Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mauya: Moto tulioanza nao msimu huu hauzimiki

Zawadi Mauya Jamhuri Zawadi Mauya

Sat, 29 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi ndani ya kikosi cha Yanga, Zawadi Mauya (35) amesema kuwa morali ya kupambana kimataifa waliyoanza nayo mwanzo mwa msimu huu haitashuka mpaka wahakikishe wanafikia malengo waliojiwekea.

Mauya amesema hayo leo Jumamosi, Aprili 29, 2023 wakati akizungumza na vyombo vya habari kuelekea mchezo wao wa marudiano wa robo fainali ya kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria.

“Sidhani kama kuna ugumu wowote kushinda hii mechi kwa sababu historia ipo lakini sisi kama wachezaji tuna ari kubwa ya kushinda hii mechi na kwenda hatua inayofuata.

“Ni muda mrefu timu yetu haikuwa kwenye kiwango kizuri katika mashindano ya kimataifa, lakini morali tuliyokuwa nayo kwenye michuano ya CAF tangu msimu huu umeanza ilikuwa ni kubwa sana ili kuhakikisha tunavunja huu mwiko.

“Kwa hatua tuliyofikia ni rahisi kuliko tulikotoka kwenye hatua za awali, palikuwa pagumu sana kupambana na kuhakikisha tunafikia kile tulichokuwa tumejiwekea.

“Mpaka hapa tumefika klabu imepiga hatua kubwa sana zaidi ya huko nyuma, lakini hii haituondolei ile hamu ya kupambana ili tuweze kuweka rekodi kubwa zaidi ya hapa tulipofikia.

“Sio mchezo mgumu katika historia ya Yanga lakini ni mchezo mgumu katika kuvuka hatua inayofuata. Tuna nafasi ya kuweza kufanya vizuri. Sisi tunafuata maelekezo ya mwalimu na benchi zima la ufundi. Mashabiki waendelee kutusapoti,” amesema Zawadi Mauya.

Yanga wakiwa na mtaji wa bao 2-0, kesho watashuka katika dimba la Mkapa kukipiga na Rivers United wakisaka tiketi ya kusonga katika hatua ya nusu fainali ya kombe la shirikisho barani Afrika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live