Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema licha ya kutopata michezo mingi ya kirafiki ila wapinzani wao, Yanga wasitarajie mchezo mwepesi wakati watakapokutana Uwanja wa Azam Complex Aprili 11.
Timu hiyo haijacheza mchezo wowote tangu mara ya mwisho ilipofungwa mabao 2-0 dhidi ya KMC Machi 9.
Akizungumza Maxime alisema licha ya kukaa kwa muda mrefu bila ya michezo yoyote ya kiushidani, ila haijawaathiri sana na badala yake imetoa nafasi ya kurekebisha mapungufu yao.
“Baada ya mapumziko ya wachezaji, nimegundua stamina na fitinesi yao ilipungua, sasa tulikuwa na programu mbalimbali za Gym na ufukweni ili kuwarudisha katika hali zao za kawaida,” alisema.
Maxime aliongeza anawashukuru viongozi wa Kitayosce kwa kuwakubalia kucheza nao mchezo wa kirafiki ambao anaamini utaleta tija kwao hasa kipindi hiki wanapojiandaa kupambana na Yanga.
“Tunatarajia kucheza leo au kesho Jumanne na baada ya hapo tutaanza safari ya kuja Dar es Salaam na kama tutapata pia timu huko tutacheza mchezo mmoja tu kabla ya kukutana na washindani wetu.”
Mchezo wa mwisho uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, baina ya timu hizo Kagera ilifungwa na Yanga bao 1-0, Novemba 13, mwaka jana lililofungwa na nyota wa kikosi hicho, Clement Mzize.