Mashabiki wa Manchester United ni kama wamepewa zawadi ya Krismasi baada ya tajiri waliyekuwa wakisubiri kwa muda mrefu, Sir Jim Ratcliffe kuwekeza rasmi Old Trafford baada ya kununua asilimia 25 za hisa za umiliki wa klabu hiyo.
Sakata hilo limechukua miezi 13, ambapo ilifika wakati mashabiki walikata tamaa kwamba huenda jambo hilo lisingetimia. Lakini, ilipofika Desemba 24, siku moja kabla ya Krismasi, bilionea Ratcliffe aliweka mzigo kununua hisa hizo zenye thamani ya Pauni 1.3 bilioni.
Familia ya Glazer inayomiliki klabu ya Man United iliiweka sokoni timu hiyo mwaka mmoja uliopita, lakini ilishindwa kupata mnunuzi wa jumla, ambapo tajiri Ratcliffe na bilionea Sheikh Jassim walikuwa wakichuana kuinunua klabu hiyo.
Tajiri Ratcliffe yeye atahusika zaidi kwenye masuala ya kisoka - ikiwamo dili za usajili. Na sasa maswali yaliyopo ni kama mmiliki huyo mpya atawekeza kwenye usajili kunusuru hali ya mambo kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Mdachi, Erik ten Hag.
Kuhusu wachezaji wa kuwasajili, Man United imekuwa ikihusishwa na mastaa kibao, ambapo sasa kazi ya bilionea Ratcliffe itakuwa kutoa mkwanja tu kwenda kukamilisha dili za mastaa hao, akiwamo mmoja aliyewahi kukipiga kwa mafanikio katika kikosi hicho cha Old Trafford.
Victor Osimhen
Suala la kufunga mabao linaonekana kuwa tatizo kubwa Man United msimu huu, ambapo kwenye mechi 18 ilizocheza kwenye Ligi Kuu England, imefunga mabao 18. Man United ilitoa Pauni 72 milioni kunasa huduma ya straika, Rasmus Hojlund, lakini staa huyo wa Denmark ameshindwa kuonyesha makali. Hajafunga bao wala kutoa asisti hata moja kwenye ligi.
Hojlund hapewi huduma inayotosha kwa maana ya kupigiwa pasi kwa wingi na wachezaji wenzake, lakini tajiri Ratcliffe anaweza kufikiria kuleta straika mwingine wa kuja kuongeza makali haraka. Na Osimhen, 24, ni jina linalotajwa kwenye klabu hiyo kwa sasa, ambapo klabu hiyo alifunga mabao 31 katika mechi 39 alizocheza msimu uliopita kwenye Serie A. Huduma ya Osimhen itawagharimu pesa nyingi.
Frenkie de Jong
Straika Hojlund hawezi kulaumiwa kwa kushindwa kufunga mabao, kwa sababu hapewi pasi za kutosha, hasa kutoka kwa wachezaji wa pembeni na viungo. Kwa kifupi, Man United ina shida pia kwenye ubunifu wa eneo la kiungo yao.
Kiungo Scott McTominay ni kinara wa mabao wa timu hiyo msimu huu, lakini ameshindwa kuwatengenezea nafasi za kufunga wenzake. Kiungo wa Barcelona, De Jong, 26, amekuwa kwenye mipango ya Man United mrefu, ambapo kwenye dirisha lililopita walijaribu sana kumsajili wakakwama.
Lakini, kwa ujio wa tajiri Ratcliffe - mambo yanaweza kuwa tofauti na Man United ikafanikiwa kunasa saini ya mkali huyo wa zamani wa Ajax ili kuja kuongeza ubunifu kwenye eneo la kati la uwanja.
David de Gea
Aliondoka Man United mwishoni mwa msimu uliopita na ameacha tatizo kubwa kikosini. Man United imekuwa dhaifu sana golini baada ya kumsajili kipa Andre Onana kwa ada ya Pauni 47 milioni kutoka Inter Milan.
Kipa huyo Mcamerooni, Onana amekuwa na makosa mengi yaliyoigharimu timu kwenye michuano mingi tofauti ikiwamo Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kitu kingine, Onana atakosekana Januari, akitarajiwa kwenda kujiunga na timu yake ya taifa ya Cameroon kucheza michuano ya Afcon 2024.
Hivyo, Man United inaweza kushawishika kusajili kipa na hapo Ratcliffe anaweza kumrudisha De Gea na kumpa anachokitaka ili aokoe jahazi. Uzuri De Gea bado mchezaji huru hajapata timu hadi sasa.
Serge Gnabry
Man United inahitaji winga kwa nguvu zote. Straika wao, Hojlund ni kama amekuwa ametengwa kisiwani kutokana na mawinga waliopo Man United kwa sasa kushindwa kumchezesha.
Wachambuzi wa soka wamekubaliana kwamba Hojlund hapaswi kubeba lawama na badala yake hilo lielekezwe kwa mawinga Anthony, Alejandro Garnacho na wengine kushindwa kumchezesha straika huyo.
Mawinga hao wawili, wamempigia pasi sita tu Hojlund hadi kufika sasa, hivyo Ratcliffe atashawishika kuingia sokoni kunasa winga mpya na chaguo la kwanza ni mkali wa Bayern Munich, Gnabry. Man United itakuwa kwenye mikono salama ikifanikiwa kunasa saini ya Gnabry hasa kwa kipindi hiki Jadon Sancho akitarajia kuondoka.
Goncalo Inacio
Je, beki ni tatizo Man United? Si sana. Man United ina mabeki wengi wa kiwango cha dunia, akiwamo Raphael Varane. Veterani Jonny Evans na kinda Willy Kambwala walianzishwa kwenye kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya West Ham United, Jumamosi iliyopita kutokana na mabeki wengi wa kikosi hicho kuwa majeruhi.
Harry Maguire alionyesha kiwango kizuri kwenye kikosi cha kwanza na kuchaguliwa Mchezaji Bora wa Mwezi Novemba, lakini kwa sasa ni majeruhi. Na sasa, Man United inahitaji huduma ya staa wa Sporting Lisbon, Inacio, 22, ambaye mkataba wake una kipengele kinahitaji kulipa Pauni 50 milioni tu ili kuvunja na kunasa saini yake. Skauti wa Man United wamekwenda Lisbon kumfuatilia Mreno huyo.