Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa wamlilia Dk Mwankemwa

Daktari Wa Azam FC Afariki Dunia Aliyekuwa Kocha wa Azam FC, Dk Mwanandi Mwankemwa

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mwili wa aliyekuwa Kocha wa Azam FC, Dk Mwanandi Mwankemwa unatarajiwa kuzikwa leo Alhamisi, Februari 29, 2024 katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam huku mastaa mbalimbali wa soka wakiendelea kumlilia na wengine kueleza namna kifo chake kilivyowagusa kwa jinsi alivyokuwa kama baba katika suala la matibabu.

Dk Mwankemwa alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Temeke huku chanzo cha kifo chake kikiwa bado hakijafahamika na anatarajiwa kuzikwa leo mara baada ya swala ya alasiri msiba wake ukiwaliza wengi ilhali baadhi ya wachezaji wakieleza jinsi alivyowagusa kwa namna moja au nyingine enzi za uhai wake.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wamesema wamempoteza mshauri, mzazi na daktari kwenye masuala ya soka.

Beki wa Azam FC, Abdallah Kheri 'Sebo' amesema amepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mwankemwa ambaye mbali na kusimama naye kila alipokuwa anapata matatizo, alikuwa ni mzazi kwake na mara baada ya kuambiwa amefariki dunia alijaribu kupiga simu yake kwanza.

"Nimepokea taarifa kwa mshtuko na nikawa siamini nikashika simu yangu na kumpigia simu yake haikuita na sio kawaida ndipo nilipoamini kama hatupo naye tena," amesema.

"Nimesafiri na Mwankemwa mara mbili akinipeleka nje ya nchi kwa ajili ya matibabu zaidi na alikuwa mzazi kwangu kwa kunipa ushauri namna natakiwa kujitunza, simu zake zilikuwa hazikatiki nje ya matibabu alikuwa mshauri mzuri wa maisha yangu binafsi."

Kiungo wa zamani wa Azam anayekipiga kwa sasa timu ya Tala'ea El Gaish SC nchini Misri, Himid Mao amesema kama wanasoka wamepoteza mtu muhimu.

"Sio daktari tu alikuwa kiongozi, mlezi na baba yetu sote ni njia moja tunachotakiwa ni kumuombea apumzike kwa amani," amesema Mao, huku mshambuliaji wa Azam, Prince Dube akisema ameshtushwa na taarifa za kifo cha Mwankemwa ambaye amemtaja kama mzazi.

"Ilikuwa taarifa ngumu sana kwangu kuipokea ndiye daktari ambaye amesimamia matibabu yangu ya mara kwa mara na amekuwa akinisimamia hata kipindi nikiwa kwenye hali nzuri kwa kunipa programu za kufanya ili niwe imara," amesema.

Winga wa zamani wa Yanga, Simba na Azam FC, Mrisho Ngassa amesema alikuwa sio daktari tu, bali mzazi kutokana na namna alivyokuwa anaishi na wachezaji huku akikiri kuwa sio kwa walio ndani ya timu iliyomuajiri tu.

"Mimi nimepita Azam miaka ya nyuma, lakini nikiwa na tatizo hata nilipotoka kwenye timu hiyo mtu wa kwanza kumtafuta alikuwa yeye ananipa ushauri kwa simu au ananiambia nimtafute tuonane ajue tatizo kwa karibu," amesema Ngassa kinara wa mabao wa timu ya taifa, Taifa Stars, akifunga mabao 25 katika mechi 100.

Wachezaji wengine walioumizwa na kifo cha Dk Mwankemwa ni nahodha wa Simba, Mohammed Hussein 'Tshabalala'; kiraka Novatus Dismas, Kenneth Muguna, Waziri Junior, Kipre Tchetche.

Chanzo: Mwanaspoti