Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maxime na akili za makocha wazawa

Maxime Benchikhas Maxime na akili za makocha wazawa

Sun, 17 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ulisikia alichosema Kocha Mecky Maxime kabla ya mechi dhidi ya Simba? Yawezekana hujasikia. Ni kichekesho cha kufungia mwaka. Ni kauli ya kufungia mwaka. Ni kituko.

Wakati akihojiwa na moja ya televisheni ya mtandaoni, Maxime aliulizwa tofauti yake na kocha mpya wa Simba, Abdelhak Benchikha.

Akiwa na utulivu wa hali ya juu. Maxime alisema labda wametofautiana majina, Benchikha amemzidi weupe, anavaa kofia na yeye havai. Ila wote ni makocha. Kimbinu ni vilevile tu. Inachekesha sana.

Haijalishi matokeo ya Simba dhidi ya Kagera Sugar yangekuwaje, lakini yawezekana hii ndio kauli mbaya zaidi kuwahi kutolewa na kocha wa mpira kwa mwaka huu. Kauli ya kipuuzi.

Kama kocha ni lazima uweze kutambua uwezo wa mwenzako. Ni lazima uheshimu uwezo wa mwenzako. Hii ndio heshima ya makocha wote duniani. Lakini Maxime hakutaka kufanya hivyo. Akajiweka daraja moja na Benchikha. Inashangaza sana.

Maxime katika maisha yake ya ukocha hajawahi kufundisha timu yoyote kubwa nchini. Amefundisha Mtibwa Sugar na Kagera Sugar. Amekuwa Kocha Msaidizi wa Taifa Stars mara moja. Ndiyo wasifu wake ulipoishia.

Vipi kuhusu Benchikha? Kocha ambaye amewahi kufundisha Raja Casablanca, Al Ahly Tripoli, ES Setif, RS Berkane, MC Alger na USM Alger na nyingine leo anakuwa amemzidi weupe tu Maxime? Ni ajabu na kweli. Ni maajabu ya mwaka 2023.

Yawezekana wote wana vyeti ambavyo vinashabihiana, ila ukweli utabaki kuwa wazi. Benchikha hawezi kufananishwa na kocha yeyote nchini. Sio Maxime tu peke yake, bali wengine wote.

Wakati Maxime akiwa hajawahi kushinda taji lolote kubwa katika ngazi ya klabu, Benchikha ameshinda karibu kila kitu. Ametwaa Ligi Kuu ya Tunisia akiwa na Club Africain. Ametwaa Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na USM Alger. Ametwaa CAF Super Cup mara mbili tofauti. Ni kocha wa viwango.

Wakati Maxime akiwa hana historia yoyote na mashindano ya CAF, mwenzake ana medali tatu. Amekuwa katika mashindano hayo kwa miaka nenda rudi. Ilikuwa kauli ya kumkosea sana heshima Benchikha na mafanikio yake Afrika.

Hata hivyo, sishangia kuhusu hiki alichosema Maxime. Haya ndio mawazo ya makocha wengi wa Tanzania. Wanaamini kuwa wageni wanakuja kufanya kazi nchini ni kama tu wanakuja kuchota pesa na kuondoka. Hawaamini kama wamezidiwa uwezo.

Ndio sababu ni vigumu kwa makocha wa Tanzania kwenda kufanya kazi nje ya nchi.Mawazo yao hayana ushindani. Ni kama vile wameridhika na kile wanachopata hapa. Ndio uhalisia.

Siku moja kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi tulikuwa tukibadilishana mawazo na kocha mmoja mzawa. Kukawa na mjadala kuhusu aliyekuwa Kocha wa Yanga, Nasredine Nabi. Kocha huyu mzawa aliamini Nabi anabebwa na uwezo wa wachezaji wake tu.

Alikwenda mbali na kusema kama angekuwa anaifundisha Yanga angeweza kufanya makubwa kuliko Nabi. Inachekesha kweli. Huyu kocha hakuwa na heshima hata kidogo kwa Nabi. Alimuweka katika daraja lake.

Hebu fikiria huyu ni kocha mzawa ambaye hana mafanikio hata kidogo. Hajawahi kushinda taji lolote nchini. Msimu huu alipewa timu moja ya Ligi Kuu akafukuzwa mapema tu kufuatia matokeo mabaya. Ila alituaminisha kuwa anaweza kufanya vizuri na Yanga kuliko Nabi.

Kocha aliyeifikisha Yanga fainali ya kwanza ya mashindano ya CAF. Kocha aliyeipa Yanga ubingwa bila kupoteza mchezo hata mmoja. Mzawa mmoja tu anaibuka huko na kusema angeweza kufanya zaidi. Ndio mawazo yao na uwezo wao ulipoishia.

Hivyo alichosema Maxime ndio uhalisia wa mawazo mengi ya makocha wa Bongo.  Hawafikirii kuongeza uwezo wao na kushindana zaidi. Ndiyo sababu wanamuona Benchikha amewazidi weupe tu.

Unashindwa hata kuheshimu ukweli kuwa Benchikha alikuwepo kwenye tatu bora ya makocha waliokuwa wakiwania tuzo ya CAF kwa mwaka 2023. Ndiye kocha pekee wa ngazi ya klabu aliyekuwa katika kinyang’a€nyiro hicho. Ni jambo kubwa lakini hawa kina Maxime hawawezi kuliona.

Huwezi kuona makocha wakubwa Ulaya kama kina Pep Guardiola na wengineo wakiwachukulia poa makocha wa timu pinzani.

Hata kama anacheza dhidi ya Arsenal, Guardiola atamheshimu Mikel Arteta. Hata kama anacheza dhidi ya Manchester United, Guardiola atamheshimu Erik Ten Hag. Ndio heshima ya soka.

Kama tunataka kupiga hatua, lazima tuwe na makocha wenye mtazamo tofauti na hawa kina Maxime. Lazima wafikirie mbali zaidi. Lazima wafikirie kufanya kazi nje ya mipaka ya nchi.

Kama wanavyofanya Burundi. Mwaka 2019 walikuwa na makocha 52 wanaofanya kazi nje ya nchi yao. Ndio hawa kina Etienne Ndayiragije, Cedric Kaze na wengineo. Wanajenga msingi wa nchi yao.

Yote kwa yote tusiache kuwaambia ukweli makocha wazawa kuwa wana hatua kubwa wanazotakiwa kuiga mbele ya makocha wa kigeni. Wana safari ndefu ya kuaminika zaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live