Nyota wa zamani wa AFC Leopards,Shabana FC na timu ya taifa ya Kenya (Harambee Stars) ambaye kwa sasa ni kocha mkuu wa Dodoma Jiji FC Francis Baraza amefunguka kuwa ili kufikia malengo ambayo timu imejiwekea msimu huu ni lazima afanyie kazi mapungufu ambayo yapo katika safu ya ushambuliaji.
Safu ya ushambulaiji ya Dodoma Jiji inaongozwa na wachezaji Hassan Mwaterema, Christian Zigah, Meshack Mwamita, Idd Kipagwile, Yasin Mgaza na Anuary Jabir amejiunga na timu hiyo dirisha dogo akitokea Kagera Sugar.
Katika mechi 16 ambazo timu hiyo imecheza sawa na magoli iliyofungwa imepachika magoli 13 pekee huku ikikusanya alama 19 zinazowaweka kwenye nafasi ya nane baada ya kupata ushindi mechi tano,sare nne na vichapo saba.
Baraza alisema licha ya timu kucheza vyema lakini changamoto kubwa iliyoko ni kushindwa kugeuza magoli nafasi ambazo wanazitengeza ili kuweza kupata matokeo mazuri.
Alisema anaumiza kichwa kulifanyia kazi kusudi katika mechi ambazo ziko mbele yao waweze kupata matokeo ambayo itaendeleza morali ya kupambania kufikia malengo ya timu kwa msimu huu.
“Ndio lazima nifanyie kazi safu ya ushambualiaji ili zile nafasi tunazokosa zote kwa kiasi kikubwa ziwe ni magoli ambayo pia itatufanya tumalize nafasi za juu,” alisema Baraza. Mchezaji huyo wa zamani wa Transcom ya Nakuru, miaka ya 1991-92 lakini Rivatex ya Eldoret mwaka 1993-96 alisema katika mechi ambazo ameiongoza Dodoma Jiji kuna muunganiko mkubwa baina ya wachezaji wa zamani pamoja na wale wa dirisha dogo jambo ambalo linampa matumaini makubwa ya kufanya vizuri.
“Naamini kama wale wachezaji wetu wawili vibali vyao vitapatikana mapema kisha wakaja kuongeza ngumu mabadiliko yatakuwa makubwa sana,” aliongeza Baraza.
Kocha huyo alisema Ligi sio nyepesi kila timu imejipanga kuhakikisha inafanya vizuri huku akiamini mambo makubwa yanakuja kwa upande wao.