Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maxi aingia anga za Okwi, Kiiza

Maxi Insta Maxi aingia anga za Okwi, Kiiza

Wed, 8 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mabao ya dakika ya 64 na 77 aliyofunga wakati Yanga ikiizamisha Simba kwa mabao 5-1 katika mechi ya Ligi Kuu Bara, yamemfanya mshambuliaji, Maxi Nzengeli kufikia rekodi za nyota wa kigeni waliowahi kuzichezea timu hizo za Kariakoo ya kutupia mara mbili katika mechi moja ya watani.

Maxi aliyesajiliwa msimu huu kutoka AS Maniema Union ya DR Congo alifunga mabao hayo juzi wakati Yanga ikipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kumfanya afikishe jumla ya mabao saba msimu huu akilingana na Stephane Aziz KI.

Mabao hayo yamemfanya Maxi alingane na nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza ‘Diego’ waliokuwa wakishikilia rekodi ya nyota wa kigeni kufunga mabao mawili kwenye mechi moja ya watani.

Okwi ndiye aliyeanza kuandika rekodi hiyo kwenye mechi iliyopigwa Mei 6, 2012 ambapo Simba ilishinda mabao 5-0 kabla ya Kiiza aliyepo kwa sasa Kagera Sugar kuijibu Oktoba 20, 2013 katika pambano lililoisha kwa sare ya mabao 3-3.

Katika mechi ya Mei 2012, Okwi alifunga mabao yake katika dakika ya kwanza na 65, wakati yale ya Kiiza, yalifungwa kwenye dakika ya 35 na 45 ambapo Yanga ilienda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-0 kabla ya Simba kuyachomoa kipindi cha pili na mchezo kuisha kwa sare hiyo ya 3-3.

Kama ilivyokuwa kwenye mechi ya mwaka 2012, ambao Okwi alikuwa na nafasi ya kuvunja rekodi ya King Abadllah Kibadeni ya kufunga hat trick mwaka 1977, kwa Simba kupata penalti tatu, lakini hakupewa hata moja kuipiga na badala yake Patrick Mafisango, kipa Juma Kaseja na Felix Sunzu ndio walioipiga, ndivyo ilivyotokea kwa Maxi juzi Kwa Mkapa.

Katika mchezo huo Maxi akiwa tayari ana mabao mawili, Yanga ilipata penalti dakika ya 87, lakini kiungo huyo hakupewa nafasi ya kupiga na badala yake, Pacome Zouzoua ndiye aliyepiga mkwaju huyo na kuiandikia Yanga bao la tano, hivyo kuifanya rekodi ya Kibadeni iendelee kudumu kwa zidi ya miaka 46 kwani Kibadeni alifunga kwenye mechi iliyopigwa Julai 19, 1977 Simba ikishinda 6-0.

Mbali na kufikia rekodi za Okwi na Kiiza ambao wote ni raia wa Uganda, Maxi pia ameingia katika anga za Wakongomani wenzake waliowahi kufunga mabao kwenye Kariakoo Derby za Ligi Kuu akifuata nyayo Pitchou Kongo aliyefunga wakati Yanga ikilala 2-1 katika mechi iliyopigwa Agosti 7, 2004, Mafisango aliyefunga katika ushindi wa 5-0 wa Simba mwaka 2012, japo alibadili uraia na kuwa Mnyarwanda hadi alipokumbwa na mauti Mei 17, 2012.

Deo Kanda alikuwa mchezaji wa tatu Mkongo kufunga kwenye Kariakoo Derby ya Ligi Kuu katika mechi ya Jan 04, 2020 iliyoisha kwa sare ya 2-2 akiifungia Simba bao la pili baada ya awali Meddie Kagere kuitanguliza Simba kwa penalti na Yanga kuchomoa klupitia kwa Mapinduzi Balama na Mohammed Issa ‘Mo Banka’.

Beki Henock Inonga ndiye aliyekuwa mchezaji wa mwisho Mkongo kufunga kwenye derby ya TPL wakati Simba ikiicharaza Yanga 2-0 mechi ya msimu uliopita kabla ya Maxi na Pacome kutupia juzi na kuiweka Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikifikisha pointi 21 baada ya mechi tisa.

Hata hivyo, nyota wa zamani wa Yanga na mwanamuziki maarufu wa Kikongo, Fredy Mayaula Mayoni ndiye aliyekuwa mchezaji wa kwanza kutoka DR Congo kufunga mabao mawili kwenye Kariakoo Derby katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Karume ambapo Yanga ilishinda mabao 2-1, mchezo uliopigwa Juni 30, 1970, huku Fiston Mayele alifunga kwenye mechi ya Ngao ya Jamii ya msimu uliopita ambapo Simba ilicharazwa mabao 2-1. Mayele pia alifunga kwenye mechi ya Ngao ya Jamii ya msimu wa 2021-2022 Yanga iliposhinda 1-0.

Chanzo: Mwanaspoti