Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matokeo ya Pre Season yaibua maswali mengi Arsenal

Arsenal Utata Matokeo ya Pre Season yaibua maswali mengi Arsenal

Sat, 3 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Sare moja. Ushindi mmoja. Kipigo kimoja. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwenye pre-season ya Arsenal huko Marekani na kumfanya kocha Mikel Arteta kuwa na maswali mengi ya kujiuliza wakati kikosi hicho kikirejea England.

Kocha huyo wa Arsenal hakuwa na huduma ya mastaa kadhaa wa kikosi chake cha kwanza kwa sababu walikuwa wameongezewa siku za mapumziko baada ya kukamilika kwa fainali za Euro 2024 na bahati nzuri kwake kwenye mechi alizocheza dhidi ya Bournemouth, Manchester United na Liverpool hakukuwa na mchezaji yeyote aliyepata majeraha.

Wakati akitumia damu changa za mastaa wa kutoka kwenye akademia, Arteta pia alimkaribisha beki wake mpya wa Pauni 42 milioni, Riccardo Calafiori, aliyemsajili kutoka Bologna. Lakini, wakati Arsenal ikijiandaa na mchezo wa kwanza kwenye Ligi Kuu England dhidi ya Wolves, Agosti 17, kuna vitu gani Arteta anapaswa kuvifanya ili msimu ujao uwe tofauti na misimu miwili iliyopita? Kuna maswali mengi kuhusu Arsenal.

Je, Arsenal inahitaji straika? Mpango wa Arsenal kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi ni wazi kabisa inahitaji huduma ya mshambuliaji wa kati na kama kutakuwa na chaguo sahihi sokoni basi bila shaka kocha Arteta anapambana kupata huduma yake.

Mastraika wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres na Newcastle United, Alexander Isak wamefuatiliwa sana na timu hiyo baada ya kukosa huduma ya Benjamin Sesko, aliyekuwa chaguo lao la kwanza kuamua kusaini mkataba mpya wa miaka mitano kubaki Red Bull Leipzig.

Hata hivyo, eneo hilo bado linahitaji mtu wa maana ili kufanya kazi nzuri zinazofanywa na mawinga Bukayo Saka na Gabriel Martinelli pamoja na viungo matata kama Martin Odegaard kuzaa matunda.

Eddie Nketiah anahusishwa na mpango wa kuondoka kwenda Marseille, hivyo hilo ni eneo ambalo piga ua, Arteta atahitaji kuleta mtu wa kuja kupokezana nafasi na Gabriel Jesus, la sivyo atalazimika kumtumia Kai Havertz kwenye nafasi ya straika kwa msimu ujao.

Je, Ethan Nwaneri yupo tayari? Kuna kitu kikubwa kimeonyeshwa na kinda huyo wa kutokea kwenye akademia ya Arsenal, kwamba anaweza kufanya kitu ndani ya uwanja. Nwaneri aliandika historia Septemba 2022 wakati alipokuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kupata nafasi ya kucheza kwenye mechi ya Ligi Kuu England, alipofanya hivyo akiwa na miaka 15 na siku 181 ugenini dhidi ya Brentford.

Kisha alitokea benchini kwenye mechi ya ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya West Ham United kwenye Ligi Kuu England na kumfanya kocha Arteta kusisitiza kwamba mchezaji huyo sasa ataanza kutumika. Kwa sasa umri wake ni miaka 17 na alitumika kwenye mechi zote za pre-season, alipocheza winga dhidi ya Bournemouth kwenye kiungo dhidi ya Man United na alitokea benchini katika dakika 20 za mwisho kumbadili Havertz kwenye kipute cha Liverpool. Ndiye aliyeasisti bao la Jesus kwenye mchezo dhidi ya Man United.

Sambamba na mastaa kadhaa kwenye safu ya kiungo kama Thomas Partey, Jorginho, Declan Rice na Martin Odegaard, Arteta mpango wake ni kuongeza sura mpya kwenye eneo hilo kutokana na kuhitaji saini ya staa wa Real Sociedad, Mikel Merino.

Je, Jurrien Timber atarudi kugombea nafasi yake? Kocha Arteta aliweka wazi msimu uliopita kwamba alilazimika kubadili mbinu zake za kiuchezaji ili kumpa nafasi Jurrien Timber ya kutamba kwenye beki ya kushoto. Mpango huo ulikomea baada ya dakika 50 tu katika mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu England dhidi ya Nottingham Forest – baada ya beki huyo aliyenaswa kutoka Ajax kwa ada ya Pauni 38.5 milioni kuumia mguu.

Majeraha hayo yalimweka nje ya uwanja kwa muda mrefu na kurejea kwenye mchezo wa mwisho wa msimu uliopita dhidi ya Everton huku akiamini kipindi hiki cha pre-season kitamrejesha kwenye ubora wake.

Kama hakutakuwa na shida yoyote bila shaka Mdachi huyo ataanza kwenye mechi ya Emirates, dhidi ya Wolves. Lakini, mwenyewe anapaswa kufahamu kwamba kuna beki mwingine wa kushoto ameletwa kwenye dirisha hili, Riccardo Calafiori, hivyo kutakuwa na ushindani wa nafasi.

Arteta alimleta Calafiori baada ya kuona Oleksandr Zinchenko na Jakub Kiwior wameshindwa kufanya vizuri kwenye eneo hilo. Lakini, kitu kizuri kutoka kwa Timber ni kwamba anaweza pia kucheza kama beki wa kati, ambapo alitumika hapo kwenye mechi za kirafiki dhidi ya Bournemouth na Man United huko Los Angeles, Marekani.

Chanzo: Mwanaspoti