Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa waumizwa na kifo cha Yahya Akilimali, kuzikwa leo

Akilimali Pic Data Mastaa waumizwa na kifo cha Yahya Akilimali, kuzikwa leo

Sat, 30 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MASIKIO ya mastaa wa zamani wa Simba na Yanga, yalisita kuamini taarifa ya  kifo cha aliyekuwa winga teleza Yahya Akilimali, ambaye umauti umemkuta usiku wa kuamkia leo Jumamosi ya Oktoba 30, 2021 katika Hospital ya Mawenzi, Kigoma.

Baada ya mastaa hao kuhojiwa namna walivyomfahamu, Yahya wamesikitishwa na taarifa hiyo, wakishindwa la kufanya kwa kuwa Mungu hapangiwi kazi.

Kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Athuman Idd 'Chuji' ameshtushwa na kifo cha chake na ameshindwa cha kufanya zaidi ya kukubaliana na kazi ya Mungu, huku akiahidi kumuombea pumziko la amani.

Amesema hatawahi kumzika rafiki yake, kutokana na imani ya Kislamu kutolaza mwili wa marehemu, hivyo kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma hawezi kuwahi.

"Ni msiba mzito kwa sisi tuliyecheza naye, tutamuombea kwa Mwenyenzi Mungu apumzike kwa amani, nasikitika nitashindwa kwenda kumzika rafiki yangu, kwasababu Waislamu hawalazi mwili, hivyo atazikwa leo leo," amesema.

Kwa Ulimboka Mwakingwe aliyekuwa analala naye chumba kimoja wakiwa Simba, amepokea kifo chake kwa majonzi mazito na alipopewa yake alidhani ni sikukuu ya  wajinga duniani.

"Labda nithibitishe kwako mwandishi ni kweli Yahya hayupo, naumia sana, Simba nilikuwa nakaa naye chumba kimoja, kuna wakati nilikuwa nasingizia naumwa ama nimeumia ili mradi apate nafasi ya kucheza, alikuwa anatumia mguu wa kushoto, mimi nilikuwa nacheza miguu yote," amesema Ulimboka na ameongeza kuwa;

"Alikuwa mcheshi, mwenye nidhamu ya hali ya juu kwa wachezaji wenzake, kuna wakati nilikuwa namtuma kunifulia jezi na wala hakuwahi kulalamika, sijui niseme nini, itoshe kusema dunia tunapita, namuombea kwa Mungu apumzike kwa amani," amesema.

Amesema ameshindwa kwenda kumzika rafiki yake (Yahya), kutokana na kuwa Iringa kuuguza ndugu yake, anaiombea familia yake Mungu aipe  uvumilivu kipindi hiki.

Kwa upande wa Shaban Kisiga amesema kifo chake kinatoa funzo la kuishi vyema, kujua fumbo la Mwenyenzi Mungu, aliloliweka kwa wanadamu.

"Kuna wakati unaweza ukapokea taarifa ambazo hakutarajia kama hizi za mchezaji mwenzangu Yahya,tuliobakia tujifunze kuomba mwisho mwema kwani hatujui saa yetu," amesema. Klabu ya Simba imetuma salamu za pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki kufuatia kifo cha mchezaji wao huyo wa zamani.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz