Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa wanotajwa kunyakua tuzo ya mchezaji bora

Haaland Rash Saka Mastaa wanotajwa kunyakua tuzo ya mchezaji bora

Fri, 14 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Nani, Bukayo Saka au Marcus Rashford? Martin Odegaard au Kevin De Bruyne?

Wanatajwa wengi na wote ni vichwa.

Erling Haaland, Casemiro, Jack Grealish, Leandro Trossard, Gabriel Martinelli na Harry Kane. Kuna mmoja tu hapo, ndiye anayestahili kuvikwa taji la kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Kulipwa kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Unaambiwa hivi, sare iliyopata Arsenal dhidi ya Liverpool kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu England uwanjani Anfield, umetibua matumaini ya Saka kuibuka kidedea kwenye kinyang'anyiro cha mchezaji bora wa mwaka, ambapo sasa ameshuka kutoka nafasi ya tatu hadi ya sita kwenye orodha ya wachezaji wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda.

Kwa mujibu wa wacheza kamari, hawa hapa mastaa 10 kulingana na namba walizowekwa ndio nafasi wanazopewa kwenye mchakamchaka huo wa kumpata mchezaji bora wa mwaka kwenye ligi hiyo yenye ushabiki mkubwa duniani.

1) Erling Haaland

Mambo yalivyo kwa sasa, straika wa Manchester City, Erling Haaland ndiye anayepewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Ligi Kuu England.

Amewekwa kwenye namba moja na hakika mavitu yake yanabainisha kila kitu. Haaland amefunga mabao 30 katika mechi 27 alizocheza kwenye ligi, ameasisti mara tano na amepiga mashuti 77.

2) Martin Odegaard

Arsenal ipo vizuri msimu huu, lakini kwa namna kubwa hilo linachangiwa na kiungo mshambuliaji na nahodha wao, Martin Odegaard. Chama hilo la kocha Mikel Arteta linaongoza msimamo wa ligi dhidi ya Manchester City kwa tofauti ya pointi sita, lakini Odegaard amekuwa bora kabisa uwanjani. Amefunga mabao 10 na kuasisti mara saba katika mechi 29 alizocheza, huku akiwa amepiga mashuti 46.

3) Marcus Rashford

Tangu arudi kutoka Qatar kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022, Marcus Rashford amekuwa kwenye kiwango bora kwelikweli huko Manchester United.

Mabao yake yamekuwa na faida kubwa katika kikosi cha Erik ten Hag na ndio maana anapewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo ya mwaka huu. Rashford amefunga mabao 15, asisti nne katika mechi 29, huku akiwa amepiga mashuti 59 kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

4) Kevin de Bruyne

Hata katika msimu ambao hayupo kwenye ubora wake huko Manchester City, Kevin de Bruyne bado ameendelea kuwa mjadala.

Hakuna mchezaji aliyewahi kushinda tuzo ya PFA zaidi ya mara mbili na De Bruyne anataka kuwapiku Mo Salah, Gareth Bale, Cristiano Ronaldo, Thierry Henry, Alan Shearer na Mark Hughes kwenye ishu hiyo. KDB amefunga mabao matano, asisti 14 katika mechi 27 huku akitengeneza nafasi 74 za mashambulizi.

5) Harry Kane

Straika, Harry Kane mara zote amekuwa akijitolea kwa kadri ya uwezo wake katika kuisaidia Tottenham Hotspur, lakini shida timu hiyo haishindi mataji.

Kwenye Ligi Kuu England msimu huu, Kane amefunga mabao 23 na kuasisti mara mbili katika mechi 30 alizocheza, ambapo pia amepiga mashuti 79. Kane yupo kwenye namba tano katika orodha ya wachezaji wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo ya ubora wa ligi ya England msimu huu.

6) Bukayo Saka

Kinda matata wa Arsenal, Bukayo Saka amekuwa kwenye kiwango bora kabisa msimu huu na mchango wake wa uwanjani umekuwa na faida kubwa kwa kocha Mikel Arteta.

Kwenye ligi hiyo, Saka amefunga mabao 12 na kuasisti mara 10 katika mechi 30 alizocheza, huku akipiga mashuti 45. Saka ametengeneza nafasi 54 na pasi sahihi 803. Awali alikuwa akishika namba tatu kwenye uwezekano wa kubeba tuzo hiyo ya England.

7) Gabriel Martinelli

Ubora wa Arsenal kwenye Ligi Kuu England msimu huu ndio unaowafanya wawe na orodha ya wachezaji wengi wanaofukuzia tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa England.

Mbrazili, Gabriel Martinelli amekuwa kwenye ubora mkubwa, akifunga mabao 14 na kuasisti mara nne katika mechi 30 na amepiga mashuti 49. Kama Arsenal itanyakua taji la ligi msimu huu, basi Martinelli mchango wake utakuwa mkubwa sana kwenye kikosi hicho.

8) Leandro Trossard

Ametua Emirates kwenye dirisha la Januari na hakika tangu alipotua Arsenal mchezaji huyo amekuwa muhimu kwelikweli kwenye kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta.

Staa huyo amehusika kwenye mabao 17, akifunga mara nane na kuasisti tisa katika mechi 27 alizocheza kwa ujumla tangu akiwa Brighton na sasa Arsenal. Amepiga mashuti 32, huku akitengeneza nafasi 29 na amepiga pasi 702, huku sahihi zilizofikia watu ni 543.

9) Jack Grealish

Mchezaji ghali kabisa Ligi Kuu England, Jack Grealish amefunga mabao manne na kuasisti mara tisa katika mechi 21 za mwisho alizochezea klabu yake ya Manchester City.

Lakini, mkali huyo amefunga mabao matano na kuasisti sita kwenye mechi 23 alizocheza kwenye Ligi Kuu England. Ametengeneza nafasi 35 na kupiga pasi sahihi 730 kutoka pasi za jumla 830 alizopiga. Hiyo ina maana, pasi 100 tu ndizo ziliharibika.

10) Casemiro

Pengo la kiungo wa Kibrazili, Casemiro limeonekana bayana kwenye kikosi cha Manchester United kwa mechi zote ambazo hakucheza.

Mchezaji huyo amekuwa muhimu kwenye timu hiyo tangu alipojiunga mwaka jana, akiwasaidia kuwa washindani kwenye mataji mengi, ambapo kwa sasa wanafukuzia Kombe la FA na Europa League, huku tayari wakiwa wameshabeba Kombe la Ligi. Man United inasaka nafasi pia ya kucheza Ulaya msimu ujao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: