Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa walioteswa na Msuva Afcon

Msuva Mateso AFCON Mastaa walioteswa na Msuva Afcon

Tue, 6 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ni ndoto za wachezaji wengi wa mataifa mbalimbali barani humu kushiriki fainali za mataifa ya Afrika kutokana na mashindano hayo kuwa yenye thamani na mvuto mkubwa zaidi kisoka kulinganisha na mengine.

Lakini huwa ni jambo la fahari zaidi kwa mchezaji kufunga bao kwenye mashindano hayo ambayo hufanyika kila baada ya miaka miwili kutokana na ugumu uliopo kwa wachezaji wengi kufumania nyavu katika Afcon kwa nyakati tofauti.

Nyota wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Saimon Msuva anaweza kuwa mchezaji wa Kitanzania aliyeweka alama kubwa katika fainali za Afcon kwa kufunga mabao mawili tena katika awamu mbili tofauti za mashindano hayo, jambo ambalo halijawahi kufanywa na mwingine yeyote katika ushiriki wa Taifa Stars kwenye mashindano hayo.

Msuva alifunga bao la kwanza kwenye fainali za Afcon mwaka 2019 katika mchezo dhidi ya Kenya ambao Taifa Stars ilipoteza kwa mabao 3-2 na kisha akafunga katika fainali zinazoendelea huko Ivory Coast katika mechi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Zambia.

Inawezekana mabao mawili ya Msuva kwenye Afcon ni machache lakini kuna idadi kubwa ya wachezaji ambao hawajawahi kufikisha na Spoti Mikiki inakuletea orodha ya nyota wa Afrika wenye majina makubwa katika soka ambao hawakuweza kufanya kile ambacho nyota huyo wa Taifa Stars amekifanya kwenye fainali hizo.

Hakim Ziyech

Pamoja na kuchezea timu kubwa barani Ulaya kama Chelsea, Ajax na Galatasaray, winga huyo ameifungia Morocco bao moja tu kwenye Afcon ambalo alipachika dhidi ya Zambia katika fainali za mwaka huu.

Selim Amallah

Alikuwa miongoni mwa nyota wa Morocco waliotoa mchango katika kuifanya timu hiyo kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2022 lakini amefunga bao moja tu katika Afcon.

Kwesi Appiah

Nyota huyo wa zamani wa Ghana amefunga bao moja tu kwenye Afcon ambapo ilikuwa ni mwaka 2015.

Modibo Maiga

Ukitaka kuamini kuwa alichokifanya Msuva sio kitu chepesi, mlinganishe na mshambuliaji wa Mali, modibo Maiga ambaye licha ya kushiriki Afcon mara nne tofauti, alifunga bao moja tu.

Christian Bassogog

Nyota wa Cameroon, Christian Bassogo licha ya kucheza fainali tatu tofauti za Afcon, amepachika bao moja tu.

Keita Balde

Bao moja ambalo Keita Balde amefunga katika awamu mbili tofauti za Afcon zinamfanya awe mnyonge wa Msuva kwenye fainali hizo.

Philemon Masinga

Marehemu Philemon Masinga anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji bora waliowahi kuitumikia timu ya taifa ya Afrika Kusini 'Bafana Bfana' lakini pamoja na hilo, alifunga bao moja tu kwenye Afcon.

Achille Emana

Katika Afcon, nyota wa zamani wa Cameroon, Achille Emana alipachika bao moja.

Julio Tavares

Staa wa zamani wa timu ya taifa ya Cape Verde, Julio Tavares, amefunga bao moja kwenye Afcon hivyo Msuva ni mbabe mbele yake.

Patson Daka

Licha ya kutamba akiwa na Leicester City, huku kwenye Afcon hana jeuri mbele ya Msuva kwani ana bao moja tu ambalo amelifunga.

Ismael Bangoura

Nyota wa zamani wa Guinea, Ismail Bangoura ameachwa na Msuva kwa bao moja kwenye Afcon licha ya kuwahi kuwa tegemeo kubwa kwa taifa lake.

Mame Diouf

Alipata umaarufu alipojiunga na Manchester United mwaka 2009 lakini pamoja na hilo, timu yake ya taifa ya Senegal ameifungia bao moja tu kwenye Afcon.

Brown Ideye

Bao lake moja alilofunga kwenye Afcon linampa unyonge mbele ya Msuva mwenye mawili.

Emmanuel Adebayor

Licha ya kung'aa akiwa na Arsenal na Manchester City, Adebayor ameifungia Togo, bao moja tu kwenye Afcon.

Cheik Tiote

Marehemu Cheik Tiote aliifungia Ivory Coast bao moja katika awamu tofauti alizocheza katika mashindano hayo.

Kelechi Iheanacho

Sio miongoni mwa nyota wa Nigeria waliopo Afcon mwaka huu na pengine hiyo imechangia asiongeze bao/mabao hivyo amesalia na bao lake moja alilopachika akiwa na kikosi cha timu yake ya taifa kwenye mashindano hayo.

Finidi George

Anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji bora kuwahi kutokea Nigeria lakini amefunga bao moja tu kwenye Afcon

Arouna Kone

Mshambuliaji Arouna Kone licha ya kucheza Afcon kwa nyakati tofauti, ana bao moja kwenye Afcon akiwa na jezi ya Ivory Coast.

Yannick Bolasie

Alitamba akiwa na kikosi cha Everton lakini kwenye Afcon ana bao moja akizidiwa na Msuva.

Nonda Shaban

Staa wa zamani wa Yanga, Nonda Shaban yeye ana bao moja tu kwenye Afcon.

Chanzo: Mwanaspoti