Pazia na michuano ya kimataifa kwa msimu wa 2023-2024 lilifunguliwa Jana Agosti 18 kwa mechi za raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Mapema saa 10 jioni ilikuwa KMKM dhidi ya St George ya Ethiopia katika mechi ya Ligi ya Mabingwa na saa 1:30 usiku ilikuwa ni zamu wa wanandugu, Singida Fountain Gate na JKU kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Mechi za michuano hiyo zitaendelea tena Jumapili kwa timu za Tanzania kushuka uwanjani, Yanga itakuwa wageni wa Assas FC ya Djibouti iliyoomba kucheza mechi zao jijini Dar es Salaam katika Ligi ya Mabingwa, ilihali Azam itakuwa ugenini nchini Ethiopia kuvaana na Bahir Dar Kenema.
Yanga inarudi kwenye michuano ya CAF ikitoka kufika fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita ilikotoka sare ya 2-2 na USM Alger ya Algeria. Lakini macho mengi yatakuwa kwa mastaa wapya akiwemo Maxi Nzengeli ambao mashabiki wanataka kuona utofauti.
Yanga inarudi tena kimataifa ikijiuliza kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo msimu uliopita iliishia raundi ya kwanza kwa kufungwa na Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1 na kuangukia mtoano Shirikisho na kuvuka makundi kisha kufika hadi fainali.
Safari ya mafanikio hayo ya Yanga kwa msimu uliopita kwenye Shirikisho yalianzia kwenye Ligi ya Mabingwa ambako kwenye mchezo wa mtoano wa awali walikutana na Zalan FC ya Sudan Kusini ambayo mechi ya kwanza wakisomeka kama wako ugenini, Wananchi walishinda kwa mabao 4-0 kisha kushinda tena kwa mabao 5-0, mechi zote zikichezwa hapa nchini na kufuzu kwa jumla ya mabao 9-0.
Yanga ilikutana na kisiki hatua ya pili ya mtoano walipokutana na Al Hilal ya Sudan wakianzia nyumbani na kulazimishwa sare ya bao 1-1 kisha kwenda kupoteza ugenini kwa bao 1-0 na kujikuta wakitupwa nje ya mashindano hayo na kutua Shirikisho.
Ilipotua Shirikisho Yanga ilishuka na moto mkali ikitinga makundi baada ya kuitupa nje Club Africain na Tunisia kwa ushindi wa jumla wa bao 1-0 wakitangulia kutoa suluhu nyumbani kisha kushinda ugenini kwa bao 1-0.
Kwenye makundi hawakushikika pia. Baada ya kuchapwa mabao 2-0 na US Monastir katika mechi ya ufunguzi, Yanga ilishinda mechi zake nne zilizofuatia na kulazimishwa sare moja ya mwisho na kuongoza kundi lake huku wakifuzu robo fainali ambako nako waliwatupa nje Rivers United ya Nigeria kwa jumla ya mabao 2-0.
Hawakuishia hapo. Wakakutana na Wasauz Marumo Gallants, wakashinda nyumbani kwa mabao 2-0 kisha kushinda tena ugenini kwa mabao 2-1 na kufuzu fainali kwa jumla ya mabao 4-1. Wakatinga fainali dhidi ya USM Alger ambako hapa nyumbani walianza vibaya kwa kupoteza kwa mabao 2-1 kisha kupindua meza kwa kushinda ugenini kwa bao 1-0 na vijana hao wa kocha Nasreddine Nabi kulikosa taji kwa kanuni ya bao la nyumbani na ugenini.
WAANZA NA DJIBOUTI
Msimu huu Yanga ikiwa mpya chini ya kocha mpya, Miguel Gamondi itakutana na Association Sportive d’Ali Sabieh (ASAS) na kama ilivyokuwa dhidi ya Zalan, Yanga imepata habari njema za kwamba mechi hizo mbili zitachezwa hapa nchini baada ya wapinzani wao viwanja vyao kukosa sifa ya kutumika kwa mashindano ya CAF.
IKIPENYA HAPO
Endapo Yanga itafuzu hatua hiyo itakutana na mshindi wa mchezo wa AS Otoho ya Congo Brazzaville itakayokutana na Al Merrikh ya Sudan ambayo ni moja ya timu kongwe Afrika.
Na kama itakomaa raundi hiyo ya kwanza ni wazi Yanga itaenda makundi na kurudia kile ilichokifanya mwaka 1998 ilipofika hatua hiyo ikiwa ni klabu ya kwanza kutoka Tanzania tangu michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilipobadilishwa kutoka ile ya Klabu Bingwa Afrika 1997.
Lakini Yanga inapaswa kukumbuka kuwa msimu huu hakuna kapu la kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika, kama itashindwa kufanya vema katika raundi ya kwanza, basi safari yao itaishia hapo kwani itang’olewa na kuziacha zilizopenya zikienda kuchuana makundi nao watajipanga kwa msimu ujao.
MACHO KWA GAMONDI
Msimu huu Yanga itakuwa na mabadiliko kwenye benchi lake la ufundi ambapo baada ya kukimbiwa na kocha Mtunisia Nasreddine Nabi aliyewapa mafanikio ya msimu uliopita, safari hii watakuwa chini ya Muargentina Miguel Gamondi ambaye ni kama aliunda jeshi lake jipya akiwa na wasaidizi watatu wapya.
Gamondi tayari ameshaanza kuonyesha utofauti wa soka ambalo anataka lipigwe na vijana wake akicheza soka la pasi za haraka za kwenda mbele na kunyang’anya mpira kwa haraka baada ya kuupoteza, jambo ambalo limeanza kuonyesha falsafa hiyo imeingia kwa wachezaji wake.
NYOTA 8 BILA MAYELE
Staa mkubwa ambaye atakosekana kwenye kikosi cha Yanga ni aliyekuwa mshambuliaji wao Mkongomani Fiston Mayele ambaye msimu uliopita alikuwa na balaa kubwa akiibuka kuwa mfungaji bora wa Afrika kwa kufunga mabao 7 na pia kwenye zile mechi za awali za mtoano wa Ligi ya Mabingwa alifunga mabao 7 ndani ya mechi nne tu na sasa ameuzwa Misri pale kwa matajiri wa Pyramids.
Msimu huu Yanga itakuwa na watu wapya wanane wakiwamo mabeki Gift Fred, Kouassi Yao, Nickson Kibabage wako pia viungo Pacome Zouzoua, Jonas Mkude, Mahalatse Makudubela ‘Skudu’, Maxi Nzengeli na mshambuliaji Hafiz Konkoni.
SHIDA IKO HAPA
Ukiangalia Yanga ya msimu huu jinsi ilivyocheza mechi mbili za kuwania Ngao ya Jamii pale Tanga, Gamondi amefanikiwa kuunda kikosi imara ikiwa sawa kuanzia eneo la ulinzi na kiungo lakini changamoto yao iko kwenye umaliziaji.
Gamondi anatakiwa kukuna kichwa haraka kuboresha safu yake hiyo ili iwe na makali ya kumaliza mechi haraka, tatizo ambalo limechangia kutema taji lao la kwanza msimu huu la Ngao ya Jamii mbele ya Simba.