Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mauya? Msimchukulie poa!

Mauya Pic Kiungo wa Yanga Zawadi Mauya

Fri, 31 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kama unadhani kiungo wa Yanga, Zawadi Mauya amebahatisha kuupiga mwingi dhidi ya Prisons na Biashara United, utakuwa umechemka kwani fundi huyo ana mikakati maalumu ya kufanya kazi ya kuacha alama msimu huu.

Alifichua kwamba kila dakika anayopewa kucheza na kocha Nesreddine Nabi kwake anaitazama kwa jicho makini ili kuhakikisha anaitendea haki, huku akizingatia ushindani wa namba uliopo ndani ya kikosi.

Alisema anautazama msimu huu kibingwa kwenye klabu yake na hilo linamfanya kila wakati kuongeza bidii kuhakikisha anakuwa miongoni mwa wachezaji wenye mchango mkubwa.

“Kikubwa naomba uzima, ila ninachozingatia katika majukumu yangu ni kutumia nafasi nayopewa na kocha ili kuipa manufaa timu. Nimejipanga kuipigania timu yangu,” alisema.

“Najua msimu huu ni mgumu, ila kadri tunavyoshinda mechi na kuendelea kukaa kileleni, binafsi inanipa moyo kuendelea kuutamani ushindi kila tunapokuwa uwanjani. Hilo linanifanya nijitume kwa kadri niwezavyo.”

Ufundi wa Mauya uliwahi kuonekana machoni mwa aliyekuwa kiungo mpaka rangi wa timu hiyo, Haruna Niyonzima aliyesema anamuona mbali na ipo siku kila jicho la soka litaona maajabu yake.

“Mauya ni fundi sana. Naamini atakuja kufanya makubwa zaidi akiendelea kupata nafasi ya kucheza. Anaujua mpira kwani nilikuwa naona anachofanya wakati nipo Yanga,” alisema.

“Jezi niliyokuwa naitumia nilitamani angeivaa Mauya kutokana na kile ambacho nakiona mguuni kwake. Ajitume asikate tamaa, atakuja kuwa gumzo kila sehemu.”

Kiungo wa zamani wa Simba, Shaban Kisiga alisema Mauya ni mchezaji mzuri huku akitarajia kuuona mwendelezo wa kiwango chake endapo kocha atampa nafasi kucheza mara kwa mara.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz