Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa wenye thamani kubwa sokoni kwa kuzingatia umri

Haaland Vs Young Boys Mastaa wenye thamani kubwa sokoni kwa kuzingatia umri

Thu, 9 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Achana na bei ambayo klabu inaweza kuamua kumuuza mchezaji wake kama kutakuwa na timu inayomhitaji. Kuna mchezaji mwenye thamani ndogo sokoni, utauziwa kwa bei kubwa.

Kwa mujibu wa Transfermarkt, hawa ndio mastaa wenye thamani kubwa sokoni katika kila umri, kuanzia miaka 16 hadi 40, ambayo inawapa ruhusa ya kuonyesha kitu uwanjani.

16: Lamine Yamal – Euro 50 milioni

Licha ya kwamba umri wake ni mdogo sana ambapo haruhusiwi kupiga kura wala kulewa, Yamal tayari ameshakuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Barcelona na timu ya taifa ya Hispania. Thamani yake ni Euro 50 milioni.

17: Warren Zaire-Emery – Euro 50 milioni

Ufaransa ina kikosi kipana sana, lakini haitashangaza kama Zaire-Emery atajumuishwa kwenye Euro 2024. Kinda huyo ana kipaji matata kwelikweli, akionyesha hilo huko Paris Saint-Germain. Thamani yake ni Euro 50 milioni.

18: Mathys Tel – Euro 50 milioni

Licha ya kwamba Harry Kane ni chaguo la kwanza huko Bayern Munich kwenye eneo la ushambuliaji, Tel bado ameonyesha uhai mkubwa, akifunga mara sita na asisti moja katika dakika 330 alizocheza. Thamani yake Euro 50 milioni.

19: Gavi – Euro 90 milioni

Fundi wa mpira kwenye kikosi cha Barcelona, Gavi hana mjadala juu ya ubora wa kiwango chake ndani ya uwanja. Soka la pasi hapo ndipo mahala pake na Gavi anawindwa na vigogo wengi. Thamani yake Euro 90 milioni.

20: Jude Bellingham – Euro 150 milioni

Real Madrid yenyewe ililipa pesa nyingi sana kunasa saini ya kiungo wa mpira, Jude Bellingham. Na baada ya kutua Bernabeu, kile ambacho amefanya hapo, kimepandisha thamani yake. Sokoni kwa sasa Jube ni Euro 150 milioni.

21: Josko Gvardiol – Euro 80 milioni

Ndiye beki mwenye thamani kubwa duniani kwa sasa. Gvardiol amezoea haraka Ligi Kuu England kama bata kwenye maji baada ya kujiunga na Manchester City. Staa huyo kwa sasa ukimtaka, thamani yake Euro 80 milioni.

22: Bukayo Saka – Euro 120 milioni

Saka amekuwa na wakati mzuri kwenye kikosi cha Arsenal.

Msimu uliopita alifunga mabao 14 kwenye Ligi Kuu England. Msimu huu ameanza na moto uleule na kufanya thamani yake kupanda. Ukimtaka Saka ni Euro 120 milioni.

23: Erling Haaland – Euro 180 milioni

Staa mwenye thamani kubwa kwenye soka kwa sasa. Straika huyo wa Manchester City, Haaland amekuwa na moto kwelikweli uwanjani, anafunga kama anavyotaka. Hilo limepandisha thamani yake, anauzwa Euro 180 milioni.

24: Kylian Mbappe – Euro 180 milioni

Haina ubishi ni mmoja wa wanasoka mahiri duniani kwa sasa. Fowadi huyo wa PSG amefunga mabao 224 katika mechi 272 alizotumikia klabu yake. Ubora wake wa uwanjani umemfanya kuwa na thamani ya Euro 180 milioni.

25: Federico Valverde – Euro 100 milioni

Valvede ni mchezaji muhimu sana kwenye kikosi cha Real Madrid na tayari ameshanyakua mataji kibao na timu hiyo. Makali yake uwanjani yanafanya thamani yake kuzidi kupanda huko sokoni, ukimtaka Euro 100 milioni.

26: Lautaro Martinez – Euro 100 milioni

Straika Lautaro Martinez amekuwa kwenye kiwango bora kwa miezi 18 iliyopita. Amekuwa na mchango mkubwa huko Inter Milan na hilo linafanya thamani yake kuwa kubwa sokoni, ambapo ukimtaka ni Euro 100 milioni.

27: Rodri – Euro 100 milioni

Mtu anayefanya Manchester City mambo yake kwenda sawa ndani ya uwanja. Huduma yake imekuwa muhimu kwelikweli kwenye kikosi hicho cha Pep Guardiola na jambo hilo limefanya thamani kwenda juu, Euro 100 milioni.

28: Jack Grealish & Joshua Kimmich – Euro 75 milioni

Hawa ni mastaa waliolingana umri na wamelingana pia thamani zao sokoni, ukitaka ni Euro 75 milioni. Mastaa hao ni Jack Grealish wa Manchester City na Joshua Kimmich anayekipiga kwenye kikosi cha Bayern Munich.

29: Bernardo Silva – Euro 80 milioni

Kama kuna wachezaji ambao Pep Guardiola anashukuru kuwa nao kwenye kikosi chake basi ni Bernardo Silva. Mreno huyo makali yake ni makubwa kwelikweli na hilo limemfanya awe na thamani ya Euro 80 milioni.

30: Harry Kane – Euro 110 milioni

Umri ni namba tu na hilo linathibitishwa na straika Harry Kane kwa kile anachokifanya kwenye timu yake mpya ya Bayern Munich. Kane anafunga tu na kufanya thamani yake kupanda zaidi, Euro 110 milioni kama utamhitaji.

31: Mohamed Salah – Euro 65 milioni

Kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, timu moja ya Saudi Arabia iliweka mezani Pauni 150 milioni kumsajili Mo Salah. Liverpool iligoma, lakini thamani yake mchezaji huyo ni Euro 65 milioni.

32: Kevin De Bruyne – Euro 70 milioni

Hajaonekana uwanjani muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi na huenda akaonekana Januari mwakani. Lakini, De Bruyne ni mchezaji mwenye thamani kubwa sokoni, ambapo ukimtaka ni Euro 70 milioni inahusika.

33: Ilkay Gundogan – Euro 20 milioni

Kwenye wachezaji wenye umri wa miaka 33, staa mwenye thamani kubwa sokoni ni kiungo wa Barcelona, Ilkay Gundogan. Staa huyo wa zamani wa Manchester City na Borussia Dortmund, thamani yake ni Euro 20 milioni.

34: Thomas Muller – Euro 12 milioni

Ametamba kwenye soka tangu akiwa na umri mdogo sana na hakika Muller ameliweka pazuri jina lake kwenye ramani za mchezo wa soka. Staa huyo anayekipiga Bayern Munich, thamani yake sokoni ni Euro 12 milioni.

35: Robert Lewandowski – Euro 30 milioni

Poland imekuwa imara kwenye soka la kimataifa kwa karibu muongo mmoja uliopita, lakini kwa sasa inapambana kufuzu Euro 2024 na hilo linatokena na Lewandowski umri kuanza kumtupa mkono. Thamani yake Euro 30 milioni.

36: Lionel Messi – Euro 35 milioni

Mshindi wa Ballon d’Or 2023, Lionel Messi umri wake kwa sasa ni miaka 36. Bado yupo vizuri uwanjani na kuifungia timu yake Inter Miami mabao ya kutosha yanayofanya thamani yake kuimarika, ukimtaka Euro 35 milioni.

37: Manuel Neuer – Euro 5 milioni

Amekuwa majeruhi na kukaa nje ya uwanja kwa miezi 10. Lakini, hakuna ubishi Neuer anatajwa kama mmoja wa makipa bora kabisa waliopata kutokea kwenye soka. Hata hivyo, umri umekwenda na thamani yake Euro 5 milioni.

38: Cristiano Ronaldo – Euro 15 milioni

Alishtua wengi baada ya kujiunga Al-Nassr, Desemba mwaka jana. Cristiano Ronaldo amekuwa na kiwango bora na kufunga mabao ya kutosha, lakini umri umefanya thamani yake ishuke, sokoni ni Euro 15 milioni tu.

39: Thiago Silva – Euro 2 milioni

Bado amekuwa mchezaji muhimu kwenye safu ya ulinzi ya Chelsea. Umri wake ni miaka 39, lakini shughuli yake ya uwanja ni pevu. Thiago Silva bado yupo fiti, licha ya thamani yake kushuka, Euro 2 milioni.

40: Claudio Bravo – Euro 1 milioni

Bravo alizichezea Barcelona, Manchester City na alikuwa muhimu sana Chile. Lakini, kila kitu kinakwenda na umri, kipa huyo kwa sasa ana umri wa miaka 40, mambo mengi yanakwama ikiwamo thamani kushuka, Euro 1 milioni.

Chanzo: Mwanaspoti