Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maxime: Mtibwa, Kagera Sugar sikieni tu! ni balaa

Mecky Mexime.jpeg Kocha Mecky Maxime

Thu, 1 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mtibwa ni moja ya timu iliyowahi kutingisha nchi kwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara 1999. Ilikuwa chini ya nahodha aliyetikisa muda mrefu kwenye soka la Tanzania, Mecky Maxime ambaye anasema dabi ya Mtibwa na Kagera ni ngumu kuliko mechi yoyote aliyowahi kukutana nayo.

“Hakuna mechi ngumu kama Mtibwa ikikutana na Kagera. Nawaambia hivi kwa sababu nimeishi katika klabu zote hizi mbili. Hii ni mechi ambayo timu huwa zinakamiana sana. Ni bora ucheze na Simba au Yanga kuliko ukutane na Kagera au Kagera akutane na Mtibwa huwa kila timu inataka kumuonyesha mwenzie kuwa wao ni bora,” anasema. “Ushindani huo mpaka sasa bado upo. Nimetoka Kagera juzi tu watu wasidhani eti kwa kuwa umiliki wa hizi timu ni mmoja watasaidiana, hiyo haipo. Huku ndani Kagera anaomba Mtibwa ashuke hayo kama hamuamini chukueni, nimeishi ndani nayajua,”anaeleza na kufafanua jinsi beki wa kulia anapaswa kuwa.

“Beki bora wa kulia au kushoto ni yule anayejua kwanza kuzuia vizuri, lakini baada ya kuwa na ubora huo pia anatakiwa kuwa na ubora wa kujua kupandisha mashambulizi. Siku hizi mpira unachezwa sana na mabeki wa pembeni.

“Mimi ni kocha lakini ukiniambia vitu ambavyo vinanipa nafasi ya kuchagua beki gani wa kuanza nitamchagua ambaye anatimiza vizuri majukumu ambayo nataka ayafanye uwanjani. Siwezi kusema beki gani mzuri kwa sasa ila mabeki wa pembeni wako wengi wazuri.” Anatamani Mtibwa ingerejea kwenye ubora wake kwani enzi hizo ilikuwa ikienda sambamba na Simba na Yanga kwenye kuwania wachezaji wakubwa sokoni.

“Mtibwa ilipochukua ubingwa ilikuwa imeamua kwelikweli na ikawa. Sasa hivi si Yanga na Simba wanapora wachezaji Mtibwa? Wakati huo Mtibwa ilikuwa ndio inapora wachezaji Yanga na Simba.

Nitakutajia kina Monja Liseki, Mwanamtwa Kihwelo, Ally Yusuf Tigana, Yusuf Macho ‘Musso’, Steven Nemesi yaani mastaa wa nchi wengi wamechezea Mtibwa,” anasema. Anasema Mtibwa yao ilikuwa timu bora sana na hakuna timu kubwa iliyokuwa inawapa shida kwani hata wachezaji wenyewe walikuwa wanapambana kibabe. Akiwa anacheza Maxime alikuwa nahodha wa Mtibwa Sugar na pia wa kikosi cha Taifa Stars na hapa anaeleza jinsi alivyokuwa anapasua katikati ya mastaa wa Simba na Yanga na kuvaa kitambaa.

“Unajua kwanza nilitangulia kuwa nahodha wa klabu yangu nikiwa pia nina uhakika wa nafasi ya kucheza mara kwa mara. Kiwango changu ndani ya Mtibwa Sugar ndio kilitengeneza njia ya mimi kuwa nahodha wa Taifa Stars,” anasema Maxime.

“Unajua wakati nikiwa Mtibwa Simba na Yanga zilikuwa na wachezaji bora sana na ushindani ulikuwepo, lakini bahati ilikuwa kwangu kila kocha alipokuwa anakuja ananiona nastahili kuwa nahodha na wenzangu wanakubali, basi maisha yalikuwa yanaenda,” anasema staa huyo ambaye sasa ni Kocha wa Akademi ya Cambiaso huku mchezaji mwenzie wa Mtibwa ile iliyobeba Ubingwa, Zubery Katwila akiinoa Ihefu iliyoko Ligi Kuu Bara.

ASAINI MTIBWA 80,000

Maxime ameichezea klabu moja tu maishani mwake - Mtibwa Sugar iliyomsajili akitokea timu ndogo ya kwao iliyofahamika kama Ruaha Stars. Alisajiliwa kwa Sh 80,000. “Nilitoka pale (Ruaha Stars) nikiwa kijana mdogo. Nilisoma shule za pale Shule ya Msingi Ujirani nikapata elimu ya sekondari shule ya Malecela. Sasa hapa Malecela shule ile ilikuwa ni ya kutwa ninaporudi nyumbani nachezea timu yangu ya Ruaha Stars na Mkamba Rangers.”

“Mtibwa wakawa wanakuja Ruaha kwenye eneo lile ambako kuna chuo cha sukari. Lengo la Mtibwa kuja kule walikuwa wanakuja kuweka kambi za maandalizi, sasa wanapocheza mechi za kirafiki walikuwa wanacheza na sisi Ruaha Stars au Mkamba Rangers. Tulikuwa bado wadogo nikawa nacheza wakaniona, basi nilipomaliza shule wakanichukua Mtibwa.

“Nilipata pesa kidogo wakati huo nakumbuka ilikuwa mwaka 1996 Mtibwa walinipa kiasi cha Sh80,000. Walinipa pesa hizo baada ya kufika Mtibwa nikapokewa na kusaini mkataba.”

“Pia nikakuta vijana wenzangu ambao walikuwa wamepandishwa kama Masumbuko Hassan hiyo ilinipa imani kwamba hapa nitafanikiwa kama nitaweka juhudi,”anasema Maxime.

“Kikubwa ni malengo. Siku nilipoondoka (Ruaha Stars) niliapa kwamba nataka kufanikiwa hapahapa Mtibwa. Nilijua nini nakwenda kufanya, Mungu alinipa uwezo wa kujua kuzima mpira na kutoa pasi. Sikuwa na wasiwasi tena kikubwa nilitanguliza mbele juhudi zangu,” anasema.

“Maisha yangu yote nimeyapata nikiwa Mtibwa na hata baadaye nilipokuja kuwa kocha nilifundisha klabu mbili za Mtibwa na Kagera ambazo zote mmiliki ni mmoja. Kwa hiyo maisha yangu yote yalibebwa na tajiri mmoja tu ambaye ndio mwenye viwanda (vya sukari), Nassoro Seif ambaye alikuwa na wasaidizi wake Mzee Said, Seif na Jamal Bayser ambaye pale Mtibwa alikuwa kama mtendaji mkuu.

“Ukiondoa bosi mwenye zile kampuni Seif, lakini mtu ambaye nitamshukuru sana kwenye maisha yangu ni Bayser huyu alikuwa ni zaidi ya bosi wangu.

Alikuwa kama kaka wa familia yangu katika kunishauri na kila nilipokuwa napata ofa za Simba na Yanga na klabu zingine nilikuwa nakwenda kwake namueleza tunakaa tunajadili kisha ananiambia mdogo wangu, sisi Mtibwa tunacho hiki lakini bora uchukue hiki kidogo kuliko kuchukua kikubwa ambacho kitakupoteza ndani ya muda mfupi na kiukweli nilikuwa namsikiliza kwa kuwa nilikuwa naona ushauri wake una maana kwangu na maisha yangu.”

SIMBA, YANGA

“Ofa (Yanga na Simba) nilipata nyingi sana. Hakuna klabu kubwa ya Tanzania wakati huo ambayo haikuwahi kunipa ofa Simba, Yanga kulikuwa na Kajumulo, Tanzania Prisons baadaye ikaja Moro United ikatikisa nchi hizo zote kwa nyakati tofauti au kwa pamoja zilihangaika sana kupata huduma yangu.

“Hizi Simba na Yanga nilikuwa naongea nao kabisa na kila kitu kinakaribia kukamilika, lakini mwisho wa siku ndio nilikuwa naamua kubaki Mtibwa Sugar.

“Mfano nilikuwa na Victor Costa nakumbuka ilikuwa mwaka 2003 tulicheza pale Morogoro nikamchukua na Juma Kaseja akiwa bado mdogo, tukacheza Mtibwa na Yanga mechi ya FA mpaka mpira unaisha dakika 90 hakuna timu iliyopata bao.

“Tukaenda kwenye penalti, Kaseja akadaka penalti tatu baada ya kumaliza hiyo mechi tunakuja Dar es Salaam tunapanda ndege tunakwenda Mwanza tunakwenda kucheza Cecafa, tulipokuwa timu ya taifa ikaja ofa mimi Victor na Kaseja tunatakiwa na Simba kwa pamoja, lakini wao wakaenda mimi nikaona nibaki Mtibwa.

“Simba na Yanga inataka moyo kuweza kukataa ofa zao. Zilikuwa zinakuja kwa nguvu sana ingawa siwezi kusema ni kiasi gani walikuwa wanataka kunipa. Kama wakikuta umelegea au mwepesi lazima watakutingisha. Kuna watu wakisikia Simba na Yanga hata akili inavurugika, mimi namshukuru Mungu hizo timu hazikunivuruga.”

“Nakumbuka miaka ya 2000-2002, kuna wakati nilikuwa katika vikao na viongozi wa klabu za Simba na Yanga kwa nyakati tofauti na mkimaliza kikao kati yao, mmoja au wawili watakufuata watakwambia usije huku tulia hapo hapo Mtibwa na kikubwa nilikuwa naona wananishauri kitu cha msingi.”

“Mpaka kuwa kocha wa Cambiaso sijawahi kutoa hata shilingi mia kugharamia masomo ya ukocha,” anasema. “Fedha zote zimetoka Mtibwa Sugar, kozi zote mpaka sasa nina leseni A wamenisomesha na kunigharamia hoteli wakati wote nikiwa kwenye masomo.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz