Mara baada ya matunda ya kikosi cha vijana kilichowahi kuanzishwa na kikosi cha Simba na baadaye kupungua makali sasa wameamka tena na kuanza pale walipoishia.
Simba iliyokuwa chini ya Meneja Patrick Rwyemamu na Kocha Selemani Matola waliunda kikosi kilichotoa vijana zaidi ya 200 baada ya kuzunguka kwenye timu za Ligi Kuu Bara pamoja na visiwani kwa miaka kadhaa.
Hata sasa bado nembo yao ipo, hawa ndiyo waliowazalisha Jonas Mkude ambaye sasa yupo Yanga, Hamis Ndemla, Ibrahim Ajibu pamoja na mastaa wengine wengi ambao wamewahi kutisha na wanaendelea kutisha kwenye soka.
Lakini kwa zaidi ya miaka 10, Simba haijafanikiwa kuzalisha mchezaji yeyote kutoka kwenye timu yao ya vijana ambaye ametikisa kwenye soka la Tanzania, hapa ndipo walipoona kuwa kuna jambo linatakiwa kufanyika ili waweze kurudi kule nyuma walipokuwa wakizalisha mastaa kibao.
Walijaribu kwa makocha mbalimbali lakini mpango wao ukafeli, wakakaa vikao na kuona wanatakiwa kurudi kwa Matola ambaye alifanya kazi kubwa miaka ya nyuma, kwanza walimtoa kwenye timu ya wakubwa, wakampeleka shule kusoma zaidi, wakati anakaribia kufuzu wakamtangaza kuwa kocha mkuu wa timu za vijana.
Baada ya kumpa timu hiyo, Matola akiwa na Patrick walianza mchakato wa kutafuta wachezaji kutoka sehemu mbalimbali, walienda Morogoro, Kigoma, Zanzibar na mikoa mingine mingi ndipo walipowakusanya mastaa kibao jijini Dar es Salaam na kuwaweka kwenye hosteli za Chuo cha Aridhi jijini Dar es Salaam ili waweze kujifua asubuhi na jioni, wakiendelea na mchakato wa kuwachuja, lakini wakiwa wamechukua wachezaji wenye umri chini ya miaka 17 tu.
WALIWAPATA HIVI:
Matola anasema kuwapata vijana zaidi ya 150 halikuwa jambo rahisi hata kidogo kwani iliwalazimu kuzunguka kwenye mikoa mingi ili kupata vipaji.
Anasema hawakuweza kumaliza mikoa yote lakini walifanikiwa kwenda kwenye mashindano ya Umisseta kitaifa yaliyofanyika Tabora na kukusanya vipaji kadhaa ambavyo wanaamini baadaye ndivyo vitavaa jezi ya Taifa Stars.
“Hatukuweza kwenda kila mkoa ila tulipita baadhi yake na tukamaliza kwa Tabora kulipokuwa mashindano ya wanafunzi wa sekondari kitaifa Umisseta.
“Zanzibar nako tulikwenda na kupata vijana, hivyo tumekusanya vipaji katika maeneo mbalimbali na hii litakwenda kuunda kitu kikubwa sana.”
ISHU YA UMRI
Kocha huyo wa zamani wa Lipuli ya Iringa amesema moja ya changamoto ambayo wamekutana nayo ni kupata wachezaji wenye umri sahihi kwani kuna ujanja mwingi sana unafanyika.
Anasema wengi wanafoji vyeti ili kupata fursa ya kucheza ila wanachokiangalia zaidi ni kipaji na sio kingine.
“Kawaida kwa wachezaji kufoji umri ili wapate nafasi ya kucheza, hilo siyo kwetu tu hata nje ya Tanzania wanafanya hivyo, lakini tumejitahidi kweli kuhakikisha kuwa kila kitu kinakwenda vizuri na tunapata wachezaji imara.
“Wapo wengine wanaletwa na watu tunaowafahamu na kuwaamini kuwa wanajua kuangalia vijana wenye uwezo, lakini tunafika mahali tunapata hofu kwenye umri.
“Sura ya mtoto haifichiki na ya mtu mkubwa pia hasa kwa wanaume, hivyo kuna wengine tunawajua kwa sura tu hata wakija na vyeti vya uongo, unajua huku nimekaa muda mrefu sana vijana wengi nawafahamu,” anasema Matola.
VIPAJI GHANA
Matola anasema kabla ya kuanza mchakato wa kuangalia vipaji hapa nchini alipata mwaliko wa kwenda Ghana kwa ajili ya kutazama mashindano ya vijana ya huko na kuona jinsi ambavyo nchi za wenzetu wanaandaa vijana wao.
“Nimeona wenzetu wamefanikiwa kuanzisha academy nzuri na za viwango lakini hawana vipaji vya kutuzidi huku na mafunzo ya muda mrefu ndio yaliyoweza kuwafanya wawe bora, lakini kwetu vipaji vipo vingi shida inakuja kwenye kuviendeleza kwa kuwa hakuna academy nyingi, hiyo ndiyo tofauti yetu kubwa.
“Hata mfumo wa kutafuta vijana hauna tofauti sana na sisi, ingawa wao wanawawapata wengi kutoka kwenye academy wakiwa wameshaanza kuandaliwa sisi tunawakuta mtaani, hii ina tofauti kubwa,” anasema Matola.
MIPANGO ZAIDI
Kocha huyo wa zamani Polisi Tanzania anasema mipango yao sio kuwa na kikosi cha vijana tu, bali academy kabisa itakayozalisha vijana wengi wenye vipaji, ambavyo vitadumu kwa muda mrefu.
“Yajayo yanafurahisha hatukwami kama zamani kwani tunajua kabisa kuwa tulikosea wapi na tunakwenda kujenga kikosi kikubwa, lakini pia mwendelezo ni kuhakikisha tunakuwa na akademi ya kudumu ambayo itakuwa chini ya Simba na itazalisha wachezaji wengi mahiri kwa miaka kadhaa ijayo.”
MTIBWA KIBOKO
Kocha huyo wa zamani msaidizi wa Taifa Stars, amesema Mtibwa Sugar ina timu nzuri ya vijana, lakini hilo haliwaumizi vichwa kwani mwisho wao umefika.
“Mtibwa tunawaheshimu lakini wana kazi ya ziada msimu ujao kwani hakuna kitu tutaacha kuanzia timu ya wakubwa mpaka vijana kwa kuwa kama timu ikiwa na vijana imara, hata ile ya wakubwa itakuwa bora,” anasema kocha huyo.
SIMBA DAY
Kocha huyo anasema wameandaa zawadi kubwa kwenye Simba Day, litakalofanywa na vijana hao na kila shabiki ataamini wanastahili kuvaa jezi ya timu yao.
“Vijana 60 wataingia uwanjani na kufanya makubwa ikiwemo kucheza mbele ya mashabiki wa timu hiyo ili wadhibitishe ubora wao nafikiri wataona ni jinsi gani walivyo bora, tunawaomba wawaunge mkono,” anasema Matola ambaye aliitumikia Simba kama mchezaji kwa miaka 10.