Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matola arejea Msimbazi

Matola Shuleni Kocha msaidizi Simba Seleman Matola

Mon, 5 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa Simba na hata wadau wa soka kwa ujumla walikuwa wakijiuliza maswali mengi kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola, akimaliza kozi yake ya ukocha atarejea Msimbazi au atachimba moja kwa moja, majibu haya hapa.

Matola aliyekuwa visiwani Zanzibar kusoma kozi ya ukocha Leseni A ya CAF iliyokuwa ikifundishwa na wakufunzi kutoka nje ya nchi ametua jijini Dar juzi jioni akiwa amemaliza siku zake 10 za kwanza darasani na kusema anakisubiri kikosi cha timu hiyo kitoke mkoani Tanga baada ya kucheza dhidi ya Coastal Union jana ili kuendelea na majukumu yake.

Siku kadhaa zilizopita kulisambaa taarifa ya Matola kuondoka Simba kwenda kusoma kozi hiyo ya daraja la juu la ukocha, na sasa ifahamike kuwa amerejea jijini akiwa na akili kubwa zaidi.

“Nimerejea, nitaungana na wenzangu katika majukumu yangu kwenye mazoezi ya kwanza kujiandaa na mchezo wa ASFC ambao tutacheza dhidi ya Eagle FC, ila kwa sasa kila kitu kipo vizuri najiona kuwa nina vitu vingi zaidi vya kuongeza kwenye kikosi cha Simba,” alisema kocha huyo wa zamani wa Polisi Tanzania na Lipuli.

Inafahamika kuwa ufundi wa Matola umekuwa na msaada mkubwa kwenye kikosi cha timu hiyo na hata kwenye mazoezi ndiye amekuwa msimamizi pamoja na kufanya kazi chini ya Juma Mgunda ambaye ni kocha mkuu wa muda wa timu hiyo.

Kwenye mazoezi ya Simba wachezaji wa timu hiyo wamekuwa wakimtania kwa kumwambia mbinu anazotumia ni za makocha waliopita kwenye timu hiyo ambao alikuwa msaidizi wao akiwemo Sven Vandebroeck, Pablo Franco na Patrick Aussems.

Kwa siku kumi Matola amekuwa nje ya timu hiyo Simba imecheza michezo mitatu ilitoka sare 1-1 na Mbeya City na kupata ushindi 3-1 dhidi ya Polisi Tanzania na jana ilicheza dhidi ya Coastal Union.

Wakati Matola ameondoka uongozi ulimchukua kocha wa timu ya vijana, Mussa Mgosi kwenda kumuongezea nguvu Mgunda.

Kikosi cha Simba baada ya kurejea Dar kutokea Tanga kwenye mazoezi ya kwanza kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC), Matola atarudi kazini kuendelea na majukumu yake kama ilivyokuwa hapo awali huku taarifa zikieleza kuwa Simba wapo kwenye mchakato wa kuendelea kutafuta kocha mkuu.

Matola atakuwepo kwenye timu hiyo kwa miezi mitatu kufanyia kazi yale aliyofundishwa kwenye masomo yake huko Zanzibar baada ya hapo atarejea tena darasani kwa siku kumi.

“Baada ya miezi mitatu nitarudi tena shule kwa muda mfupi halafu nitarejea tena mimi ni mwajiriwa wa Simba,” alisema Matola ambaye ni kati ya makocha watatu wazawa waliozifikisha timu fainali ya FA.

Chanzo: Mwanaspoti