Kikao cha mawaziri na wataalamu wa michezo kutoka Uganda, Kenya na wenyeji Tanzania jijini Arusha kimejadili mpango wa nchi hizo kuwa mwenyeji wa Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2027.
Kikao hicho kilichoongozwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Pindi Chana kiliridhia kuundwa kwa Kamati ya Maandalizi ya kuratibu mpango huo.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na viongozi wa mashirikisho ya michezo kutoka nchi hizo ili kufanikisha azma hiyo.
“Wajumbe ni viongozi wa Mashirikisho ya Mpira wa Miguu wa nchi za Kenya, Uganda na wenyeji Tanzania, Baraza la Michezo (BMT) na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo,” amesema Dk Chana.
Tanzania imepitishwa na Wajumbe wa Baraza la Michezo la Umoja wa Afrika Kanda ya IV kuwa Makao Makuu ya Sekretarieti ya baraza hilo linaloundwa na nchi 14.
Nchi hizo ni Comoro, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Madagascar, Mauritius, Rwanda, Shelisheli, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Uganda na wenyeji Tanzania.
Tanzania ilitumia fursa ya Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka barani Afrika uliofanyika jijini Arusha Agosti mwaka jana, kuwasilisha ombi la kuwa mwenyeji wa Fainali za Mataifa ya Afrika ‘Afcon’ 2027.
Tanzania haijawahi kuwa mwenyeji wa fainali hizo tangu zilipoanzishwa mwaka 1957, licha ya kuwahi kupata nafasi ya kuwa mwenyeji wa fainali za vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019 zilizofanyika jijini Dar es salaam.
Iwapo mataifa hayo matatu yatafanikiwa itakuwa ni mara ya kwanza kwa michuano hiyo mikubwa ya Soka Barani Afrika kufanyika Afrika Mashariki.