Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maumivu yalivyomtafuna Dele Alli

DeleFEAT 768x448 Maumivu yalivyomtafuna Dele Alli

Mon, 17 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Maisha yanatufundisha mengi. Usimnyooshee mtu kidole na wala usimcheke yeyote kisa ameshindwa jambo.

Maisha ya watu yamebeba siri kubwa. Mengine yamebeba madhila makubwa yenye kuumiza.

Mchezaji Dele Alli amefichua jinsi alivyonyanyaswa kingono na rafiki wa mama yake wakati alipokuwa mdogo.

Staa huyo wa kimataifa wa England alifichua jambo hilo lililoshtua wengi katika kipindi maalumu cha mahojiano kwenye televisheni wakati aliporejea Everton, Aprili mwaka huu.

Katika kipindi hicho cha The Overlap kinachoongozwa na Gary Neville, beki wa zamani wa Manchester United na England, ambaye aliwahi kuwa kocha wa Three Lions na Valencia, Dele alifichua kipindi cha karibuni alilazimika kwenda kwenye kituo maalumu za tiba baada ya kuathiriwa na dawa za usingizi.

Dele amekiri yeye ni mwathirika wa pombe na dawa za usingizi kiasi kilichomfanya aende kwenye kituo maalumu cha tiba maarufu kama vituo vya soba. Alifunguka kuhusu manyanyaso makubwa aliyokutana nayo alipokuwa mdogo.

Dele alisema: “Nilipokuwa na umri wa miaka sita nilikuwa natumikishwa kingono na rafiki wa mama yangu...kwa sababu mama yangu alikuwa mlevi sana. Hilo lilitokea nilipokuwa na miaka sita.”

Dele wakati anahadithia hilo alikuwa kwenye hisia kali sana, machozi yalimmiminika wakati alipofunguka kuhusu machungu hayo ya moyoni na hisia.

Dele aliendelea: “Kisha nikapelekwa Afrika kujifunza nidhamu, halafu nikarudi. Nilipokuwa na miaka saba, nilianza kuvuta sigara, kisha nilipofika miaka minane nilianza kuuza dawa za kulevya.

“Kuna mtu mmoja hivi mkubwa aliniambia watoto wakiwa na baiskeli zao mtaani hawasimamishwi, hivyo nilikuwa nikiendesha nikiwa na mpira wangu wa soka ambao ndani ulikuwa umejazwa dawa za kulevya.

“Nikiwa na miaka 11 nilining'inizwa darajani…na mtu mmoja hivi wa kutoka mji wa jirani. Mwanamume.

“Nilipofika miaka 12 nilichukuliwa na familia nyingine na tangu hapo, hakika nilikuwa kwenye familia bora kabisa.

“Sikuhitaji watu bora zaidi ya wale walionichukua kwa namna ambavyo walikuwa wakinifanyia. Kama Mungu aliumba watu basi ni wao – walikuwa watu wema na walinisaidia sana.

“Nilipokuwa naishi nao ilikuwa ngumu kwangu kufunguka kwao kwa sababu nilihisi kama wanaweza kunifukuza.”

Wakati anakipiga Tottenham Hotspur, kiungo huyo alibadili jina lake lililokuwa likionekana kwenye jezi yake kutoka 'Alli' na kuwa 'Dele', kwa kuwa alijiona hana muunganiko na jina la ubini wake la Alli.

Hivyo tangu wakati huo, jezi ya staa huyo mgongoni ilikuwa ikiandikwa jina la 'DELE'.

Alisema: "Nilihitaji jina litakalotokea kwenye jezi yangu basi liwe linaniwakilisha na kunitambulisha na niliona sina muunganiko na ubini wa Alli. Huo haukuwa uamuzi ambao sikuupa muda wa kujadili, nilifanya hivyo na familia iliyokaribu na mimi."

Kipindi hicho kilifuatia na nyakati mbaya za Dele kwenye kikosi cha Spurs na mara kadhaa alijikuta akiwekwa benchi na hata Jose Mourinho alipowasili kwenye timu hiyo alibainisha atampa nafasi kiungo huyo kama tu ataonyesha mabadiliko makubwa ya kiuchezaji ndani ya uwanja.

Kumbe wakati hayo yote yanamkuta Dele, moyo wake ulikuwa umebeba mazito mengi yaliyokuwa yanamfanya akose usingizi na kujikuta akiibukia kwenye wimbi la matumizi yaliyopitiliza ya dawa za usingizi.

Dele, 27, aliporudi England akitokea Uturuki alikokuwa akicheza kwa mkopo, aliamua kutafuta tiba ya matumizi yaliyokithiri ya pombe na dawa za usingizi na alijipeleka mwenyewe kwenye kituo cha waathirika.

"Niliporejea kutoka Uturuki nilijigundua nahitaji oparesheni maalumu kwa sababu nilikuwa kwenye hali mbaya kiakili, hivyo nilikwenda kwenye vituo vya kisasa kabisa kurekebisha afya yangu ya akili.

"Kituoni hapo wanajishughulisha na waathirika wa ulevi na mambo yenye kuumiza hisia. Niliona ni wakati mwafaka kwangu. Huwezi kuambiwa uende hapo kama mwenyewe haupo tayari, ni kitu unachopaswa kuamua mwenyewe, la mambo hayawezi kuwa sawa. Nilijikuta kwenye kundi mbaya sana kitu ambacho kingekwenda kuniumiza."

Dele alikiri kuna nyakati alifikiria kustaafu soka miaka mitatu iliyopita wakati alipokuwa na umri wa miaka 24. Na mkali huyo alisema: "Asubuhi moja niliamka, nilikuwa na safari ya mazoezini. Nakumbuka nilisimama mbele ya kioo na kujihoji vipi kama nitastaafu sasa hivi. Miaka 24. Kuacha kufanya kitu ninachokipenda. Kwa upande wangu huo ni wakati ambao nilivunjika sana moyo." Aliongeza: "Nilikuwa kwenye vita ya mimi na mimi katika kila kitu.

Nilikuwa naonyesha nina furaha, lakini kwa ndani, nilikuwa nateketea." Mpenzi wake wa sasa Dele, mrembo Cindy Kimberly alituma ujumbe wa kumsapoti mpenzi wake baada ya kufunguka kila kitu kilichokuwa kikimuumiza, baada ya ujumbe wa mrembo huyo kwenye Twitter kusomeka hivi: "Najivunia wewe." Na Prince William alimpongeza Dele kwa kuonyesha ujasiri na hamasa kwa wengine.

Prince William alisema: "Kujadili afya ya akili si udhaifu. Acha tuendelee kutoa nafasi kwa mijadala kama hii. Tupo pamoja nawe na tunakutakia kila la heri." Kiungo James Maddison, ambaye alijiunga na Spurs hivi karibuni, alituma ujumbe wa kumsapoti Dele, alipoposti kwenye Instagram, alipoandika "Nakupenda kaka" na kuambatanisha emoji ya emoji.

Ryan Sessegnon, ambaye alicheza pamoja na Dele walipokuwa Spurs, aliandika: "Nakupenda kaka. Jivunie."

Nahodha wa England, Harry Kane alipendezwa na posti hiyo sambamba na Declan Rice na Kieran Trippier. Wakati Kyle Walker-Peters aliandika: "Najivunia wewe kaka, nakupenda."

Mtangazaji wa kipindi cha Overlap, Neville, ambaye alimnoa Dele walipokuwa pamoja kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England alikaribia kumwaga machozi wakati staa huyo alipokuwa akihadithia magumu aliyopitia maishani.

Neville alisema: "Mazungumzo yaliyokuwa na hisia kali niliyowahi kufanya katika maisha yangu."

Dele alikuwa mmoja wa wachezaji wa Everton waliwahi kabisa kurudi kujiunga na timu kwa ajili ya pre-season wiki iliyopita.

Lakini, kocha Sean Dyche ameshindwa kumhakikishia maisha kiungo huyo baada ya kurudi Goodison Park.

Mchumba wa Dele, mrembo Cindy Kimberly ameoongoza kwenye watu wanaotuma ujumbe mara nyingi kumsapoti mpenzi wake na kuonyesha kwamba yupo naye bega kwa bega na anajivunia kwa ujasiri wa kufunga machungu yake.

Chanzo: Mwanaspoti