Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu michezoni ni vita ya kudumu

Skysports Pogba Paul Juventus 6083136 Paul Pogba

Fri, 10 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

‘Binadamu wameumbwa kutafuta nafuu na kuongeza faida au mafanikio”. Hayo ni maneno ya wana saikolojia.Ukweli huu unadhihirika katika michezo ambako pamoja na mazoezi, lishe na mambo mengine yanawawezesha mwanamichezo kufanya vizuri lakini bado wengine huenda hatua zaidi na kutumia madawa ya kusisimua miili na kupata nguvu na kufanya kazi zaidi ya asili ya maumbile kiasi cha kuwaongeza kasi au pumzi .

Matumizi ya vitu mbalimbali kuongeza ufanisi katika michezo inasemekana yalianza miaka zaidi ya 2500 iliyopita wakati wa michezo ya Olimpiki ya asili huko Ugiriki.Yasemekana wanamichezo walitumia sharubati au juisi iliyokamuliwa kwenye mmea unaofanana na bangi. Na kwa kutumia mmea huo miili yao ilipata nguvu na kuwawezesha kufanya vema dhidi ya washindani wao.

Hata katika enzi ya warumi, inasemekana farasi walilishwa au kunyweshwa vitu vilivyowafanya kupata nguvu na kasi katika mashindano.

Katika miaka ya karibuni matumizi ya dawa za kusisimua mwili yalianza kuonekana dhahiri katika karne ya 19. Mara ya kwanza mtu kuondolewa mashindanoni kutokana na matumizi ya vitu vya kuongeza nguvu ni mwaka 1968 katika mashindano ya Olimpiki ya kiangazi wakati Mwanariadha wa Sweden Liljenwall kufuatia kamati ya Olimpiki ya kimataifa (IOC) kuanzisha kanuni za kudhibiti matumizi ya madawa ya kuongeza ufanisi michezoni.Liljenwall aliondolewa kwa kosa la kupiga bia mbili ili kuondoa woga kabla ya kuingia mchezoni.

Hivi karibuni mchezaji wa kimataifa wa Ufaransa na klabu ya Juventus, Paul Pogba alipimwa na kuonyesha vipimo chanya vya dawa za kusisimua mwili kosa ambalo kwa mujibu wa shirikisho la udhibiti wa madawa ya kuongeza nguvu duniani (WADA), Pogba anaweza kufungiwa kushiriki michezo kwa miaka minne.

Huko nyuma kulikuwa na matukio ya namna hiyo na mengi ya matukio yamekuwa katika michezo ya riadha na hasa katika unyanyuaji wa vitu vizito (weight lifting). Hata hivyo, kumekuwa na matukio maarufu au yaliyohusu wachezaji maarufu katika mpira wa miguu. Kesi maarufu za matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu katika mpira wa miguu ni zile zilizowahusu wachezaji Diego Maradona (1991, 1994, 1997), Edgar Davids (2001), Jaap Stam (2001), Pep Guardiola (2001), Rio Ferdinand (2003), Adrian Mutu (2004), Kolo Toure (2011) na Andre Onana (2021).

Wakala wa kudhibiti madawa ya kusisimua mwili duniani (WADA) ulianzishwa mwaka 1999 na Kamati ya Olimpiki duniani (IOC) ili kupambana na tatizo sugu la matumizi ya vitu vya kuongeza nguvu. Hata hivyo vita bado ni vigumu kwani usisimuaji mwili unaweza kufanyika kwa njia mbalimbali ikiwemo vyakula, madawa ya hospitali hata dawa za mswaki. WADA imekuwa ikitengeneza na kuratibu sheria na kanuni za udhibiti wa madawa haya duniani ili kuwa na kipimo kinachofanana kwa michezo yote na mataifa yote. WADA ndio wanatengeneza orodha ya madawa yaliyopigwa marufuku michezoni.

Shirikisho la vyama vya soka la kimataifa (FIFA) lina kanuni zake za kudhibiti madawa ya kuongeza ufanisi. Kanuni za Fifa zimetengenezwa kuendana na kanuni za WADA. Fifa inayo idara na wataalamu duniani wenye jukumu la kuhibiti na kubaini matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu.

Fifa ina utaratibu wa kupima wanamichezo wakati wanapokuwa mashindanoni na pia wanapokuwa nje ya mashindano.

Juhudi za kudhibiti madawa michezoni zinakumbana na vikwazo katika mazingira tofauti.Gharama za utafiti na kununua vyombo vya kupimia si rahisi kwa kila mamlaka za kimichezo. Mfano kwa nchi zinazoendelea ni kazi ngumu kuwa na wataalamu na nyenzo zote za kupima matumizi ya madawa ya kuongeza ufanisi michezoni.

Changamoto nyingine katika udhibiti wa matumizi ya vitu vya kuongeza nguvu ni kwamba kuna taasisi au hata vyama vya michezo vinavyobariki matumizi ya madawa haya vikiona kwamba kuna faida kwa timu au nchi kama inashinda bila kujali njia zilizotumika kupata ushindi.Mfano mzuri ni katika Taifa la Urusi ambapo iligundulika kubariki matumizi ya dawa hizi kwa wachezaji wake wa Olimpiki.

Pamoja na changamoto hizi, ni muhimu vita dhidi ya matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu michezoni iendelee kushika kasi.Matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu ni kinyume cha maadili ya kimichezo ya kushinda kwa njia halali na kwa utaratibu uliowekwa kwenye mchezo husika. Kuendelea kwa matumizi ya madawa haya kutawakatisha tamaa wanamichezo na mashabiki wanaopenda kuona washindi waliopita kwenye kanuni na matumizi ya nguvu zinazokubalika.

Matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu yanaweza kumsababishia mtumiaji matatizo ya moyo, figo, macho na hata kupoteza kumbukumbu. Kuna wanamichezo wengi wamepata matatizo ya kiafya na hata kupoteza uhai kutokana na matumizi ya madawa.

Pamoja na hatua za kisayansi na zisizo za kisayansi zinazochukuliwa, elimu kwa wanamichezo ni silaha muhimu sana katika kufanikisha vita hii. Ni muhimu wanamichezo kujua tangu utotoni kwamba michezo ni michezo na siyo suala la kufa au kupona. Na pia wajue kuwa mwanamichezo husifika si kwa ushindi tu bali pia sifa zitatokana na namna ushindi ulivyopatikana. Hii ni vita ya kudumu.

Chanzo: Mwanaspoti