Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matola aachiwa msala Simba

Matola Suleiman SS Matola aachiwa msala Simba

Fri, 8 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Simba kilikuwa njiani kwenda jijini Tanga kutoka Morogoro kuwahi pambano la Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union litakalopigwa kesho Jumamosi, huku ikimkosa kocha mkuu, Abdelhak Benchikha katika mechi mbili zijazo akienda kushiriki kozi ya ukocha ya siku tano, akimuachia msala Seleman Matola na Farid Zemit.

Benchikha anaenda kufanya kozi ya kuboresha taaluma yake na atakuwa nje kwa siku tano hivyo atakosa mechi dhidi ya Coastal Union na Singida FG na kama atarudi mapema atakuwepo benchini watakapoivaa Mashujaa mechi ya Machi 15.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alikaririwa jana akisema kocha huyo aliyepoteza mechi yake ya kwanza katika Ligi Kuu juzi dhidi ya Tanzania Prisons, nafasi yake kikosini itashikiliwa na makocha wasaidizi, Zemit na Matola.

Simba itashuka dimbani kesho kwenye Uwanja wa Mkwakwani kuvaana na Coastal iliyotoka sare ya 1-1 juzi usiku mbele ya Azam FC, huku Wekundu wakitoka kupasuka 2-1 kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Benchikha ameondoka akiwa ameiongoza Simba kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiifunga Jwaneng Galaxy ya Botswana 6-0, huku timu hiyo ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo kwa pointi 36 baada ya mechi 16.

Katika hatua nyingine kocha wa timu ya soka ya wanawake ya Simba Queens, Juma Mgunda anatajwa kuwa mbioni kutua Singida Fountain Gate iliyovunja benchi lote la ufundi kutokana na matokeo mabaya iliyopata timu hiyo katika mechi saba zilizopita.

Benchi hilo lilikuwa chini ya kocha Msauzi, Thabo Senong na tayari mabosi wa klabu hiyo wameanza msako wa kocha mkuu mpya, huku Mgunda akitajwa kuwa ndiye mtu anayefukuziwa na klabu hiyo kubeba mikoba hiyo.

Mwanaspoti imepenyezwa taarifa kwamba Singida inamsaka kocha mkuu ili kuendeleza pale alipoishia Msauzi Senong aliyekuwa akiinoa timu hiyo baada ya Mjerumani Ernst Middendorp kutimkia Afrika Kusini.

Inaelezwa kwamba kiuchumi hali ya Singida haipo vizuri, jambo linawafanya na baadhi ya wachezaji ambao hawakutaka kutaja majina yao, kujiandaa kuvunja mikataba yao mwishoni mwa msimu huu, kama ilivyotokea kwa Bruno Gomes aliyeachana na timu hiyo hivi karibuni na anayetajwa kuwindwa na Ihefu.

Habari kutoka ndani ya Simba zinadokeza kuwa, Mgunda aliyebakisha muda mfupi wa mkataba yupo mbioni kutua Singida akiwa ni kati ya makocha waliopo kwenye rada za mabosi wa klabu hiyo ya Ligi Kuu Bara.

“Mgunda amebakiza mkataba mfupi, hivyo viongozi wa Singida wametuma maombi, kuwaruhusu wamuachie akawasaidie kumalizia msimu huu,” kilisema chanzo makini kutoka ndani ya Simba, huku kigogo mmoja kutoka Singida ambaye naye hakutaka jina litajwe amethibitisha juu ya msako wa kocha mpya.

“Ni kweli ishu ipo ila bado haijakamilika, wamezungumza na makocha wengi ila Mgunda ndiye ana asimilia kubwa ya kupatikana.”

Kwa upande wa Mgunda, aliyewahi kutamba na Coastal Union enzi akicheza kabla ya kugeukia ukocha akiinoa timu hiyo na kuajiriwa Simba misimu uliopita kabla ya kuhamishiwa Simba Queens, alipoulizwa juu ya taarifa hizo za kujiandaa kutua Singida alisema;

“Ndio kwanza nakusikia wewe ndugu mwandishi, ila waswahili wanasema dalili ya mvua ni mawingu, japo mawingu yanaweza yakatanda na mvua isinyeshe, ila kwa sasa karibuni kwenye mazoezi ya Simba Queens.”

Singida imekuwa na mwenendo mbaya katika Ligi Kuu ikicheza mechi saba bila ushindi tangu Novemba 27 ilipoichapa Coastal mabao 2-1, huku ikiwa imekimbiwa na baadhi ya mastaa waliohamia Ihefu ambayo imetangaza kuhamia kwenye Uwanja wa Liti, Singida kutoka Highland Estate uliopo Mbarali Mbeya.

Kwa sasa timu hiyo inashika nafasi ya 11 ikitoka ya nne iliyokuwa inaishikilia kabla ya ligi haijasimama kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 ikiwa na pointi 21 kutokana na mechi ya 19.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live