Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matola awashusha presha Wanasimba

Seleman Matola Malawi Kocha msaidizi wa Simba Seleman Matola

Tue, 11 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Simba jioni ya juzi Jumapili kilikuwa uwanjani mjini Luanda nchini hapa kumalizana na wenyeji wao, Primeiro de Agosto katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku kocha msaidizi wa timu hiyo, Seleman Matola mapema amewahakikishia mashabiki kuwa utamu zaidi unakuja Msimbazi.

Matola alisema kuna makubwa zaidi yanakuja Simba kwa siku za mbeleni na kuwataka mashabiki wa timu hiyo kukaa mkao wa kula ili kuendelea kupata burudani bora zaidi.

Matola anayesaidiana na kocha mkuu, Juma Mgunda kuongoza benchi la ufundi la Simba alisema kwa namna walivyoanza msimu huu ni tofauti na ilivyo sasa.

Alisema Simba ya sasa imekuwa ikivutia kuitazama kutokana na kiwango bora ambacho imekuwa ikionyesha uwanjani pamoja na kupata matokeo mazuri katika mechi zake.

“Kwa sasa timu imeanza kukaa kwenye mstari, mimi pamoja na bosi wangu Juma Mgunda tunashirikiana vyema kuhakikisha wachezaji wanakuwa katika ubora ambao utatuwezesha kufanya vyema katika mashindano tunayoshiriki.

“Na kwa bahati nzuri wachezaji wanafanyia kazi kile ambacho tumekuwa tukiwaelekeza. Jambo la msingi kwa Wanasimba ni kuendelea kutuunga mkono ili tuweze kufanya vizuri zaidi. Timu inazidi kuimarika na nina imani kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutatimiza malengo yetu,” alisema Matola.

Simba chini ya Mgunda na Matola imeonekana kuwa tishio kutokana matokeo mazuri ambayo imekuwa ikiyapata huku ikicheza soka la kuvutia.

Kabla ya mechi ya juzi ugenini dhidi ya Agosto, Simba chini ya Mgunda na Matola, ilikuwa imeshinda mechi zote nne za mashindano, zikiwa mbili za Ligi Kuu Bara na nyingine kama hizo za Michuano ya CAF ikifunga jumla ya mabao tisa bila kuruhusu wavu wake kuguswa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live