Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa wote Simba niwakute kambini - Kocha Benchikha

Kocha Abdelhak Benchikha Kocha Benchikha

Sun, 26 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya mechi ya jana dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast, kikosi cha Simba kimepewa mapumziko ya siku moja na kesho kitarejea mazoezini huku kocha mkuu mpya wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha akianza mikwara kwa kuwataka mastaa wote wa timu hiyo kambini, ili aanze mambo.

Simba ilikuwa uwanjani jana jioni kuvaana na Asec kwenye mchezo wa Kundi B wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni saa chache tangu mabosi wa klabu hiyo kumalizana na Benchikha aliyeizuia Yanga kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika wakati akiinoa USM Algers.

Benchika anakuchukua nafasi ya Mbrazil, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyefutwa kazi baada ya kichapo cha 5-1 ilichopata timu hiyo mbele ya Yanga, alitambulisha Ijumaa usiku, akiwa kwao Algeria na jana Jumamosi alianza safari ya kuja Bongo kabla ya kesho Jumatatu ataanza rasmi kazi ndani ya kikosi hicho.

Mwanaspoti limebahatika kuzungumza na kocha huyo kwa njia ya simu akiwa kwao Algeria na kuweka mipango yake mara atakapoanza kazi na alifunguka kitu cha kwanza ni kutaka kuwaona wachezaji wote kisha ataanza kusuka mipango.

“Naijua Simba ni timu nzuri na imekuwa na ushindani mkubwa katika bara hili la Afrika, nina furaha kujiunga nao. Kwa sasa siwezi kusema chochote kuhusu mipango yangu binafsi, naenda kutimiza mipango ya timu kutokana na makubaliano yetu,” alisema Benchikha na kuongeza;

“Kitu cha kwanza nitakachofanya ni kukutana na wachezaji wote kambini, nataka nionane na kila mmoja na kutambua uwezo wake na baada ya hapo nitaanza kutengeneza timu nikiendeleza nilipoikuta.”

Pia kocha huyo aliyetwaa mataji nane hadi sasa ikiwemo CAF Super Cup alilobeba mara mbili na Kombe la Shirikisho Afrika alilotwaa msimu uliopita akiwa na USM Algers akiitibulia Yanga kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2 alisema anajua kiu ya Simba ni kufanya vizuri zaidi kimataifa na anauzoefu na michuano hiyo hivyo yupo tayari kwa vita.

“Mashindano ya kimataifa ndio shauku kubwa ya timu nyingi Afrika ikiwemo Simba. Kwa bahati nzuri nimekuwa kwa muda mrefu kwenye soka la Afrika nalijua vizuri na nimefanya kazi kwa mafanikio barani hapa, nipo tayari kushirikiana na Simba kuanzia viongozi, benchi la ufundi na wachezaji kuhakikisha tunafika malengo,” alisema Benchikha.

Benchikha ataanza kuiongoza Simba kwenye mechi ya michuano ya CAF, itakayopigwa Desemba 2 ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, ukiwa ni mchezo wa pili kwenye kundi la timu hizo lenye Wydad Casablanca ya Morocco.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live