ajira. Mimi napumzika kwa muda lakini sitafurahi kusikia uongozi mpya ukilalamikiwa kwa namna yoyote kutokana na timu kufungwa, lazima tuwe tayari kwa matokeo yoyote,” alisema Kimbe.

Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Ally Nnunduma alisema wataendeleza alipoishia Kimbe kwa kufanya liwezekanalo City irudi Ligi Kuu. “Tunachoomba ni ushirikiano kwani timu ni yetu sote.”

Chanzo: Mwanaspoti