Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa waliokanyaga Kwa Mkapa

Didier Drogba Didier Drogba

Wed, 18 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Oktoba 20 Simba itautumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mara ya kwanza baada ya kufanyika maboresho katika maeneo mbalimbali.

Simba itacheza mchezo wa ufunguzi wa mashindano ya African Football League dhidi ya Al Ahly maboresho hayo yatakapokamilika kabla ya mchezo huo.

Hadi sasa ni takriban miaka 15 tangu kuzinduliwa kwa uwanja huo unaoingiza mashabiki 60,000 na mastaa wengi wakubwa wamecheza kwenye uwanja huo wakiziwakilisha nchi zao au klabu zao.

YAYA TOURE/DIDIER DROGBA NA IVORY COAST YAO

Mastaa hawa walikanyaga uwanja wa Mkapa kwa nyakati tofauti. Januari 2010, Drogba alikuja na timu ya taifa ya Ivory Coast kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Tanzania na kushinda bao 1-0.

Toure alicheza kwenye uwanja huo Juni 2013, mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia na Ivory Coast iliibuka na ushindi wa mabao 4-2, kwa mabao ya Lacina Traore, Yaya Toure mawili na Wilfried Bony, huku mabao ya Tanzania yakifungwa na Amri Kihemba na Thomas Ulimwengu.

Toure na Drogba waliambatana na mastaa wengine kama Solomon Kalou, Gervais Gervinho, Didier Zokora, Gervais Yao na Kolo Toure kwenye mchezo huo.

MBWANA SAMATTA

Kwa Mkapa ni nyumbani, alianza kukanyaga akiwa nchini kabla ya kutimkia ughaibuni anakokipiga soka la kimataifa.

Aliichezea Simba na kwenye uwanja huo ndiko alikoonekana na TP Mazembe na kwenda kucheza Ligi ya Condo kabla ya kwenda Ulaya.

Uwanja huo pia ameukanyaga akiwa na timu ya Taifa, Taifa Stars kwenye mechi mbalimbali.

Kwa sasa anakipiga klabu ya Paok ya Ugiriki ingawa amepita kwenye timu nyingine kubwa ikiwamo Aston Villa ya Ligi Kuu England, Genk na Royal Antwerp za Ubelgiji, Fenerbahce ya Uturuki na sasa Paok.

WAYNE ROONEY

Utawaambia nini mashabiki wa Manchester United kwa staa wao huyu.

Bao lake la umbali wa mita 20 alilofunga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa akiwa na Everton dhidi ya Gor Mahia ya Kenya kwenye mchezo wa fainali ya Sportpesa Super Cup mwaka 2017 bado linakumbukwa na mashabiki wa soka Afrika Mashariki na hasa Tanzania kwa waliofika uwanja huo kushuhudia mchezo huo.

Amecheza kwa mafanikio makubwa kwenye soka lake akiwa na Everton kabla ya kutua Man United iliyompa jina akiichezea kwa misimu 13 kisha akahamia Marekani na sasa ni kocha.

Rooney aliambatana na mastaa wengine katika timu hiyo akiwemo Phil Jagielka, Morgan Schneiderlin, Gylfi Sigurdsson, Cuco Martine na wengineo.

LUIS FIGO

Mwaka 2014, mastaa waliokipiga Real Madrid miaka ya nyuma walikuja Tanzania na kucheza mchezo wa kirafiki na wachezaji wa zamani wa Taifa Stars ‘Tanzania Eleven’ mchezo uliomalizika kwa wageni hao kushinda mabao 3-1.

Staa wa kikosi hicho alikuwa Luis Figo aliyeambatana na wenzake wengi waliokuwa kivutio katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam na kutandaza soka safi kabisa.

Mabao ya Real Madrid, yote matatu yalifungwa na Ruben de la Red na bao la Tanzania lilifungwa na Roberto Rojas ambaye alijifunga.

Figo aliambatana na wachezaji wenzake wa zamani akiwemo mkali Christian Karembeu na wengine wengi walioshuhudiwa na Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete.

RICARDO KAKA

Alitamba sana na timu ya Taifa ya Brazil na klabu ya AC Milan ya Ligi Kuu ya Italia, Serie A.

Kwa sasa amestaafu soka na anaendelea na maisha mengine.

Alikanyaga Uwanja wa Mkapa akiwa na timu ya Taifa ya Brazil iliyokuwa njiani kwenda Afrika Kusini kwenye Fainali za Kombe la Dunia June, 2010.

Katika mchezo huo wa kirafiki, Brazil ilishinda mabao 5-1 kwa mabao ya Robinho mawili, Ramires mawili na Kaka moja, huku la Stars likifungwa na Jabir Aziz.

Mastaa wengine katika kikosi hicho walikuwa Michael Bastan, Gilberto Silva, Luis Fabiano, Julio Cesar, Felipe Melo na wengineo.

EVER BANEGA

Alitua Uwanja wa Mkapa akiwa na Sevilla ya Ligi Kuu ya Hispania, La Liga.

Ni kiungo mshambuliaji wa timu ya taifa ya Argentina na kwenye mchezo huo ulioandaliwa na Sportpesa dhidi ya Simba iliyokuwa ikidhaminiwa na kampuni hiyo, Sevilla ilishinda mabao 5-4.

Mabao ya Simba yalifungwa na John Bocco mawili, Meddie Kagere na Clatous Chama.

Mastaa wenzake waliokuja siku hiyo walikuwepo Alex Vidal, Ben Yedder, Jesus Navas, Roque Mesa, Sergi Gomez, Juna Soriano na wengine wengi.

SAMUEL ETOO

Ni jina lingine kubwa duniani lililowahi kukanyaga Uwanja wa Mkapa.

Hakuna asiyemfahamu rais huyu wa sasa wa Shirikisho la Soka Cameroon (Fecafoot) baada ya kustaafu soka.

Amepita timu nyingi kubwa zikiwamo Real Madrid, Barcelona, Chelsea na Everton na kutengenza jina na ujio wake Tanzania ilikuwa ni moja ya vivutio kwa watazamaji.

Cameroon ilicheza mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Tanzania Juni 2008 ikiwa ni mwaka mmoja tangu ufunguliwe uwanja huo mwaka 2007.

Kwenye mchezo huo timu hizo zilitoka suluhu na aliambatana na mastaa wengine wa nchi hiyo na waliotamba duniani kama Jean Makoun, Stephane Mbia, Pierre Webo, Alex Song, Rigobert Song, Andre Bikey, Allan Nkong na wengine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live