Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matampi, Diarra vita yao ni kali Ligi Kuu

Diarra Matampi WA0001 Matampi, Diarra vita yao ni kali Ligi Kuu

Thu, 16 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Yanga ikijihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ushindani sasa unaonekani kuhamia kwa wachezaji katika kuzisaka takwimu bora zinazoweza kuwaweka katika nafasi nzuri ya kushinda tuzo binafsi mwishoni mwa msimu.

Ukiweka kando ushindani ambao ulianza kuonekana mapema wa kuwania tuzo ya mfungaji bora ambao unawahusisha Stephane Aziz Ki wa Yanga na Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam FC, vita nyingine ambayo inaonekana inazidi kuwa tamu mwishoni mwa msimu ni ile ya kipa aliyecheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao ambayo inahusisha Djigui Diarra wa Yanga pamoja na Ley Matampi wa Coastal Union.

Wakati zikibakia raundi tatu kwa Ligi Kuu msimu huu kufikia tamati, Diarra na Matampi ndio vinara kwa kucheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao msimu huu ambapo kila mmoja nyavu zake hazijaguswa katika mechi 13 za Ligi.

Kitendo cha kuruhusu bao katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar katika ushindi wa mabao 3-1 ambao Yanga iliupata, kimeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kumrudisha nyuma Diarra ambaye sasa atalazimika kutoruhusu bao katika mechi tatu zilizobakia dhidi ya Dodoma Jiji, Tabora United na Tanzania Prisons kisha kuombea Matampi afungwe ili arudie alichokifanya msimu uliopita ambapo alimaliza akiwa kinara kwa kucheza idadi kubwa ya mechi za Ligi Kuu bila kuruhsu bao.

Lakini ikiwa kinyume, Matampi ama anaweza kuwa kinara iwapo hatoruhusu bao katika mechi tatu ambazo timu yake imebakiza dhidi ya Kagera Sugar, JKT Tanzania na KMC.

Kocha wa zamani wa makipa wa Yanga, Peter Manyika alisema Diarra na Matampi wameonyesha kiwango cha kuvutia msimu huu.

"Wote wawili ni makipa wenye uzoefu mkubwa na wameongeza kitu kwenye ligi yetu na uwezo wao wa uwanjani hautii shaka na ndio maana unaweza kuona walivyoweza kuimarisha safu za ulinzi za timu zao.

"Mimi nawatazama kwa jicho chanya kwamba ni makipa ambao wanaongeza kitu fulani katika ubora wa makipa wetu wazawa ambao wanapaswa kujifunza kutoka kwao," alisema Manyika.

Kipa wa zamani wa Simba, Iddi Pazi 'Father' alisema kuwa Diarra na Matampi wameongeza chachu katika ligi.

"Kunapokuwa na makipa ambao wanaonyeshana ushindani, washambuliaji wanaimarika lakini pia inasaidia kuboresha makipa wengine. Hata yule kipa wa Simba,. Ayoub (Lakred) naye nimemtazama ni mzuri sana na nazipongeza timu kwa kuleta makipa bora," alisema Pazi.

Beki wa kulia wa Yanga, Yao Attohoula naye anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Mohammed Hussen wa Simba, Pascal Msindo wa Azam FC na Rahim Shomari wa KMC katika chatri ya mabeki waliosaidia upatikanaji wa mabao mengi kwenye vikosi vya timu zao msimu huu.

Yao ambaye hadi sasa amepiga pasi saba za mwisho huku akiongoza, ananyemelewa kwa ukaribu na Mohamed Hussein ambaye ana pasi sita za mabao wakati Shomari na Msindo kila mmoja ametoa usaidizi wa bao mara tano.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa wachezaji hao, shughuli ya kuwania ufungaji bora baina ya Aziz Ki na Fei Toto nayo inaonekana inaweza kuamriwa hadi katika mechi ya mwisho ya ligi msimu huu kutokana na mwendelezo mzuri wa kufumania nyavu ambao wawili hao wamekuwa nao katika Ligi Kuu msimu huu.

Wawili hao kila mmoja amefumania nyavu mara 15 katika Ligi Kuu msimu huu na timu zao zimebakisha mechi tatu kila moja hivyo yeyote ambaye atachanga vyema karata zake na kufanya vizuri katika mechi zilizobakia, atajiweka katika nazingira mazuri ya kupata tuzo hiyo.

Ikitokea wawili hao wakawa sawa katika ufungaji, ni lazima apatikane mshindi mmoja kwa mujibu wa kanuni tofauti na msimu uliopita ambapo Fiston Mayele wa Yanga na Saido Ntibazonkiza wa Simba walilingana.

Kanuni ya 11 ya Ligi Kuu msimu huu, imeainisha vigezo vitakavyotumika kupata mfungaji bora iwapo wachezaji wawili au zaidi wamefunga idadi sawa ya mabao. "Magoli yaliyofungwa kwa njia ya kawaida yatakuwa na alama mbili (2) na magoli yaliyofungwa kwa njia ya penalt yatakuwa na alama moja (1). Mchezaji mwenye alama nyingi atakuwa mshindi.

"Endapo watalingana alama, mchezaji aliyecheza muda mchache zaidi atakuwa mshindi. Endapo watafanana katika vigezo vyote viwili hapo juu, mchezaji aliyefunga mabao mengi ugenini atakuwa mshindi.

"Katika mashindano ya mtoano, mshindi atakuwa mchezaji ambaye timu yake imefika hatua ya juu zaidi kuliko mwingine na endapo hatua hii haitotoa mshindi, kipengele cha i-iii vitatumika kwa mpangilio wake," inafafanua kanuni hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live