Siku chache tangu arejee Kagera Sugar, Kocha Mecky Mexime amepewa rungu la kutafuta watu sahihi wa kufanya nao kazi ilimradi timu hiyo irejeshe heshima iliyokuwa nayo misimu kadhaa nyuma.
Katibu Mkuu wa Kagera, Ally Masoud amesema katika kikosi hicho wamemkabidhi Kocha Maxime kutafuta watu wa kufanya nao kazi atakaoona anaendana nao.
Kauli ya Masoud inajiri baada ya hivi karibuni klabu hiyo kuachana na Kocha wa Makipa, John Waow na Kocha wa Utimamu wa Mwili (fitness coach), Buberwa Bilikesi.
Masoud alisema malengo ya kufikia uamuzi huo ni kutotaka tena kuliingilia benchi la ufundi, hivyo wameamua kumpa uhuru wa kuchagua watu wa kufanya nao kazi.
“Tunaamini ili afanikiwe kama ambavyo mwanzo tulieleza baada ya kumuondosha mtangulizi wake ni kutaka kuleta ufanisi katika timu yetu na hilo litafanikiwa tukimwachia uhuru wa kufanya uamuzi.”
Kwa upande wa Maxime alisema ni jambo jema kupewa mamlaka hayo na viongozi wake ingawa bado hajaamua kuchagua watu wa kufanya nao kazi na atakapokamilisha kila kitu kitawekwa wazi.
Maxime aliteuliwa kukiongoza kikosi hicho baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Francis Baraza kusitishiwa mkataba wake Oktoba 28 kutokana na mwenendo wa timu hiyo.
Sio mara ya kwanza kwa Maxime kurejea tena Kagera Sugar kwani alishawahi kuifundisha hapo kuanzia mwaka 2016-2021.