Vigogo wa shirikisho la soka Tanzania (TFF), wakiongozwa na Katibu Mkuu, Kidao Wilfred huku akiwemo Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almas Kasongo bado wanaendelea na vikao vya hapa na pale kujadili namna ambavyo mabingwa wa Sudan, Al Hilal watashiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao wa 2024/25.
Al Hilal ambao wamekuwa wakishiriki michuano ya kimataifa iliwabidi kutuma barua ya maombi ya kushiriki Ligi Kuu Bara kupitia chama chao cha soka - SFA kwenda TFF kutokana na ligi ya nchini kwao kusimama.
Kwanini ligi yao imesimama? Hii ni kutokana na mapigano yanayoendelea katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum na kwingineko yote hayo ikiwa ni matokeo ya moja kwa moja ya mvutano wa madaraka ndani ya uongozi wa jeshi la nchi hiyo.
Sasa Al Hilal ikitua katika Ligi Kuu Bara Itakuwaje? Hilo ndilo swali ambalo wadau wengi wa soka nchini limekuwa vichwani mwao tangu kuripotiwa kwa taarifa za ujio wa timu hiyo msimu ujao.
Katika mahojiano maalumu ambayo Mtendaji Mkuu wa TPLB, Kasongo ambayo amefanya na Mwananchi Digital, amethibitisha juu ya taarifa hizo huku akienda mbali zaidi kwa kusema kwa sasa wapo kwenye vikao ambavyo vitatoa picha kamili juu ya maombi hayo, akidai inawezekana kwa Al Hilal kushiriki Ligi Kuu msimu ujao.
"Ni taarifa ngeni lakini itoshe kusema uhalisia weke ni kweli Al Hilal ya Sudan iliomba kuweza kuwa sehemu ya Ligi Kuu utakuja kuona kwamba Sudan kwa takribani miaka miwili kumekuwa na vurugu kubwa amani haipo shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii zimesimama," amesema.
"Makundi tofauti yanatoka Sudan kwa ajili ya kuendeleza kazi zao kuna kundi la timu ambalo limeona kama timu haiwezi kukaa tu kwa hiyo wameomba. Ni kweli TFF wamepokea maombi. Sekretarieti ya TFF ikiongozwa na katibu wanawajibu wa kukaa na kuchakata wakijiridhisha wanapeleka katika kamati ya utendaji.
"(Kule) wanapokea, wanajadili na kufanya uamuzi. Kwa hiyo nisingependa kuwa msemaji katika hilo kama mtendaji mkuu nahudhuria kwenye kikao hicho, lakini kama sekretarieti na sio kama mjumbe pale kunapokuwa na jambo la ligi kwa ajili ya ufafanuzi."
Haya ni maswali matano kuhusu ushiriki wa Al Hilal msimu ujao kwenye Ligi Kuu Bara ambayo pia yamekuwa vichwani mwa wadau mbalimbali wa soka nchini wanayojiuliza wakati huu ambao bado TFF haijaeleza kwa kina juu ya namna itakavyokuwa kutokana na vikao vinavyoendelea.
1. Wanachezaje bila ya kuwa kwenye msimamo? Kwa mujibu wa taarifa zilizopo ni kwamba Al Hilal haitakuwa sehemu ya msimamo wa Ligi Kuu Bara, lakini michezo yao itakuwa kwenye ratiba kama ilivyo michezo mingine.
2. Mechi zao zitapewa uzito? Ikiwa hawatakuwa sehemu ya msimamo wa Ligi Kuu Bara kama inavyoelezwa wanaweza wasipate kile ambacho wamelenga kukipata kwenye ligi maana klabu mbalimbali zinaweza zisiupe uzito mchezo kati yao na timu hiyo na miongoni mwa sababu ambazo zimeisukuma timu hiyo kushiriki Ligi Kuu ni ushindani uliopo.
3. Mfumo wa mechi utakuwaje? Je watakuwa wakicheza nyumbani na ugenini kama ilivyo kwa timu nyingine kwenye ligi? Maskani yatakuwa Dar kama ilivyo kwa Simba, Yanga, Azam FC na KMC?
4. Watapata mgawo wa udhamini? Fungu la udhamini kwenye ligi ambalo limekuwa likitolewa kwa mafungu kwenye kila msimu, husaidia katika uendeshaji wa klabu. Al Hilal watashiriki huku wakijigharamikia wenyewe au nao watakuwa sehemu ya mgawo kama ilivyo kwa timu nyingine? 5. Kitendo cha timu kuongezwa kwenye ratiba ya msimu ina maana klabu husika zitaingia gharama zaidi ya bajiti zao ambazo wamekuwa wakiziweka kwa msimu mzima. Gharama zitakuwaje? Je itakuwaje kwenye hilo au kutakuwa fungu maalumu ambalo TFF na wadhamini watalitoa kwa ajili ya kufanikisha hilo?
KWA WENZETU Yapo mataifa mengi barani Ulaya ambayo yalizikaribisha timu kutoka nchi nyingine kushiriki ligi kutokana na sababu mbalimbali, mfano mzuri ni Union Esportiva de Bossost ya Hispania ilikwenda Ufaransa kukipiga.
Timu hiyo iko katika Bonde la Aran huko Catalonia, Hispania Kaskazini na inachezea nchini Ufaransa kutokana na hali ya hewa. Theluji ya majira ya baridi imekuwa kikwazo kwao kusafiri kwenda katika maeneo mengi ya nchi yao hivyo ni rahisi kwao kwenda Ufaransa.
Mfano mwingine ni kwa FC Busingen ya Ujerumani iligonga hodi Uswisi. Hii ndio timu pekee kutoka Ujerumani kucheza nchi nyingine. Kulingana na maelezo ya Busingen, hicho ni kipande cha ardhi ambacho ni sehemu ya Ujerumani, lakini kipo Uswisi.
Klabu hiyo inashindana katika mfumo wa Ligi ya Uswisi. Hata England zipo timu kutoka Wales na Scotland ambazo zinashiriki katika ngazi tofauti ya ligi nchini humo na zinachukuliwa kama zilivyo timu nyingine kwenye ligi.