Baadhi ya washambuliaji wa zamani wamechambua mabadiliko ya kanuni ya 11 inayohusu vikombe na tuzo kipengele cha 12 na 13 cha mfungaji bora wa mashindano msimu huu.
Katika mabadiliko hayo Mfungaji akifunga bao la kawaida anakuwa na pointi mbili, huku atakayefunga la penalti anayo moja tofauti na msimu uliopita mabao yote yalihesabiwa sawa.
Hii ina maana kuwa mchezaji atakayefunga mabao mengi ya penalti akilingana na aliyefunga yale ya kawaida mwenye mabao ya kawaida atakuwa na nafasi kubwa ya kutangazwa mfungaji bora.
Msimu uliopita, washambuliaji wawili Saido wa Simba na Fiston Mayele walifungana na wote kupewa tuzo ya ufungaji bora licha ya kwamba baadhi walitaka apewe Mayele kwa kuwa Saido alikuwa na mabao mengi ya penalti.
Washambuliaji wa zamani wamesema hawaoni kama ni sawa kutenganisha aina hiyo ya mabao wakidai yote ni mabao. Mshambuliaji wa zamani Simba, Bakari Kigodeko alisema: “Mtu aliyekosa penalti ndiye huathirika zaidi kuliko aliyekosa kawaida. Watu watamsema (aliyekosa penalti) na anaweza akatoka mchezoni kabisa. Kwa hiyo nadhani kusingekuwa na tofauti yangekuwa sawa tu,” alisema Kigodeko.