Baada ya kuiongoza Kagera Sugar katika mechi tatu sawa na dakika 270, kocha mkuu wa timu hiyo, Mecky Maxime amekiri ligi kuwa ngumu huku akisifia ubora wa vijana wake akisema upungufu ni mdogo ambao unarekebishika.
Maxime alipumzika kufundisha timu za Ligi Kuu kwa zaidi ya msimu mmoja baada ya uongozi wa klabu hiyo kufikia makubaliano ya kuachana naye na kutimkia kituo cha michezo cha Cambiaso kabla ya kurejeshwa tena hivi karibuni kuchukua nafasi ya Francis Baraza raia wa Kenya.
Katika michezo mitatu aliyoiongoza, Maxime ameshinda mmoja dhidi ya KMC 1-0, sare ya mabao 2-2 na Mbeya City, imepoteza mbele ya Yanga bao 1-0 ambapo inashika nafasi ya 12 ikiwa na pointi 12 baada ya mechi 12. Maxime alisema tangu arejee kwenye majukumu yake ameona upinzani ulivyo mkali kwenye ligi akieleza kuwa kiwango cha nyota wake si haba japokuwa upungufu upo katika baadhi ya maeneo.
Alisema anaendelea kuwajenga kiushindani akibainisha kuwa hakuna timu nyepesi na inahitaji kujipanga ili kupata matokeo mazuri na kujiweka pazuri akiahidi kuwa Kagera Sugar itaamka na kufanya vizuri.
“Matokeo siyo mabaya sana ila inahitaji nguvu ya ziada kutokana na hali ya ushindani ulivyo kwa timu pinzani, nina matumaini kwamba vijana watafanya kweli sisi waliopo kwenye timu hali ni mbaya sana” alisema Maxime.
Nahodha wa timu hiyo, mkongwe David Luhende alisema bado matokeo si mazuri sana hivyo wachezaji wanaendelea kupambana kusaka ushindi katika mechi zinazofuata na kwamba hawajakata tamaa.
“Ni kweli bado hatupo sehemu nzuri lakini kutokana na mwenendo tulio nao inatupa matumaini ya kufanya vizuri hatujakata tamaa.”