Klabu ya Simba imemtangaza Selemani Matola kuwa kocha mpya wa timu za vijana huku Patrick Rweyemamu akiwa Mkuu wa Programu, huku Selemani Matola akisema wanatafuta wachezaji wenye vipaji.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Imani Kajula alisema hakuna kocha mzuri kama Selemani Matola na majukumu yake yatajumuisha timu za vijana za miaka 17 na 20.
"Ukichunguza timu kubwa za Afrika wana timu za vijana imara ambazo baadae wanaingia kwenye timu ya wakubwa. Leo (jana) tunatoa taarifa ya kuboresha timu za vijana, la kwanza ni Mkuu wa Programu za Vijana wa Simba, Patrick Rweyemamu."
Aidha Kajula alisema licha ya Rweyemamu kukabidhiwa majukumu hayo ila ataendelea kusimamia timu ya wakubwa kwa maana ya Meneja wa Simba na siku zijazo watasema watafanya nini ili kuboresha klabu yao. Akizungumza baada ya uteuzi huo, Matola alisema anaipongeza bodi na uongozi kwa kuona fursa hiyo kwani sio jambo geni kwao kutokana na awali kufanya hivyo na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana.
"Naamini sasa tutazalisha vitu vizuri zaidi ikiwezekana zaidi ya ile ya mwanzoni, sitawaangusha wapenzi wa Simba, tafanya wanachotaka mimi nifanye kwenye Youth Development (maendeleo ya vijana)." Kwa upande wa Rweyemamu alisema mpira hauwezi kuendelea bila uwekezaji wa vijana kwani walishawahi kufanya hilo kazi na matunda yake yanajulikana
"Kuanzia 2008 hadi 2015 tumetoa wachezaji takribani 250. Hakuna timu za Ligi Kuu Bara hadi madaraja ya chini hayajawahi kukosa wachezaji ambao wamepita kwenye timu ya vijana ya Simba," alisema na kuongeza;
"Tunatafuta wachezaji wenye vipaji, wenye uwezo, tunatengeneza ajira na tunapunguza mchakato wa usajili sababu kutafuta kitu ambacho hujawekeza kina gharama yake, hivyo lazima tuandae kizazi kipya."