Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastraika washika karata ya Taifa Stars

Msuva X Samatta Mastraika washika karata ya Taifa Stars

Wed, 15 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Takwimu za mechi tano zilizopita za mashindano zinawalazimisha washambuliaji wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kufanya kazi ya ziada katika mechi mbili zijazo za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Niger na Morocco zitakazochezwa ugenini na nyumbani Novemba 18 ni 21 ili ipate matokeo mazuri.

Kibarua cha kwanza cha Taifa Stars kitakuwa dhidi ya Niger huko Morocco, Novemba 18 na Novemba 21 itaikaribisha Morocco katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa ni michezo ya kundi E la mashindano hayo ambalo pia lina Zambia na Congo.

Katika mechi tano zilizopita za mashindano tofauti, safu ya ushambuliaji ya Stars imefunga mabao mawili ikiwa ni wastani wa bao 0.4 kwa mchezo na yamefungwa katika mechi mbili huku mechi tatu ikimaliza bila kufunga bao.

Michezo ambayo Stars imefunga mabao hayo mawili ni dhidi ya Uganda na Niger kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) ambapo katika kila moja iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Ilitoka sare ya bila kufungana katika mechi yake ya mwisho ya kimashindano ambayo ilikuwa ya kuwania kufuzu Afcon dhidi ya Algeria ugenini na mechi nyingine mbili ambazo haikufunga bao ni dhidi ya Uganda katika kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (Chan) ambapo ilifungwa nyumbani kwa bao 1-0 kisha ikapoteza kwa mabao 3-0 ugenini.

Mshambuliaji ambaye amekuwa akiiweka mgongoni Stars katika mechi za hivi karibuni ni Saimon Msuva anayeitumikia JS Kabylie ndiye amepachika mabao yote mawili ambayo imeyafunga katika mechi tano zilizopita.

Lakini safari hii mambo yanaweza kuwa mazuri kwa Stars kwani inazikabili Niger na Morocco katika kipindi ambacho mshambuliaji na nahodha wake, Mbwana Samatta ameonekana kufanya vizuri katika klabu ya PAOK ya Ugiriki ambapo hadi anajiunga na kambi ya timu ya taifa, ametoka kufunga mabao mawili katika mechi mbili mfululizo dhidi ya Aberdeen kwenye mashindano ya Uefa Conference League na dhidi ya Panaitolikos katika Ligi Kuu Ugiriki.

Mambo hata hivyo yanaonekana kutokwenda vizuri kwa Msuva ambaye hajafunga bao lolote katika mechi tatu za Ligi Kuu Algeria akiwa na kikosi cha JS Kabylie.

Kocha msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Morocco alisema wana imani na wachezaji waliowaita kwamba wataipa matokeo mazuri ingawa wana michezo migumu.

“Tuna mechi mbili ngumu dhidi ya Niger na Morocco, lakini tuna imani na ubora wa wachezaji wetu na maandalizi tuliyofanya kupata matokeo mazuri. Dhidi ya Niger mechi haitakuwa rahisi kwa sababu tumeshatoka kucheza nao mechi mbili siku za hivi karibuni na hii itakuwa ya tatu na zote hawakuwahi kutufunga hivyo watakuja wamejipanga vilivyo, lakini Morocco ni timu nzuri na bora Afrika.

“Sio mechi nyepesi lakini vijana wetu watapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema Morocco.

Naye Msuva alisema: “Tuko hapa kwa ajili ya kupambania nchi yetu, kupambania taifa letu. Kuwepo katika timu ya taifa ni fahari.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live