Camas Kamji kadogo katika eneo la Jiji la Seville, Hispania. Hadi sasa katika mji huo kuna wakazi 27,463. Kuna watu wawili maarufu zaidi Hispania wamezaliwa katika mji huu.
Wa kwanza? Rafael Nunez Florencio. Mwanahistoria, mwanafalsafa na mwanaharati maarufu Hispania. Wa pili? Jina lake unaweza kulikumbuka kwa urahisi. Sergio Ramos. Kule kwa Walatini huenda kuna Sergio Ramos wengi lakini Sergio Ramos maarufu ni mmoja tu. Huyu hapa anayepiga soka.
Nimekumbuka tu namna ambavyo mawimbi ya soka yalimpiga Ramos na kumpeleka juu zaidi ya alivyofikiri. Majuzi nilikuwa namtazama katika pambano moja la Sevilla. Kama kawaida yake alilamba kadi yake ya njano, pia akafunga bao. Kuna vitu vitatu ambavyo ni kawaida kwa Ramos. Kadi ya njano, kadi nyekundu na bao. Anaweza kuvipata muda wowote ule.
Ramos ni mtoto wa Camas Sevilla. Ni mtoto wa Sevilla hasa. Alianzia soka la utotoni Sevilla, kisha akajiunga na timu ya vijana, halafu timu ya wakubwa. Nakumbuka kumuona wakati huo akicheza Sevilla kama mlinzi wa kulia lakini wakati mwingine kama mlinzi wa kati.
Hata hivyo, mwaka 2005 Real Madrid walimpitia kama upepo. Amecheza Real Madrid kwa miaka 16 akishinda karibu kila kitu ambacho mwanasoka anatamani kushinda. Ameshinda hadi Kombe la Dunia achilia mbali hili la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Baadaye alifuata noti za Waarabu pale Paris lakini sasa amerudi Sevilla. Hili ndio jambo ambalo limenisisimua zaidi. Amerudi amepewa kitambaa chake cha unahodha. Ni kama vile mtoto aliyerudi nyumbani baada ya kuhangaika ughaibuni.
Sio wachezaji wengi wanaofanya hivi lakini wanaofanya hivi huwa wanasisimua. Kwa kawaida wachezaji wengi wa timu kubwa walijikuta wakicheza katika timu bila ya kupenda. Ni uwezo mkubwa ndio ambao uliwapeleka huko lakini sio mapenzi yao. Ni pesa pia ndio ambazo zinawapeleka huko lakini sio mapenzi yao.
Wachezaji wengi huota ndoto ya kuchezea klabu ambayo baba yake anamshika mkono na kumpeleka uwanjani. Sio lazima iwe klabu kubwa. Huwa ni klabu ya nyumbani tu. inawezeka kuwa Genk, Kibaha Stars, Tranmere, Wolves na nyinginezo.
Paul Scholes aliwahi kukaririwa akisema akiwa mtoto mdogo timu ambayo alikuwa akiota kuchezea ni Oldham Athletic ambayo ipo daraja la tano pale England. Sababu? Alikuwa shabiki wa timu hiyo wakati huo akibebwa na baba yake kwenda uwanjani.
Ndoto zilikuwa kwa Oldham lakini uwezo ukampeleka Manchester United. Hadi wakati huo akiwa staa wa Man United, Scholes alikuwa akihudhuria mechi za Oldham katika uwanja wao mdogo wa Boundary Park unaochukua mashabiki 13,513. Ndoto za Ramos zilikuwa Sevilla lakini ukweli, kipaji chake kikawa kikubwa kuweza kucheza Seville kwa muda wote.
Akajikuta ameangukia Real Madrid. Hata kama sio Madrid angeweza kujikuta ameangukia Liverpool, AC Milan, Man United au Bayern Munich. Zote hizi ni kubwa kuliko Seville.
Sasa anarudisha fadhila nyumbani. Anacheza katika jitihada zile zile ambazo alikuwa anaonyesha Real Madrid. Nilichompenda Ramos ni baada ya kutoka PSG angeweza kwenda zake Saudi Arabia au Marekani. Hata hivyo aliamua kurudi nyumbani kumalizia hadithi ya maisha yake.
Aliamua kurudi nyumbani kucheza katika timu ambayo anacheza kama shabiki. Timu ya nyumbani. Thierry Henry aliwahi kurudi kucheza Arsenal lakini kumbuka hapo alikuwa analipa fadhila kwa timu ambayo imempatia umaarufu lakini sio timu ya nyumbani.
Cristiano Ronaldo ni hivyo hivyo. Aliporudi Manchester United akitokea mzunguko wake wa Real Madrid na Juventus ilikuwa inamaanisha alikuwa anarudi katika timu iliyompatia umaarufu. Ukweli, timu ya nyumbani kwake ipo Ureno.
Wakati mwingine mashabiki huwa wanagawanyika linapokuja suala kama la Ramos. Ndani ya klabu kama Sevilla kuna ambao watamwona Ramos kama msaliti lakini ndani ya klabu pia kuna ambao wataendelea kumwona kama mwenzao.
Kuna mashabiki ambao hawakubali udogo wa klabu yao dhidi ya klabu nyingine. Wanaamini mchezaji aliyekulia kwao akiwa bora anastahili kubakia hapo hapo na kuifanyia makubwa klabu yao. Lakini kuna wengine ambao wanakiri klabu yao haina ubavu wa kupambana na Real Madrid, Barcelona na wengineo.
Hili kundi la pili ndilo ambalo linamuaga mchezaji kwa heshima, pia linampokea kwa heshima. Nilipotazama suala la Ramos kurudi Sevilla nimeona kundi la pili limekuwa na nguvu zaidi kiasi kwamba Ramos amepewa unahodha.
Pale pale Hispania Luis Figo aliwahi kufanya uhamisho wa kushangaza kutoka Barcelona kwenda Real Madrid. Sawa, timu zote sio timu zake za nyumbani. Mashabiki wa Barcelona walikuwa na haki kubwa ya kumchukia Figo katika uhamisho kama huu kwa sababu Barcelona wana kila sababu ya kuvimbiana na Madrid katika suala la mataji na ukubwa.
Sasa baada ya Ramos kurudi nyumbani nasubiri kuona mastaa wawili kama wataweza kumalizia soka nyumbani walau kwa msimu mmoja tu. Nasubiri kuona kama Lionel Messi ataweza kumalizia soka katika klabu ya Newell’s Boys ya Argentina.
Ni klabu ambayo aliichezea utotoni lakini kama hata hajaenda katika klabu ya vijana na klabu ya wakubwa akajikuta akitimkia Barcelona kwa matibabu na kisha kuibuka kuwa staa mkubwa duniani. Mara zote imekuwa ikizungumzwa huenda siku moja Messi atarudi katika klabu hiyo na kucheza walau msimu mmoja wa mwisho wa maisha yake ya soka.
Mwingine ni Ronaldo. Ataweza kuimalizia historia ya maisha yake? ataweza kurudi tena Sporting Lisbon na walau kucheza pambano lake la mwisho la soka akiwa na klabu hii kama ambavyo Ramos anafanya? Tusubiri na kuona.