Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matusi, kejeli vilivyompa ulaji msuva

Msuva Uvumilivu Simon Msuva, akiwa na viongozi wa Yanga alipokwenda kuwatembelea

Mon, 29 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ninapoona Mtanzania akifanya vizuri nje ya Tanzania nafarijika kwa kuwa naamini mafanikio yao ni daraja kwa wale wengine waliopo nyuma yao.

Ili kutimiza hilo tunahitaji kuwa na wachezaji ambao ni imara uwanjani na kiakili, yaani fikra na malengo yao yawe yanatazama kesho na siyo leo hii.

Simba, Yanga na Azam FC ni klabu kubwa Tanzania, mchezaji kupata nafasi ya kucheza timu hizo ni mwanzo mzuri wa kujiandaa kisaikolojia kwenda nje kupambana, japokuwa siyo wote lazima wapitie timu hizo.

Miaka kadhaa iliyopita asilimia kubwa ya wachezaji wazawa walifeli wanapoenda nje ya nchi kwa kuwa hawakuwa tayari kiakili, ndiyo maana ilipofika muda wa kushindana uwanjani hawakuwa fiti pia.

Heko kwa Simon Msuva, akiwa Yanga, alikutana na upinzani mkali kutoka sehemu mbili, kwanza ndani ya uwanja kulikuwa na wachezaji wa kimataifa waliokuwa na uwezo mzuri, alipambana akawa na uhakika wa namba.

Nje ya uwanja napo alipofanya vibaya alikutana na matusi, kejeli, zomeazomea ya mashabiki wa timu yake, lakini Msuva ni kama zile kelele za kuzomea pindi alipofanya vibaya zilimkomaza na kumfanya kuwa sugu.

Aliendelea kupambana, akawa anarekebisha makosa, akapata namba, kelele zikamfanya aongeze umakini, kwani asilimia kubwa waliokuwa wakimzomea walikuwa wanataka afanye mambo mazuri uwanjani wamshangilie.

Ilipotokea nafasi ya kwenda nje kucheza soka, bahati ni kuwa kama ni ushindani alishauzoea, kukosolewa, kuzomewa kwake hakukuwa na kitu kipya, mwisho hali hiyo naamini ilichangia kumfanya awe bora katika ushindani wa kimataifa.

Msuva wa sasa hata unapomtazama uwanjani iwe ni ngazi ya klabu au timu ya taifa, unaona kabisa amepevuka, anafunga mabao klabuni na timu ya taifa, mchango wake ni mkubwa na mwili wake upo katika ‘shape’ nzuri ya kimichezo.

Inawezekana kelele za Wanayanga haikumfanya kuwa na kinyongo na ndiyo maana licha ya leo kuwa katika hali ya kula kuku kwa mrija, kwa maana ya kucheza soka nje akiwa na mafanikio mazuri kiuchumi na uwanjani, hana kinyongo na Wanayanga kwa kuwa anatambua bila kilichotokea awali akiwa Bongo inawezekana angechukua muda mrefu kuzoea mazingira ya nje.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live