Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastraika wanavyoweka ubutu Azam FC

Amam Straika Nyota wa Azam FC katika moja ya mechi zao za lkirafiki

Mon, 15 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kila mdau wa soka nchini anahoji namna mwenendo wa Azam FC ulivyo hadi sasa kwenye Ligi Kuu Bara wanazoshiriki baada ya kuonyesha hawana makali mengi kama ambavyo ilikuwa inatarajiwa.

Azam msimu huu imefanya usajili mkubwa ikiwasajili Yvan Mballa, Edward Manyama, Paul Katema, Charles Zulu, Keneth Mguna, Idiris Mbombo na Rodgers Kola.

Upande wa ushambuliaji Azam mchezaji tegemeo ni Prince Dube na anapokuwa majeruhi benchi la ufundi linakuwa na wakati mgumu. Licha ya usajili uliofanywa lakini pengo la Dube linaonekana wazi.

Makala haya yanaelezea namna washambuliaji walivyo na ubutu wakati huo huo safu yao ya ulinzi inavyoruhusu mabao.

MECHI 9 ZA MASHINDANO

Hadi sasa wamecheza mechi tisa za mashindano yote wanayoshiriki msimu huu wakiwa chini ya kocha wao George Lwandamina akisaidiana na Bahati Vivier.

Imecheza mechi nne za kimataifa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Horseed (Mbili) na Pyramid ingawa walitolewa kwenye mashindano hayo na sasa nguvu zao zipo Ligi Kuu Bara pekee.

Upande wa mechi za ligi, wamecheza mechi tano, wanashika nafasi ya nane kwenye msimamo.

WAMESHINDA MECHI NNE

Mechi zote walizocheza wameshinda michezo minne, miwili kimataifa dhidi ya Horseed hatua ya awali na kukata tiketi ya kucheza raundi ya kwanza Kombe la Shirikisho Afrika.

Upande wa ligi imeshinda mara mbili dhidi ya Namungo bao likifungwa na Idris Mbombo, walishinda pia dhidi ya Geita Gold mfungaji akiwa ni Rogers Kola.

KUPOTEZA MARA TATU, SARE MBILI

Azam kwenye mechi zake tano za mashindano kiujumla wamepoteza mara tatu dhidi ya Pyramid 1-0, Polisi Tanzania 2-1 bao la kufutia machozi likifungwa na Idd Seleman ‘Nado’ na mchezo mwingine ni Yanga 2-0.

Wakati huo huo kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Pyramid uliochezwa Chamazi, Azam ilitoka suluhu na timu hiyo huku mchezo wa ligi dhidi ya Coastal ulimalizika kwa sare 1-1 Uwanja wa Mkwakwani.

MABEKI WAWILI WATUPIA

Wakati washambuliaji wakiwa na ubutu wa kutupia mipira wavuni basi mabeki wa timu hiyo wao wanaifanya kazi yao kwa ufasaha baada ya Lusajo Mwaikenda na Daniel Amoah kufanya hivyo.

Mwaikenda alifunga katika mchezo wa awali kombe la Shirikisho dhidi ya Horseed kwenye ushindi wa bao 3-1 huku Amoah akifunga kwenye Ligi dhidi ya Coastal Union mchezo ukimalizika kwa sare 1-1.

MASTRAIKA MABAO MATATU TU

Pamoja na kwamba msimu huu wamesajili nyota wengi wakiwemo washambuliaji wakiongozwa na Kola pamoja na Mbombo lakini bado wamekuwa na mwendo wa kusuasua.

Hadi sasa Mbombo ana mabao mawili tu moja akifunga mchezo wa kimataifa dhidi ya Horseed huku bao lingine akifunga dhidi ya Namungo akiipatia ushindi timu yake bao 1-0.

Wakati huo huo mawinga Idd Seleman ‘Nado’, Ayoub Lyanga na Ismail Aziz ‘Kada’ wakiwa sehemu ya wachezaji ambao wamechangia mabao ya timu hiyo msimu huu kila mmoja akifunga bao moja moja.

MABAO NANE MASHINDANO YOTE

Kwa ujumla katika mashindano yote wamefunga mabao nane hadi sasa, huku manne yakiwa ya Kombe la Shirikisho Afrika, mengine manne yakiwa kwenye ligi wakati huo huo wakiruhusu nyavu zao ziguswe mara tano hadi sasa.

WADAU WAFUNGUKA

Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba alisema kama timu hiyo inahitaji ubingwa inabidi waamke na kufanya vizuri mapema kwa sababu biashara ni asubuhi na jioni mahesabu huku akisema kitendo cha kuwasimamisha wachezaji wao wakongwe nacho kinachangia kwa kiasi fulani timu kuwa na mwenendo wa kusuasua.

“Pasi za mabao msimu uliopita zilikuwa zinapigwa na nani?, sawa wachezaji wamefungiwa kwa muda usiokuwa na kikomo sasa nadhani kocha ndio anajua kwanini wamesimamishwa na lini watarudi,” alisema Kawemba.

Mshambuliaji wa zamani Yanga, Hery Morris alisema; “Hawa wachezaji ambao wanacheza sasa hivi hawaonyeshi kubadilika, ni muda wa kukaa nao chini wale ambao waligombana nao na kumaliza matatizo ili warejee kikosini.

“Upande wa ushambuliaji yule Mbombo yupo fiti lakini ni mzito sana, unapokuwa mshambuliaji unatakiwa pia uwe na uwepesi kidogo ambao utakusaidia kwenye kukimbizana na mabeki.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz