Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maxi, Pacome wapewa Simba

Pacome X Nzengeli .png Maxi, Pacome wapewa Simba

Sun, 29 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga haipoi. Baada ya juzi Ijumaa kuichapa Singida Big Stars mabao 2-0 na kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, jana imekimbia haraka na kujificha kambini kujiandaa na mechi inayofuata dhidi ya watani zao, Simba huku viungo watatu Stephane Aziz Ki, Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua wakivishwa mabomu.

Yanga itakutana na Simba Novemba 5, mwaka huu na inataka kutetea taji kwa mara ya tatu mfululizo, lakini ukiachana na hilo inataka kuibuka na ushindi dhidi ya mpinzani wake wa karibu huyo ili kumpoteza mwelekeo katika kushindania ubingwa.

Ili kuhakikisha hilo linatimia, benchi la ufundi la Yanga limegoma kuwapa mapumziko Aziz Ki, Pacome na Maxi na mastaa wengine likiamini ndiyo mitambo ya mabao ambayo itatumika kuimaliza Simba hivyo wameendelea kuwafua kimyakimya kwenye kambi iliyopo Avic Town Kigamboni.

Mara nyingi baada ya mchezo mmoja kumalizika, Yanga imekuwa na utaratibu wa kuwapa wachezaji wake mapumziko ya siku moja, lakini kwa jana jambo hilo halikutokea.

Jeuri hiyo inakuja kutokana na namba za watatu hao kwenye ligi kwa msimu huu kwani hakuna kombinesheni iliyowafikia katika timu 16 zote za ligi hadi sasa na wanaonekana kuwa wanaweza kuendelea kuwika zaidi.

Viungo hao washambuliaji kwa pamoja hadi sasa wamefunga jumla ya mabao 14 kwenye ligi, Aziz Ki akiongoza kwa kuwa nayo sita akifuatiwa na Nzengeli mwenye matano huku Pacome akiwa na matatu.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alisema anajivunia timu yake kwa kazi kubwa inayofanya na sasa anarudi mazoezini kuboresha baadhi ya vitu kabla ya kuvaana na Simba Novemba 5.

Moja ya vitu ambavyo Gamondi aliweka wazi kuvifanyia kazi ni kutumia vyema nafasi wanazozipata huku akiwataja Aziz Ki, Pacome na Nzengeli.

“Tumeshinda mechi (dhidi ya Singida) lakini tumepoteza nafasi nyingi. Hili ni tatizo na haraka tunakwenda kulifanyia kazi.

‘’Eneo langu la mbele kina Aziz Ki, Pacome, Nzengeli na wengine mara nyingi walitengeneza nafasi lakini baadhi hazikutumika vizuri ila nawapongeza kwa kazi kubwa waliyoifanya,” alisema Gamondi na kuongeza;

“Hatuna muda wa kupumzika, tuna kazi kubwa ya kufanya kabla ya mechi ijayo. Hadi sasa hatutarajii kuwa na mabadiliko makubwa lakini hilo tutalijua kwenye uwanja wa mazoezi.”

Straika wa zamani wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’ alisema kwa sasa Yanga ina kikosi imara lakini uwepo wa Pacome, Aziz Ki na Nzengeli ni silaha kubwa kikosini hapo.

“Timu iko vizuri na kila mchezaji anafanya vyema. Kuna ule mstari wa mbele kina Aziz Ki, Pacome na Nzengeli, kwa sasa ndio wanaibeba timu zaidi. Wamekuwa na muunganiko bora na wanacheza kwa maelewano makubwa, nadhani ni ngumu kwa timu pinzani kuwazuia wasitengeneze nafasi,” alisema SMG.

Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa na Simba kwa matutu katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), mechi ambayo dakika zake 90 zilimalizika kwa suluhu, lakini ikiwa pia ilipoteza mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara waliokutana msimu uliopita kwa kulala mabao 2-0, huku mchezo wa kwanza wakitoka 1-1.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: