Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mavitu ya Emery Aston Villa vigogo wanateseka

Aston Villa Hesabu Mavitu ya Emery Aston Villa vigogo wanateseka

Thu, 14 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tangu achukue mikoba ya Aston Villa, Novemba mwaka jana, Kocha Unai Emery amefanya kazi kubwa huko Villa Park akikusanya pointi 84 katika mechi 41 alizosimamia timu hiyo kwenye Ligi Kuu England.

Kuonyesha namba hizo kwenye ukubwa na thamani yake, hiyo ina maana Aston Villa ya Emery ina wastani wa kuvuna pointi 2.04 kwa kila mechi, huku akiweka wastani wa ushindi wa asilimia 63.4.

Aston Villa sasa imejikuta kwenye kundi la timu zinazoshindania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu sambamba na Liverpool, Manchester City na Arsenal.

Kitu anachofanya Emery huko Villa Park si cha kubeza, huku ubora wa kikosi chake unazidi vigogo wa maana kabisa wa Ulaya, kwa pointi zao walizovuna kwenye ligi zao ndani ya muda ambao kocha huyo Mhispaniola amekuwa akifanya kazi Villa Park.

Emery alibamba dili la kuinoa Aston Villa, Novemba mwaka jana na kwa hesabu za kuanzia muda huo, amevuna pointi nyingi kuzidi klabu kubwa kibao zilizopo ndani ya Ligi Kuu tano bora za Ulaya. Cheki hapo timu ambazo zimeburuzwa na Aston Villa kwa pointi walizovuna kwa muda ambao wamekuwa chini ya Kocha Emery huko Villa Park.

Napoli - Pointi 82

Kinachovutia ni kuona Aston Villa ya Emery imevuna pointi mbili zaidi ya zile ilizovuna mabingwa wa Italia, Napoli kwa kipindi cha kuanzia Novemba mwaka jana.

Si jambo lenye kificho kwa namna Napoli imekuwa kwenye ubora mkubwa kwa kucheza soka lenye mvuto na kubeba taji la ligi la kwanza tangu msimu 1989-90.

Lakini, baada ya kuondoka kocha Luciano Spalletti timu hiyo imeshuka kiwango kidogo na hivyo inashika namba sita kwenye ligi na tangu Novemba imevuna pointi 82.

Bayern Munich - Pointi 78

Mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich wanafurahia mwanzo mzuri wa msimu huu kwenye Bundesliga.

Hata hivyo, kwa makali yao yote, basi wamezidiwa pointi sita na Aston Villa kwa kipindi cha kuanzia tangu kocha Emery alipokabidhiwa mikoba huko Villa Park. Straika Harry Kane amekuwa moto kwelikweli kwenye fowadi hiyo ya kikosi cha Thomas Tuchel, lakini bado Bayern Munich imezidiwa pointi na Aston Villa kwa hesabu za kuanzia Novemba mwaka jana. Hakuna ubishi, Emery amefanya maajabu yake.

Bayer Leverkusen - Pointi 77

Bayer Leverkusen imekuwa kwenye kiwango bora sana tangu ilipoanza kuwa chini ya Xabi Alonso kama tu ambavyo Aston Villa imekuwa ya moto baada ya kuwa chini ya kocha Emery. Alonso alichukua mikoba ya kuinoa Leverkusen, Oktoba mwaka jana, kipindi hicho timu hiyo ilikuwa ikishika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Bundesliga.

Tangu wakati huo, kikosi kimepanda na sasa kinaongoza ligi, huku kwa jumla kwa kuanzia Novemba mwaka jana, imevuna pointi 77, saba nyuma ya Aston Villa ya Emery.

Borussia Dortmund - Pointi 74

Kikosi cha Edin Terzic kilikaribia kabisa kunyakua ubingwa wa Bundesliga msimu uliopita. Dortmund ilijiharibia yenyewe kwenye mechi ya mwisho wa msimu baada ya kutoka sare na Mainz 05 na hivyo kutoa fursa kwa Bayern Munich kunyakua ubingwa huo.

Lakini, kwa hesabu za kuanzia wakati ambao Emery alikabidhiwa mikoba ya kuonoa Aston Villa, miamba hiyo ya Ujerumani, Dortmund imevuna pointi 74, pointi 10 ya zile ambazo imebeba miamba ya Villa Park chini ya Mhispaniola, Emery.

AC Milan - Pointi 73

Serie A ilikuwa na ushindani mkali sana msimu uliopita na ndiyo maana haishangazi kuona Italia kuwa na timu nyingi zilizotinga kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ikimaliza kwenye nafasi ya nne msimu uliopita na kushika namba tatu msimu huu, Milan imevuna pointi 73 kwa kipindi cha kuanzia Novemba mwaka jana hadi sasa, hiyo ikiwa pungufu ya pointi 11 ya ilizovuna Aston Villa ndani ya muda huo ambao imekuwa chini ya kocha huyo wa zamani wa Arsenal na PSG, Emery.

Marseille - Pointi 72

Miamba ya soka ya Ufaransa ilishika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligue 1 msimu uliopita na imekusanya pointi 72 kwa kipindi cha kuanzia tangu Emery alipokabidhiwa mikoba ya kuinoa Aston Villa.

Hiyo ina maana Aston Villa imevuna pointi 12 zaidi ya ambazo imevuna Marseille kwa kipindi ambacho imekuwa chini ya kocha Emery. Huko Ufaransa, mabingwa PSG wenyewe walivuna pointi 86 ndani ya muda huo na hivyo kuizidi Aston Villa ya Mhispaniola Emery kwa pointi mbili tu.

Ajax - Pointi 65

Ajax imekuwa ya kawaida sana msimu huu, ikishindwa kabisa kukaribia makali yao ya msimu uliopita, licha ya kwamba kwa sasa imeanza kupata moto baada ya kushinda mechi sita kati ya saba za mwisho. Miamba hiyo ya Uholanzi ilimaliza nafasi ya tatu msimu uliopita na msimu huu hadi sasa imeshaachwa pointi 21 na vinara PSV. Kwa kifupi tu, Aston Villa ya kocha Emery imekusanya pointi 19 zaidi ya ilizovuna Ajax kwa kipindi ambacho Mhispaniola huyo amechukua kazi Villa Park.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live