Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa walio-trend mwaka 2023

Fei Toto Mastaa walio-trend mwaka 2023

Fri, 15 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mwaka 2023 ndiyo unaisha hivyo huku kwenye tasnia ya soka mambo mengi yakiwa yametokea.

Kuna wachezaji ambao mwaka huu wamezungumzwa, kutazamwa na kuandikwa sana kutokana na matukio mbalimbali waliyoyafanya na Mwanaspoti kupitia makala haya linakuletea wachezaji waliowika zaidi nchini katika soka kwa mwaka huu.

FEISAL SALUM ‘FEI TOTO’

Staa huyu anayekipiga Azam FC kwa sasa, mwaka huu ulikuwa wa hekaheka nyingi kwake lakini baadaye aliyashinda majaribu.

Fei alianza mwaka akiwa na kesi iliyomuhusisha na waliokuwa waajiri wake wa zamani, Yanga kutokana na kitendo chake cha kuondoka kikosini hapo kinyume na utaratibu na kesi kubwa kuunguruma baina ya pande zote hizo, huku wanasheria wakibishana kuhusiana na vipengele vya mikataba.

Baada ya zaidi ya miezi sita ya kesi hiyo, Juni 8, mwaka huu Yanga ilikubali yaishe baada ya kupata maagizo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Yanga iliamua kuachana na kesi hiyo huku akimtaka Fei Toto alipe stahiki zote jambo alilolifanya kisha kuuzwa kwa Azam FC, sasa amekuwa akiwika kweli kweli huku hadi sasa akifunga mabao saba kwenye timu hiyo iliyopo kileleni na kutoa pasi nne zilizozaa mabao.

MAHLATSE MAKUDUBELA ‘SKUDU’

Julai 16 mwaka huu saa sita usiku Yanga ilimtambulisha winga Skudu kutoka kwenye kikosi cha Marumo Gallants cha Afrika Kusini kama mchezaji wake mpya na kukabidhiwa jezi namba sita iliyokuwa ikivaliwa na Fei Toto aliyetimkia Azam.

Skudu alianza kutrendi kabla hatayeye mwenyewe kutua nchini kwani Ofisa habari wa Yanga, Ally Kamwe alitumia mitandao yake ya kijamii na ile ya Yanga kuinadi jezi namba sita akitamba kuwa mchezaji atakayekabidhiwa atakuwa hatari sana.

Mashabiki wa soka nchini bila kujua ni nani huku wakihisi wachezaji tofauti, walizidi kuwa na shauku kutaka kujua huyo ‘namba sita’ atakuwa nani na mwisho wa siku akaibuka Skudu.

Utambulisho wa Skudu uliambatana na ngoma mpya ya Yanga yenye mahadhi ya ‘Amapiano’, muziki wenye asili ya Afrika Kusini anakotoka Skudu, ukiimbwa na supastaa Juma Jux na kucheza kwa pamoja na Skudu.

Jambo lingine lililomfanya mwamba huyo kutrendi ni aina yake ya uchezaji ‘Shibobo’ ambayo ni moja ya utamaduni wa wachezaji wa Afrika Kusini, hata hivyo, bado ameendelea kuwa gumzo kwa kuwa ameshindwa kupata nafasi uwanjani.

LUIS MIQUISSONE ‘KONDE BOY’

Baada ya kusubiriwa kwa misimu miwili mfululizo na tetesi nyingi kuzagaa za kiungo mshambuliaji wa Simba, Luis Miquissone raia wa Msumbiji kurejea katika timu hiyo.

Kiungo huyo alikuwa staa wa mwisho kutambulishwa ndani ya kikosi cha Simba dirisha kubwa la usajili msimu huu baada ya kufanikiwa kuvunja mkataba na Mabingwa wa Soka Barani Afrika Al Ahly ya Misri.

Luis aliondoka Simba SC miaka miwili iliyopita akisajili Al Ahly, baada ya kuonesha uwezo mkubwa katika  Ligi ya Mabingwa Afrika, akiifunga bao pekee na la ushindi katika mchezo wa mzunguko wa pili hatua ya makundi msimu wa 2020/21.

Staa huyo alianza kuzungumzwa zaidi kabla hata ya kutua nchini huku dau lake la mshahara likitajwa kuwa kubwa zaidi na wadau wengi kuhofia kama ataweza kutua nchini hadi pale alipotambulishwa na sasa anakipiga Simba tayari amehusika kwenye mabao matatu kati ya mechi tisa zilizochezwa na timu hiyo, lakini ameendelea kuwa gumzo baada ya kukosa nafasi ya kudumu kwenye kikosi hicho.

CLARA LUVANGA

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga Princess na Timu ya Taifa Chini ya Umri wa Miaka 18, Clara Luvanga ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa Saudi Arabia amekuwa kwenye vichwa vya habari msimu huu baada ya kukosekana kwenye kikosi cha Timu ya Taifa kilichofuzu Kombe la Mataifa Afrika kwa Wanawake (WAFCON).

Clara anayekipiga Al Nasr ya Saudia inayoshiriki Ligi Kuu, hadi sasa amefunga mabao sita kwenye mechi tano akiwa ni mmoja ya nyota tegemeo wa timu hiyo, lakini jina lake halikuwepo kwenye kikosi cha Twiga, mashabiki na wadau walihoji hadi kumuibua kocha wa timu hiyo ya taifa ambaye alikosa majibu.

“Hakuna aliyekuwa anamjua Clara, mimi ndiye niliyemuibua nilipomtoa nikaamini uwezo wake na kumfundisha hadi akawa vile na kuisaidia timu kukata tiketi ya Kombe la Dunia U17 zilizopita.

“Mimi ndiye ninayejua ninachokihitaji katika timu ili kupata matokeo, naumia nikisikia watu wanaongelea ishu hiyo, halafu watu hawajui, mimi ndiye niliyempeleka Saudia,” alisema Shime bila kufafanua kilichomfanya asimuite.

CLATOUS CHAMA

Ni mmoja kati ya wachezaji wenye mchango mkubwa msimu uliopita ndani ya kikosi cha Simba na ilikuwa ukitaka kugombana na mashabiki wa Lunyasi, mguse Mwamba wa Lusaka walikuwa hawataki kabisa kusikia chochote kibaya kumuhusu akiifungia timu yake mabao saba na kutoa asisti 14.

Hali hiyo iliendelea hadi mwanzoni mwa msimu huu chini ya Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kabla hajafurushiwa virago alimtoa kwenye moja ya mechi na mashabiki wakamjia juu wakimtaka amtumie jambo ambalo lilimfanya azungumzwe sana. Ufalme wa mchezaji huyo umeanza kupotea kidogokidogo ndani ya kikosi hicho kwani sasa amekuwa sio mchezaji ambaye anapiganiwa kama ilivyokuwa awali.

MOSES PHIRI

Msimu uliopita alifunga mabao 10 kabla ya kuumia na kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu. Akiwa chini ya Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambaye aliibuka na kuzungumza sababu za kutomtumia kuwa bado hajawa fiti kutokana na kutoka kuuguza majeraha lakini wadau wa soka walipaza sauti wakitaka kuona anatumika. Hata baada ya ujio wa kocha mpya, Abdelhak Benchikha bado Phiri hajapata nafasi kikosi cha kwanza na anatumika kama mchezji wa akiba.

FISTON MAYELE

Alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga hii ni baada ya ubora aliouonyesha ndani ya kikosi hicho kabla ya kutimkia Pyramids FC ya Misri.

Alikuwa kinara wa upachikaji wa mabao ndani ya kikosi hicho msimu uliopita akifunga mabao 17 na kuisaidia timu yake kufika fainali Kombe la Shirikisho Afrika, akifunga mabao manane aliondoka Yanga akiwa bado anahitajika.

AISHI MANULA

Tanzania One ndio jina alilopewa kutokana na ubora wake awapo langoni taa yake mdogo mdogo inazima hii ni baada ya kupata majeraha ya nyonga msimu uliopita ambao alicheza nusu. Kuumia kwake kumewafanya Simba imsajili Ayoub Lakred ambaye ndiye amekuwa msaada kwa timu hiyo kwa sasa, msimu huu alirudi kwa kuanza mazoezi mepesi.

Licha ya mashabiki na wadau wa soka kufurahia kurudi kwake akianza na mechi ya watani Manula alipigwa na kitu kizito akikubali kuruhusu mabao 5-1 dhidi ya Yanga matokeo ambayo yamemuondoa langoni tena hadi sasa kwenye timu hiyo.

STEPHANE AZIZ KI

Ni kiungo aliyetrendi aliposajiliwa akitokea Asec Mimosas na kujiunga Yanga kwa mkataba wa miaka miwili usajili wake ulikuwa gumzo na alitangazwa usiku wa manane.

Msimu huu amekuwa bora na anaonyesha ubora ule yuliokuwa unatarajiwa na wadau wengi wa soka kutokana na gharama kubwa aliyosajiliwa alipojiunga amerudi midomoni mwa wadau wa soka ni staa ambaye amefunga hat-trick ndani ya kikosi cha Yanga akiifunga Azam FC na ndiye kinara wa mabao akifunga mabao saba sawa na Maxi Mzingeli, akiwa sawa na Pacome Zouzoa, Aziz Ki pamoja na Baleke.

Chanzo: Mwanaspoti